Historia ya Dorah; Msanii wa filamu Bongo, Wanswekula Zacharia ‘Dorah’ ametimiza umri wa miaka 28 mwaka huu, Dorah alizaliwa huko Singida nchini Tanzania, yeye ni mtoto wa pili kati ya watoto sita.
Dorah anasema kwamba wakati anakua maisha hayakuwa mepesi kwa kuwa wazazi wake hawakuwa na uwezo, ni historia ndefu. Wakati huo tayari alikuwa ameanza kuugua hali ambayo hawakujua kwamba ilikuwa ni ugonjwa wa Seli Mundu (Sickle Cell).
Ni ugonjwa ambao huathiri mfumo wa kinga na inakuwa rahisi mtu kuandamwa na magonjwa mbalimbali katika mwili kutokana na kukosa kinga dhabiti ya kujilinda. Kwa mujibu wa Dorah, historia yake inavitu vingi na pia inahusu watu wengi ambao wamemlea na kumsaidia kufika alipo.
”Nilichukuliwa nikiwa binti wa miaka 8 na mtawa mmoja aliyekuja nyumbani kwetu kututembelea, baada ya kuona hali sio hali, wakaamua kunipeleka katika makazi ya watoto ambako nilianza masomo yangu na pia kuendelea kupewa huduma za matibabu kutokana na hali yangu”, anasema Dorah.
Aliendelea na masomo yake, huku akipewa matibabu, kulingana na msanii huyu alikuwa ameshauriwa na wataalam wa matibabu yake kwamba hali ya ugonjwa huo wa Seli mundu ingekwisha atakapokuwa mtu mzima.
Japo alipata wasamaria wema ambao walitembea naye katika kuhakikisha kwamba amepata matibabu na hali kadhalika amepata masomo anasema kwamba barabara ya kuishi maisha kwa muonekano alionao haikuwa rahisi, hasa kwa kuwa wengi ni wale ambao walimnyanyapaa licha ya miaka kusonga Dorah aliendelea kuwa na muonekano wa ‘kitoto’ na hilo lilimkosesha usingizi kwa miaka mingi.
Mwanamke huyu anasimulia siku zilizojawa na kiza kikuu ambapo baadhi ya watu katika jamii yake na hata watu waliokuwa karibu naye walimpa machungu mengi kwa kutumia muonekano wake kumdhalilisha.
”Hakuna mtu angependa kuwa tofauti na mwingine, sote tunatamani tuwe sawa kwa hivyo inauma kila wakati baadhi ya watu wakinilinganisha na mtoto , inauma sana kwa sababu nina akili za utu uzima na nina haki kama mwanamke mwengine yule ”Dorah alisema akiongea na BBC Swahili.
Ila siku zilivyozidi kwenda akajiunga na chuo kimoja kusomea uanahabari aliamua kupiga moyo konde na kukubali hatma yake kwamba huenda atakua kama wenzake.