Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Huyu ndiye ‘mtukutu’ Kizz Daniel aliyeleta balaa Dar

Kizz Daniel M Kizz Daniel

Sun, 14 Aug 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Wiki hii msanii kutoka Nigeria, Kizz Daniel ameteka mitandao ya kijamii nchini na nchini mwao, baada ya kushindwa kutumbuiza hapa nchini kwenye tamasha la Summer Applified katika ukumbi wa Werw House zamani Nextdoor Arena na kusababisha fujo za mashabiki.

Baadaye alikatwa na kufikisha kituo cha polisi na kukubali kurudia shoo hiyo Agosti 12. Mkali huyo wa wimbo ‘Buga’ alikuatana na wanahabari na kuomba radhi kwa tukio hilo.

Hii si mara ya kwanza kwa msanii huyo kuingia katika migororo ya aina hiyo, maisha yake ya kimuziki kwa kiasi fulani yamegubikwa na migororo na aliwahi kufikishwa mahakamani na lebo ya G-Worldwide Entertainment aliyosaini nayo mkataba mwaka 2013 wakati huo akijulikana kama Kiss Daniel.

Baadaye ulikuja kuzuka mgogoro wa kimasilahi kati yao hadi kuburuzana mahakamani kwa madai kuwa licha ya kutoa nyimbo zinazofanya vizuri kimauzo, G-Worldwide walikuwa wakimpatia Naira30,000 tu, wastani wa Sh160,000 kama mshahara kila mwezi.

Novemba 2017 Kizz Daniel alitangaza kuachana na G-Worldwide Entertainment na kuanzisha lebo yake Fly Boy Inc.

Hata hivyo, G-Worldwide walimfungulia kesi mahakamani kwa kukatisha mkataba wao, Kizz alishinda ingawa alipoteza hakimili ya jina lake, Kiss Daniel maana G-Worldwide ndio walikuwa na hakimiliki ya jina hilo.

Mei 2018, alitangaza kubadili jina lake la kisanii kutoka Kiss Daniel hadi Kizz Daniel, vivyo hivyo katika mitandao ya kijamii na katika majukwaa ya kidigitali aliyoweka nyimbo zake ikiwamo Spotify na Apple Music.

Mbali na saga lake na G-Worldwide, msanii huyo Juni 2022 akiwa nchini Zambia alizua hasira kwa mashabiki baada ya kuyakataa maua aliyopewa na shabiki uwanja wa ndege, hivyo watu wengi nchini humo kutaka shoo hiyo isifanyike.

Julai 2022 mashabiki kutoka nchini Marekani walitaka warejeshewe fedha zao, baada ya Kizz Daniel kuchelewe kwenye shoo kwa zaidi ya saa nne. Hata alipopanda jukwaani alitumbuiza kwa dakika 30 kisha kuondoka jambo liloibua hasira kwa mashabiki waliomngojea kwa muda mrefu.

Alianzaje muziki?

Kizz Daniel ni mwimbaji na mtunzi wa nyimbo alizaliwa Mei 1, 1994 katika Jimbo la Ogun, mtaa wa Abeokuta Kaskazini na kupewa jina la Oluwatobiloba Daniel Anidugbe. Ana shahada ya ‘Water Resources Management and Agrometeorology (Water Engineering) aliyoipata katika Chuo Kikuu cha Kilimo Abeokuta mwaka 2013.

Akiwa katika mahojiano na Factory78 TV, Kizz Daniel alisema alianza kuimba akiwa na umri wa miaka saba na baba yake alikuwa akimuunga mkono kwa kiasi kikubwa na hata fedha ya kurekodi wimbo wake wa kwanza alimpa Naira100,000 wastani wa Sh560,000.

Mei 2015, alitoa wimbo wake wa tatu uitwao ‘Laye’ katika siku yake ya kuzaliwa, wiki chache baadaye aliachia video ya wimbo huo na Aje films, Mei 14, 2016 akaachia albamu yake ya kwanza, ‘New Era’.

Chini ya lebo yake, Fly Boy Inc, mwaka 2018 ulikuwa mzuri zaidi kwake alipomshirikisha Wizkid katika wimbo ‘For You’, kisha akampa shavu Davido kwenye ngoma ‘One Ticket’ iliyofanya vizuri.

Desemba 30, 2018 alitoa albamu yake ya pili ‘No Bad Songz’ ikiwa na nyimbo 20 ikiwemo ‘One Ticket’, aliowashirikisha wasanii kama Diamond Platnumz, Nasty C, Philkeyz, Demmie Vee, Dj Xclusive, Wretch 32, Diplo na Sarkodie.

‘No Bad Songz’, inatajwa kama albamu yake iliyofanya vizuri zaidi sokoni kwa kuongoza kwenye chati za iTunes nchini Marekani. Juni 25, 2020 aliachia albamu yake ya tatu ‘King of Love’ kisha ‘Barnabas’ (2021).

Mei 4, 2022 aliachia wimbo maarufu kwa sasa ‘Buga’ walioshirikiana na Tekno na video yake kutoka Juni 22, 2022 na kupata mapokezi makubwa kiasi cha kufikisha watazamaji milioni 40 YouTube ndani ya mwezi mmoja na kukaribia rekodi ya video ya wimbo ‘Jerusalema’ wake Master KG kutoka Afrika Kusini ambayo ilifikisha watazamaji milioni 50 ndani ya mwezi mmoja na ndio video pekee ya muziki kutoka Kusini mwa Jangwa la Sahara iliyotazamwa zaidi YouTube hadi sasa.

Awakera mashabiki nchini mwake

Katika ukurasa wa instagram, mashabiki wengi nchini Nigeria wamemshauri Meneja wa Kizz Daniel, Paulo Okoye kuachana na msanii huyo kutokana na matukio yake ya utovu wa nidhamu kwa mashabiki wake kila mara, hasa tukio la juzi nchini Tanzania.

Haya ni baadhi ya maoni hayo;

007_News: Kizz Daniel anajenga picha mbaya katika soko, muache kwenye soko lake la ndani la Nigeria. Hayupo tayari kwenda kimataifa.

Propertyword: Kuwa na kipaji pekee haitoshi bali kuwa na akili na kuelewa biashara, muache peke yake ajitafute, natumaini hajachelewa sana.

Wadau watoa neno

Aliyekuwa Mkugenzi wa bendi ya Twanga Pepeta, Asha Baraka anasema ili kuondokana na matukio kama hayo mapromota wahakikishe mikataba yao inapita kwanza Baraza la Sanaa Taifa (Basata), wasilete wasanii kiholela, waishirikishe Serikali.

“Tulikuwa tunaandaa matamasha ya muziki wa dansi, wasanii wakubwa wanakuja, ila lazima tupitie serikalini, na ule mkataba unapelekwa moja kwa moja Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa ajili ya kodi, lakini kuna baadhi ya maporota wanakuwa wanadharau hilo,” anasema Asha.

Anasema mikataba ikiwa ya kirafiki msanii anaamua anavyotaka, ila suala la msanii mkubwa kama Kizz Daniel kupelekwa hadi polisi halileti picha nzuri.

“Anapoonekana msanii mkubwa anapelekwa Polisi haileti picha nzuri, kwa watu wa nje wanaweza kuona labda yule msaii kanyanyaswa. Wasanii wetu wanaweza kwenda nchi hizo hizo na wao wakafanyiwa vitu kama hivyo, hawataelewa huyu msanii wao kakosea,” anasema.

“Mfano tuchukulie hawa wasanii wakubwa wa kwetu kama Diamond, Harmonize au Alikiba, wamefanyiwa kitu kama hicho, kwa sisi Watanzania tutaona kama kuna unyanyasaji, hivyo waandaaji waweke mikataba iliyonyooka,” anasema Asha, aliyeongoza Twanga Pepeta kwa zaidi ya miaka 20.

Kwa upande wake mkongwe wa Bongofleva, Bwana Misosi anasema mwaka 2015 aliwahi kukimbiwa na promota baada ya kufanya shoo, lakini hakuwa na mkataba na ndicho hasa kilimponza.

“Kwangu ilitokea promota kanikimbia baada ya kutumbuiza, mwanzo alionyesha ubinadamu atanilipa. Unaona mashabiki wameshajaa, unatumbuiza kwa ule ubinadamu matokeo yake promotoa anakula kola, ndio hadi ile Profesa Jay aliimba promota anabipu,” anasema na kuongeza:

“Hiyo ya Kizz Daniel kama ni kweli jinsi nyie waandishi mmeandika alisahau sijui nguo, mimi naona ni utovu tu wa nidhamu ya kazi na kukosa weledi wa kazi, sio sababu yenye mashiko!” anasema Bwana Misosi.

Hili la promota kukimbia au kutolipa kama makubaliano yalivyo, liliwahi kumkuta msanii wa Bongofleva, Harmonize.

May, mwaka huu Harmonize alikamatwa huko Nairobi, Kenya na kushikiliwa katika kituo cha Polisi cha Kileleshwa kwa kudaiwa kukiuka makubaliano ya kutokea kwenye club kadhaa za jijini humo, ikiwemo Captains Lounge, kabla ya kuachiwa baadaye.

Akilizungumzi hilo, Harmonize alisema “Kilichonisikitisha ni promota kuchukua pesa za watu wasiopungua 400,000 kisha wakashindwa kuja kumalizia malipo yaliyobaki na kukimbia, hii inaumiza sana. “Ni dalili ya kunivunjia heshima na uaminifu kwa mashabiki zangu, imeniumiza kuona watu waliojitoa kulipa viingilio vyao just for me wanadhulumiwa mwishoni kabisa,” alisema Harmonize.

Alisema mkataba uliofuata sheria na taratibu ndiyo utakaomlinda msanii, tofauti na hapo promota akikimbia vyombo vya usalama vinaweza kumchukulia hatua.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz