Les Wanyika ni kundi lililojitenga kutoka Simba Wa Nyika baada ya wanamuziki kadhaa wa kundi hilo kuona wanadharauliwa na mmoja wa viongozi waanzilishi wa kundi.
Kujitenga kwa wanamuziki hawa kuliidhoofisha sana Simba wa Nyika iliyobakiwa na ndugu watatu, Wilson Peter, George Peter na William Peter ambaye wakati huu hali yake haikuwa inaweza kutegemewa katika kazi kutokana na maradhi yake ya kichwa.
Wilson hakuamini kilichotokea kwamba bendi yake iliyokuwa maarufu ikawa haiwezi tena kupiga kwa kukosa wanamuziki na hata walipojaribu kupiga walikosa wapenzi. Baada ya miezi kadhaa ya kushindwa kufanya maonyesho kwa kukosa wanamuziki na hata mashabiki, bahati kubwa ikatokea kwa Simba wa Nyika, wanamuziki watatu kutoka Kurugenzi Jazz Band ya Arusha, George Madrago mpiga besi, Joseph Tito mpiga rhythm na Mzee Maneno Shaaban aliyekuwa anapiga drums na tumba wakaungana na Wilson na George kuifufua Simba wa Nyika. Walifanikiwa kupiga muziki mzuri lakini bahati haikuwa yao wakakosa wapenzi. Haukuchukua muda mrefu, Wilson na George walianza kutofautiana tena, safari hii kukatokea mpasuko ulioanzisha Orchestra Jobiso.
Orchestra Jobiso ilianza vizuri ikiwa na wanamuziki, George Peter, George Madrago, Joseph Tito, Said Makelele na Mambi Juma.
Katika rekodi ya kwanza ya Jobiso pia walikuwa na mpiga saxaphone, George Kalombo na wakatoa vibao kama Christmas Imefika, Mwana wa Kambo, Pole Jobiso, Karibu, Chunga Heshima na Visa Vyako.
Wakati huo mdudu wa matatizo tayari aliingia Les Wanyika, pamoja na kwamba Profesa Omary ndiye aliyekuwa kiongozi, taratibu akaanza tabia ya ulevi na hivyo kutokuwa na mahudhurio mazuri kazini, usukani ukawa unashikwa na John Ngereza.
Pia Soma
- Umefikiria kufuga bata? anza leo
- ONGEA KILIMO : Inawezekana kujiajiri kwa kufuga nyuki
- Kilimo cha mbogamboga kilivyowatoa wasomi wa chuo kikuu
Kutokana na tabia hiyo mwanamuziki Stanley Mtambo na Abbu Omar wakakaribishwa ili kupiga rhythm. Abbu baadaye alikuja pia kurithi jina la Profesa Jnr.
Hali hii ya kuwa na matatizo na uongozi usioeleweka ikaanza kuleta matatizo kwa wanamuziki hasa katika malipo, ndipo wanamuziki Issa Juma na Mohamed Tika wakaamua na kuiacha bendi hiyo.
Issa Juma ndiye aliyekuwa muimbaji mkuu Les Wanyika sauti yake inatambulika dunia nzima kutokana na wimbo Sina Makosa. Watayarishaji wa kampuni mbalimbali za kurekodi mjini Nairobi waliposikia hilo wakaanza kumfuata ili arekodi katika studio zao. Kampuni iliyofanikiwa kumpata ilikuwa Meghs.
Katika kampuni hiyo alirekodi nyimbo kadhaa zilizopata umaarufu. Kimsingi inaonekana mwanzoni Issa hakuwa na wazo la kuanzisha bendi, mpaka alipolazimika kutafuta jina la bendi ya kuzibeba nyimbo alizorekodi, ndipo kwa mara ya kwanza jina la Super Wanyika lilipozaliwa.
Nyimbo zilizotolewa kwa jina la bendi hii zilikuwa kama Anita, Unataka Nikupendeje na Jennifer. Wanamuziki walioshiriki kazi hizi za mwanzo walikuwa ni Mohamed Tika, Shoushou Bainga na Michael Beche ambao ni waimbaji, Shoushou alikuwa Mkongo, aliwahi kupitia bendi ya Safari Trippers.
Mzee Maneno Shaaban alipiga drums, Issa Khalfani Bendera, kwenye solo, Stanley Mtambo gitaa la rhythm, George Madrago gitaa la besi, Said Makelele na Mambi Iddi wakiwa kwenye trumpet. Nyimbo zilipotoka zilianza kuvuma na kulazimisha bendi ianze kufanya maonyesho.
Wanamuziki wakakubaliana na Babuu ambaye pamoja na kuwa na studio pia alikuwa na vyombo vya muziki, hivyo akawakodisha vyombo kwa mkataba maalumu.
Super Wanyika ilidumu kwa zaidi ya miaka mitatu. Baadhi ya wanamuziki waliokuwemo katika kundi hilo ni Mzee Mohamed Tungwa akipiga solo, Abdalah Kimeza kwenye Saxaphone, Jumanne Kilongola kwenye trumpet, Joseph Tito akipiga gitaa la rhythm, Shwaib Ole Monduli muimbaji na wengineo.
Hatimaye bendi hiyo ilikufa kwa makosa yaleyale ya uongozi mbovu. Issa Juma akaanza kusahau kuwapa wanamuziki haki stahili. Sauti yake iliendelea kuwa muhimu katika anga la muziki, hivyo akaanza kuingia mikataba tofauti na aliokuwa nao Meghs.
Akaingia mkataba na kampuni ya AIT, halafu akaingia mkataba na mtayarishaji mashuhuri Nairobi wakati huo Joe Mwangi wa Matunda Production.
Sasa kazi ambazo zilifanywa katika mikataba hiyo mipya alitambulisha kuwa zimerekodiwa na bendi aliyoitambulisha kama Wanyika Stars, baadhi ya nyimbo ambazo zilirekodiwa kwa jina hilo ni kama Sigalame, Mpita Njia, Bomanga, Mony na kadhalika.
Kutokana na wanamuziki hawa walioshiriki kazi hizi, baadhi wakaunda kundi la Sigalame System ambalo halikudumu sana, wengine wakaunda kundi la Orchestra Vinavina.