Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hii sanaa bila King ni Majuto...

11348 Majuto+pic TanzaniaWeb

Sat, 11 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam. mazingira yake yananikumbusha maeneo mengi ya mbali na uwanda wa bahari. Uoto wa asili, hali ya hewa pamoja na wadudu wanaoruka na kutambaa ambao kwa miaka mingi wametoweka kwenye uso wa Dar es Salaam.

Sauti za ndege zimebeba nafasi ya kelele za bodaboda. Ni eneo tulivu kwa maana ya utulivu huku kukiwa na daladala chache sana zinazokwenda na kurudi. Asubuhi, mchana na nyakati za jioni ndipo uhai wa eneo hilo huonekana.

Naongelea ilipo Hospitali ya Mloganzila yenye kila kitu kinachotakiwa kuwepo ikiwa ni pamoja na uwepo wa dada yangu kipenzi akipatiwa matibabu. Dakika chache baada ya kumjulia hali na mimi kurudi nyumbani,

nikiwa na mizuka ya sikukuu ya Nanenane mara simu ya dada ikaingia. Sauti ilibadilika maumivu yakiakisi kupitia mawimbi ya sauti yake. Sikuwa na hofu na hali yake ya kiafya, “nimetoka na chaja yake?” Nilijiuliza kabla ya kupokea simu.

Hizi habari za King Majuto kufariki ni za kweli? Lilikuwa swali lake baada tu ya kupokea simu. Wameshamuua sana ikiwa kweli tutajua. Nilimjibu hivyo kwa kifupi, ingawa jibu halikuwa na ujazo wa kutuliza hofu yake.

Dada alikuwa kama kafungulia simu za maswali. Nikaanza kupokea simu na meseji nyingi sana juu ya King aliyetuachia Majuto. Nilipowasha ‘data’ ndipo nilipobaini kuwa nilikuwa nimechelewa kujua. Magrupu kama yote ni Majuto tu.

King ameondoka nyuma katuachia majuto. Amri Athuman, kiumbe mmoja mwenye kila kitu cha kumliwaza mgonjwa, mfiwa, mfungwa au mnyonge katika uso wa dunia hii ameondoka na hatutamuona tena zaidi ya kumbukizi za kazi zake bora kabisa.

Kwa mara ya kwanza King katuachia majuto katika uso wa dunia, baada ya miaka mingi ya furaha, kicheko na tabasamu tumuonapo. Kuanzia runingani, majukwaani mpaka mitaa ya Chumbageni.

Hakutulazimisha kucheka, ila tulilazimika kucheka kila tumuonapo. Gwiji la sanaa kuwahi kutokea Tanzania hii. Aliifanya sanaa ya kuchekesha watu ionekane kitu rahisi mno kupitia yeye.

Kuna mambo ambayo aliyafanya watu wakaumia mbavu kwa kicheko ambayo mtu mwingine akiyafanya inakuwa kero kwa watu. Majuto alikuwa mtu katili wa mbavu za watu kwa kazi yake hii iliyompatia pesa uzeeni.

Jambo unalofanya ukizidisha sana ni sehemu ya ukatili. Majuto alipitiliza kwenye kiwango cha kuchekesha na sasa akawa binadamu katili zaidi wa mbavu za watu. Kumuona tu kwenye shughuli zake za kawaida alikuwa kichekesho.

Tatizo siyo kuchekesha, tatizo yeye mwenyewe akichekeshwa kitendo cha kucheka kilikuwa kichekesho kuliko vichekesho vya wachekeshaji wengi sana. Hakujitengeneza, ila aliumbwa hivyo.

Sanaa ya kuchekesha ilijenga undugu na mwili wake na yeye akafunga ndoa na sanaa yenyewe. Watu tunaishi mara moja duniani, kibaya zaidi kuna watu wakiondoka hawazaliwi tena kupitia mwili wa binadamu mwingine.

Wachekeshaji Tanzania hii wapo wengi sana na walio wengi ni wale ambao waliona njia rahisi ya kupata pesa na umaarufu ni kuchekesha watu. Hawa wako wengi sana mpaka imekuwa kero na ndiyo chanzo cha kudumaa kwa sanaa.

Majuto alipoanza miaka hiyo hakufahamu kama sanaa hii inaweza kumpa fedha, nyumba, gari na utajiri mkubwa. Vyote hivyo vimemkuta Majuto akiwa tayari yuko juu kwenye sanaa, navyo vikaungana naye na kuikuza sanaa yake.

Walio wengi wamekuta sanaa ina pesa tayari wakaamua kuungana nayo ili nao wapate pesa. Wanaamua kutushikia ‘mtutu wa bunduki’ kutulazimisha tucheke kinguvu vitu visivyochekesha.

Aliyefanya tucheke mpaka mashavu yameremete kwa machozi ndiye huyohuyo kalazimisha hii leo mashavu yalowe machozi kwa vilio. Kifo hakitawahi kuwa rafiki na mioyo ya binadamu daima dumu.

Kipindi ambacho furaha inahitajika sana, Majuto aliyestahili kutupa furaha anaamua kutuachia huzuni. Miaka ya karibuni kuna mengi sana yanachangia furaha iwe kitu adimu sana kwenye mioyo ya watu.

Jamii ya leo imekuwa na mifarakano kuanzia ngazi ya familia, kaya mpaka Taifa. Watu aina ya King kipindi hiki siyo wa kutuachia majuto. Sanaa na vipawa vyao vilifaa kutuweka sehemu moja na kutuunganisha.

Katika wakati ambao watu wanahitaji furaha ili kujenga uzalendo anaosisitiza Mheshimiwa Rais Magufuli. Shamba la kuvunia hiyo furaha limetoweka, uzalendo bila furaha kwenye mioyo ya watu ni kazi bure.

Majuto alikuwa alama sahihi ya Mswahili, alikuwa ngao ya utamaduni wetu, alikuwa mhimili wa utu wetu na zaidi ni sehemu ya binadamu ambaye alitusahaulisha hata ‘watu wasiojulikana’ pindi tumuonapo.

Vituko vyake ukitazama kwenye basi ungesahau kama kuna ajali duniani. Kama ni kibarazani usingekumbuka matatizo ya mwenye nyumba. Kama ni chumbani mawazo ya kwamba kuna shetani wa usaliti wa ndoa ungeyapuuza.

King Majuto ni sehemu ya binadamu walioletwa duniani ili kuwasahaulisha watu shida zao. Mungu alitupa mtu rafiki wa maisha yetu ya shida na raha. Mungu huyohuyo katuondolea chanzo cha furaha katika maisha ya kila siku.

Kama ambavyo huwezi kuipata Tanzania nyingine, ndivyo ambavyo huwezi kumpata King Majuto mwingine. Kuna vitu vya pekee havijirudii kwenye uso wa dunia hii. Nyerere hatazaliwa tena ila Bokassa atazaliwa tena na tena na tena.

Firauni anaweza kuwa alizaliwa tena katika mwili wa Aldof Hitler, lakini Nabii Mussa mwingine hajawahi kuwepo hata wa mfano wake. Maana’ake ni kwamba mtu mwema au jambo jema hutokea mara moja.

Majuto alikuwa miongoni mwa watu wema. Siyo kwa kukosa dhambi katika maisha yake, hapana. Bali kwa kujaza upendo na furaha kwenye akili na mioyo ya binadamu hata wakawa pamoja kwenye kicheko.

Mtu mwema ni yule anayewaweka binadamu pamoja kwenye furaha. Majuto aliwafanya watu wengi kwa pamoja wawe na furaha. Dunia bila furaha haistahili kuwa dunia.

Wakati huu ambao ndugu jamaa na marafiki, pamoja na mashabiki wa kazi za Majuto wakiwa wenye huzuni, tuyaishi yale aliyofanya King Majuto. Kutengeneza furaha.

Kila mtu kwa nafasi yake atengeneze furaha, kadri unavyokaza shingo yako na kuwa ngumu kwa sababu tu ya chuki zisizo na mbele wala nyuma tambua kuwa unayakaribisha jirani mno mauti ya nafsi yako. Wenye furaha huishi muda mrefu.

Furaha nd’o kila kitu kwa maisha ya mwanadamu. Tunatafuta pesa ili kujenga furaha. Tunataka uongozi bora ili tuwe na furaha. Tunaoa au kuolewa na wapenzi sahihi ili kuishi kwa furaha. Kila kitu kinafanyika ili kuleta furaha.

Kazi ya kutengeneza furaha kwenye mioyo na nyuso za binadamu, King Majuto aliifanya kwa miaka mingi sana bila kutuangusha hata mara moja. Mpaka juzi mwili wake unaacha roho aliendelea kuwa sehemu ya kiwanda cha kuzalisha furaha.

Msanii mmoja nyota na mwenye jina kubwa aliwahi kuniambia kuwa Mzee Majuto amefanya naye kazi nyingi sana, lakini ndiye msanii pekee ambaye huwa anapata tabu sana kufanya naye kazi.

Tabu yenyewe ni kuvumilia kumaliza ‘sini’ moja baada ya nyingine. ‘Sini’ moja wangeweza kurudia hata mara kumi kwa sababu ya kushindwa kuzuia kicheko kwenye jambo ‘siriazi’.

Waliweza kuigiza wapo msibani waonekane wana majonzi, lakini Mzee Majuto angeweza kuigiza kweli mtu mwenye majonzi makubwa, lakini yule anayeigiza naye atagalagala kwa kicheko.

Kila kitu alichofanya Mzee Majuto kilikuwa kichekesho kwa wengine. Pengine mtu pekee ambaye alimzoea na kutojali ni mkewe na mama yake mzazi. Sisi wengine ingekuwa ngumu mno kumzoea. King Majuto alikuwa sanaa kamili.

Hakupaswa kufariki dunia wakati huu. Hata hivyo, tusingeweza kufanya jambo lolote. Katika kipindi hiki kigumu, tuendelee kumwombea, huku familia ikipata nafuu na utulivu wa kuondokewa na kipenzi chao. Hii sanaa bila King ni majuto.

Chanzo: mwananchi.co.tz