Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hivi ndivyo Diamond anavyoendelea kuibeba Afrika Mashariki

Platnumz Diamond Dd.jpeg Diamond Platnumz

Sun, 21 Aug 2022 Chanzo: Mwananchi

Msanii kutokea visiwa vya Puerto Rico, Luis Fonsi kupitia video ya wimbo wake, Despacito iliyotoka Januari 13, 2017 anashikilia rekodi ya video ya muziki iliyotazamwa zaidi YouTube duniani ikiwa na watazamaji zaidi ya bilioni 7.9.

Je, barani Afrika mambo yapo vipi, hasa ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara? Hizi ni video 15 za wasanii kutoka eneo hilo ambazo zimetazamwa zaidi YouTube kwa muda wote, huku Diamond Platnumz akiwa ndiye msanii pekee wa Afrika Mashariki aliyechomoza.

1. Master KG ft. Nomcebo - Jerusalema (milioni 514+)

Wimbo huu ulitoka Novemba 29, 2019 na kupata mapokezi makubwa Afrika Kusini, video yake ilitoka Desemba 12, 2019 na sasa ndio video iliyotazamwa zaidi kwenye mtandao wa YouTube Afrika, ikiwa na watazamaji zaidi ya milioni 514, alikuja kuuweka kwenye albamu yake ya pili inayokwenda kwa jina hilo iliyotoka Januari 2020.

Wimbo huu una remix mbili, ya kwanza ilitoka Juni 2020 akimshirikisha Burna Boy wa Nigeria, ilifanya vizuri na kuingia chati za Billboard nchini Marekani. Remix ya pili ilitoka Septemba 2020 ambapo aliwashirikisha Venezuela Micro TDH na Greeicy kutokea Colombia.

Master KG ambaye ni mwanzishili wa dansi maarufu ‘Bolobedu’, kupitia albamu yake, Skeleton Move alishinda tuzo ya African Muzik Magazine Awards (AFRIMMA) katika kipengele cha Best Artist/Group in the African Electro.

2. Magic System ft. Chawki – Magic in the Air (milioni 383+)

Kundi la Magic System lilianzishwa mwaka 1996 huko Abidjan nchini Ivory Coast, wasanii wake ni Salif “Asalfo” Traoré, Narcisse “Goude” Sadoua, Étienne “Tino” Boué Bi na Adama “Manadja” Fanny.

Mwaka 2014 waliachia wimbo wao ‘Magic in the Air’ wakimshirikisha Chawki kutoka Morocco, ni miongoni mwa nyimbo zilizotoka kwa ajili ya kusherehesha fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika nchini Brazil mwaka 2014.

Video yake ilitoka Machi 17, 2014 na hadi sasa ina watazamaji zaidi ya milioni 383 YouTube na kuzidi kuliweka kundi hilo katika ramani baada ya kufanya vizuri Afrika Magharibi na mtindo wa dansi ‘Zouglou’ hadi kutambulika kama miongoni mwa wasanii wakubwa Ufaransa kutoka Afrika.

3. Ckay - Love Nwantiti (milioni 296+)

Agosti 30, 2019 msanii kutokea Nigeria, Ckay aliachia Extended Playlist (EP) iitwayo Ckay yenye nyimbo nane chini ya Chocolate City na Warner Music Group, ndani yake ndipo kuna ngoma, Love Nwantiti iliyoachiwa Agosti 29, 2019.

Video ya ngoma, Love Nwantiti ilitoka Februari 14, 2020 na tayari ina watazamaji zaidi milioni 296, ikiwa ndiyo inaongoza Nigeria, huku ikishika nafasi ya tatu Afrika.

Wimbo huu umechangia sehemu kubwa ya mafanikio ya EP hiyo ambayo aliweza kuingia kwenye chati za Billboard chini Marekani, Canada na Uholanzi, pia iliingia kwenye chati za Ufaransa (SNEP).

4. Burna Boy – On The Low (milioni 284+)

Ngoma yake, ‘On The Low’ ambayo ni mchanganyiko wa Afrobeat na Dancehall imempatia mafanikio makubwa mwimbaji huyo kutoka Nigeria, ambaye alivuma zaidi mwaka 2012 baada ya kuachia ngoma ‘Like to Party’ kutoka kwenye albamu yake, ‘L.I.F.E’ iliyokuja kutoka mwaka 2013.

Video ya wimbo huo uliyotayarishwa na Kel P ilitoka Novemba 16, 2018 ikiongozwa na Meji Alabi, tayari imefikisha watazamaji zaidi ya milioni 284.

Ikumbukwe Burna Boy ambaye mwaka 2017 alisaini na Bad Habit/Atlantic Records ya Marekani na Warner Music Group, ameshinda tuzo tatu za BET na moja ya Grammy kupitia albamu yake ya tano ‘Double As Tall’.

5. Die Antwoord – Baby On Fire (milioni 263+)

Ni kundi la muziki wa Hip Hop kutoka Afrika Kusini lililoanzishwa mjini Cape Town mwaka 2008 na marapa wawili, Ninja na Yolandi Visse, mwaka 2009 walitoa albamu yao ya kwanza, ‘$O$’ ya bila malipo mtandaoni na kuwatangaza vilivyo.

Kufika Juni 2, 2012 waliachia video ya wimbo wao ‘Baby On Fire’ ikiongozwa na Ninja na Terence Neale, hadi sasa huko YouTube imefikisha watazamaji zaidi ya milioni 263.

Mwaka 2011 Die Antwoord walianzisha lebo yao wenyewe, Zef Recordz na kufuatia mfululizo wa albamu zao kali kama ‘Ten$Ion’ (2012), Donker Mag (“Dark Power”; 2014) na ‘Mount Ninji and da Nice Time Kid’ (2016).

6. Davido - Fall (milioni 246+)

Mwimbaji huyo wa Nigeria alianza muziki katika kundi la KB International, Davido alipata umaarufu mwaka 2011 alipoachia ngoma yake ‘Dami Duro’ ukiwa wa pili kutoka kwa albamu yake ya kwanza, ‘Omo Baba Olowo’.

Mwaka 2017 baada ya kurekebisha mkataba wake na Sony Music, Davido alitoa nyimbo tano, ikiwepo ‘Fall’ ambao ulifanya vizuri hadi chati za Billboard, video yake iliyotoka Juni 2, 2017 imefikisha watazamaji milioni 246.

Kupitia Twitter mwaka 2016 Davido alitangaza kusaini mkataba na Sony Music, miezi michache baadaye alianzisha lebo yake, Davido Music Worldwide (DMW) na kuwasaini Dremo na Mayorkun.

7. Sinachi – Way Maker (milioni 207+)

Ni mwimbaji wa muziki wa injili kutokea Nigeria na kiongozi wa kanisa la Loveworld, ametoa nyimbo maarufu kama ‘I Know Who I Am’, ‘Great Are You Lord’, ‘Way Maker’, ‘Jesus is Alive’ na ‘Rejoice’.

Video ya wimbo wake, ‘Way Maker’ iliyotoka Desemba 30, 2015 imefikisha watazamaji zaidi ya milioni 207 YouTube, ndio video namba moja ya msanii wa kike yenye mafanikio zaidi Afrika.

Ikumbukwe Sinachi anashikilia rekodi ya kuwa msanii wa kwanza kuongoza kwenye chati za Billboard Christian Songwriter kwa wiki 12 mfululizo. Septemba 2019 alikuwa msanii wa kwanza wa injili kutoka Afrika kuzuru India na kuongoza matamasha makubwa.

8. Burna Boy - Ye (milioni 199+)

Ngoma hii ilishika nafasi ya 26 na 31 kwenye chati za Billboard za R&B/Hip-Hop na R&B/Hip-Hop Airplay, pia ilishinda tuzo za Soundcity MVP Awards Festival 2019 kama Wimbo Bora wa Mwaka Chaguo la Wasikilizaji.

Unapatikana kwenye albamu yake ya tatu inayokwenda kwa jina ‘Outside’, video ya wimbo huo uliyotayarishwa Phantom ilitoka Agosti 6, 2018 na sasa ina watazamaji zaidi ya milioni 199 YouTube.

9. Innoss’B ft. Diamond Platnumz – Yope Remix (milioni 192+)

Hadi sasa staa wa Bongofleva toka WCB Wasafi, Diamond Platnumz ameshiriki katika video nne zilizofikisha watazamaji zaidi ya milioni 100 YouTube, video hizo ni ‘Yope Remix’, ‘Inama’, ‘Waah!’ na ‘Time To Party’.

Video ya Yope Remix ambayo Diamond kashirikiana na Innoss’B kutokea DR Kongo ilitoka Septemba 7, 2019 na hadi sasa ina watazamaji zaidi ya milioni 192 YouTube na ndiyo video iliyoongoza Afrika Mashariki.

Diamond ametoa albamu tatu, EP moja, huku akishinda tuzo zadi 40, ndiye msanii pekee Tanzania na Afrika Mashariki ambaye video zake zote zimefikisha watazamaji zaidi ya bilioni 1.6.

10. Die Antwoord – Ugly Boy (milioni 189+)

Inashikilia redodi ya kuwa video ya tatu ya muziki iliyotazamwa zaidi nchini Afrika Kusini, ilitoka Novemba 2, 2014 na hadi sasa imepata watazamaji zaidi ya milioni 189 YouTube.

Vile vile, video ya wimbo wao, ‘I Fink u Freeky’ iliyotoka Januari 31, 2012 imefikisha watazamaji zaidi milioni 177, ndio kundi lenye mafanikio makubwa zaidi katika mtandao wa YouTube barani Afrika.

11. Tekno - Pana (Milioni 183+)

Mwimbaji huyo wa Nigeria alianza muziki chini ya K-Money Entertainment, mwaka 2013 akasaini tena Made Men Music Group na kutoa nyimbo kama ‘Dance’ na ‘Anything’ zilizofanya vizuri hadi kuwania tuzo za Nigeria Entertainment 2014.

Mwaka 2015 Tekno alitoa wimbo wake maarufu, ‘Duro’, kisha ukafuata ‘Pana’ ambayo video yake ilitoka Agosti 22, 2016 na hadi sasa imetazamwa zaidi ya mara milioni 183 YouTube.

Kufika Julai 2019, Tekno alishirikishwa kwenye wimbo uitwao ‘Don’t Jealous Me’ kutoka katika albamu ya Beyonce, The Lion King: The Gift, pamoja na Yemi Alade na Mr. Eazi.

12. Davido - If (milioni 152+)

Ikumbukwe awali hii ndio ilikuwa video ya Davido iliyotazamwa zaidi YouTube, lakini ikaja kuzidiwa na ‘Fall’ iliyotoka miezi minne baadaye ndani ya mwaka 2017, video ya wimbo ‘If’ ilitoka Februari 17, 2017 na imefikisha watazamaji milioni 152.

13. Yemi Alade - Johnny (milioni 147+)

Ni mwimbaji wa Nigeria, alianza muziki mwaka 2009, alingoja hadi 2013 alipofanikiwa kutoa wimbo wake maarufu Afrika ‘Johnny’ kisha ikafuata albamu yake ya kwanza ‘King of Queens’ iliyotoka Oktoba 2014 chini ya Effyzzie Music Group.

Video ya wimbo wake, Johnny uliotoka Machi 3,2014 na tayari imejikusanyia watazamaji milioni 147 YouTube, ndio video ya muziki wa kidunia ya msanii wa kike yenye mafanikio zaidi Afrika.

Ikumbukwe hadi mwanzoni mwa 2019 Yemi Alade alikuwa ndiye mwimbaji wa kwanza wa kike Afrika kufikisha watazamaji milioni 100 YouTube, pia akiwa ni msanii wa pili Nigeria baada ya Davido.

14. Runtown - Mad Over You (milioni 147+)

Msanii na muziki kutoka nchini Kenya na mzazi mwenziye na Diamond Platnumz, Tanasha Donna alitakiwa kutokea kwenye video hii, lakini wakashindwana upande wa malipo na menejimenti ya Runtown kutokea Nigeria.

Licha ya kutoa ngoma kali kama ‘Gallardo’ akimshirikisha Davido, ‘Mad Over You’ aliyorekodi peke yake ndiyo iliyomtoa kimasomazo, video yake ilitoka Desemba 7, 2016 na ndani ya miaka mitano imepata watazamaji zaidi ya milioni 147 YouTube.

Novemba 23, 2015 Runtown aliachia albamu yake ‘Ghetto University’ chini ya MTN Music Plus ambayo iliuza zaidi ya Naira35 milioni mtandaoni.

15. Wizkid ft. Drake - Come Closer (milioni 122+)

Ni mwimbaji kutoka Nigeria, ameshinda tuzo zote kubwa Afrika, pia ameshinda BET na Grammy kupitia wimbo ‘Brown Skin Girl’ aliyopewa shavu na Beyonce katika albamu yake, The Lion King: The Gift.

Hapo Aprili 7, 2017 aliachia video ya wimbo wake ‘Come Closer’ akimshirikisha Drake kutoka Marekani, video hiyo imefikisha watazamaji zaidi ya milioni 122 YouTube.

Ikumbukwe Come Closer ni wimbo wa pili kwa wawili hao kufanya pamoja, wa kwanza ukiwa ‘One Dance’ uliotoka mwaka 2016 ambapo Drake alimshirikisha Wizkid, huu ndio ulimwezesha kinda huyu wa Afrika Magharibi kuingia kwenye chati za Billboard Hot 100 kwa mara ya kwanza. Mwaka 2021 aliingia tena kwenye chati hizo na wimbo wake, ‘Essence’ ambao umedumu kwa zaidi ya mwaka mmoja ndani ya Billboard.

Chanzo: Mwananchi