IKIWA ni takribani miezi miwili imesalia kuumaliza mwaka 2021, ambapo mara nyingi utaratibu wa wasanii wengi kote duniani katika kipindi kama hiki huandaa matamasha maalum ya funga mwaka ambayo kwa hapa nyumbani Tanzania wasanii wengi wamekuwa wakichagua kurejea katika maeneo waliyotokea kwa ajili ya kwenda kusambaza burudani ya shukurani kwa kuandaa matamasha na hafla za kutoa misaada kwa wahitaji.
Kutoka Lebo ya Konde Music Worldwide ya muziki iliyo chini ya msanii Harmonize, Hatimaye wamerejea na taarifa ya ujio wa tamasha la kwanza maalumu kwa ajili ya msanii wao wa kwanza kusainiwa chini ya Lebel hiyo, Ibraah ambaye atapiga tamasha maalumu la funga mwaka litakalofanyika nyumbani kwao mkoani Mtwara, Novemba 27, mwaka huu 2021.
Kwa mujibu wa msanii Ibraah mwenyewe ameweka wazi mapokezi ya taarifa za mpango huo ulioandaliwa na uongozi wake kuhusu kurudi kutoa shukrani kwa kuwaburudisha wananchi wa mkoa wa Mtwara ikiwa ni sehemu ya shukrani kwa kuendelea kumuunga mkono katika mapambo ya kupeleka mbali muziki wake.
"Ni takribani mwaka mmoja sasa toka nimeanza kufahamika kwenye kiwanda hiki cha muziki wa kizazi kipya na ndoto yangu kubwa ilikua siku moja niweze kufanya show kubwa nyumbani sehemu ambayo imenilea na kunikuza MTWARA... hatimaye Historia inaenda kuandikwa pale nangwanda sijaona Mtwara, narudi nyumbani tafadhari naomba ,mnipokee," alisema Ibraah.
Ibraah kwa sasa ni mmoja wa wasanii Chipukizi wanaofanya vizuri kwenye kiwanda cha muziki Afrika Mashariki akiwa na Extended Playlist (EP) yenye nyimbo takribani 6, alizoshirikiana na wasanii mbalimbali Afrika, ikiwa ni pamoja na nyimbo kadhaa zinazoendelea kufanya vizuri kwenye chati mbalimbali za muziki Afrika.