Kama unadhani umeshasikia visa vingi vya kusisimua, kuchekesha na kufikirisha, kuna kisa hiki cha mapacha wawili warembo Lucy na Anna.
Wanawake hawa ni mapacha wanaofanana sana kutoka nchini Australia. Mfanano walio nao mapacha hawa sio rahisi kuweza kuwatofautisha. Ukimuona Lucy utadhani umemuona Anna na ukimuona Anna utadhani umemuona Lucy.
Jambo la kushangaza ambalo ninataka ulifahamu siku ya leo ni kwamba mapacha hawa wanafanya kila jambo pamoja. Ndio umesoma sahihi kabisa kila jambo.
”Hakuna kama sisi, sisi tunajifikiria kama mtu mmoja”, walieleza kwa pamoja katika moja ya mahojiano yao. Wanasema ikiwa wanafanya usafi wa nyumba yao, mmoja atafanya kwa dakika tano na mwingine atafanya dakika nyingine tano. Lakini cha kuchekesha zaidi wakati mmoja anafagia mfano mwingine pia atakuwa anaonyesha ishara kwa mikono kama anafagia kwa kuigilizia upande ule ule anaofanya mwenzake.
Mapacha hao pia wanaeleza wanaamka pamoja na kuoga pamoja na hata msalani wanaenda muda mmoja. Lucy na Anna waliwahi kupata kazi moja na mmoja alikuwa analipwa na mwingine alikuwepo kama anajitolea, wanasema kwao hilo halikuwa tatizo sababu walikuwa pamoja.
VIPI KUHUSU MAHUSIANO, JE WANA WAPENZI TOFAUTI?
”Tunashirikiana kila kitu, gari,simu,kitanda na hata ukurasa mmoja wa mtandao wa kijamii wa Facebook”. Kubwa zaidi walilobainisha mapacha hao waliweka wazi hata mpenzi wao ni mmoja (waliongea huku wakicheka) kila mmoja alionekana kufurahia jambo hilo ambalo linashangaza kwa watu wengi. Unaweza ukajiuliza namna ulivyo na wivu na mume wako au mke wako lakini mapacha hawa wanabainisha hawana wivu kabisa na wanapendana sana.
WALIKUTANA WAPI NA MPENZI WAO?
Lucy na Anna walikutana na mpenzi wao Ben katika mtandao wa Facebook. Mahusiano yao na Ben yana miaka kumi na moja sasa. Wanasema, watu wengi walidhani mahusiano yao hayatadumu. Warembo hao wakiwa wamevalia nguo zao za kufanana wanasema tuliweza kuthibitisha kwamba watu wengi walikosea kufikiri hivyo.
Lucy na Anna wakamtupia swali mpenzi wao Ben ”Ulijisikiaje tulipokwambia tunataka uwe wa kwetu sote?”, Ben anasema “Nilidhani mnanifanyia mzaha tu, niliwaza mnanitania tu”.
Ben akiwa amekaa katikati ya warembo wake anaeleza zaidi kwamba walimwambia wanajisikia kama wao ni mtu mmoja. Pia wakamueleza watu wanawachukulia mapacha hao kama mtu mmoja,hivyo na yeye Ben akaamua kuwachukulia kama mtu mmoja. Ben anasema ”Kama watu wengine wana tatizo juu ya hilo, ni tatizo lao,” akionyesha hajali kuhusu hilo.
Nawaza kaka zangu wa Bongo mngeona mmeokota dodo yani zali la mentali au msingeweza?
Mapacha hao wanaamini wao watatu ilipangwa wawe pamoja na wanasema Ben anaweza kufanya jambo lolote kwa ajili yao. Pia wanaongeza wana furaha kumpata mpenzi wao wa moyo, na wanafikiria mambo mengi ya badae kwa pamoja.
KITU GANI KINASABABISHA WASIFUNGE NDOA?
Mapacha hao pamoja na mpenzi wao waliodumu kwa miaka kumi na moja wanabainisha chanzo cha kutofunga ndoa ni kubanwa na sheria za nchi yao. Ben anasema sheria za Australia zinasema mwanaume hapaswi kuoa wake wawili. Lucy na Anna kwa sauti za kulalamika wanasema hawadhani kama ni sahihi sheria kuwa hivyo.
VIPI KUHUSU TENDO LA NDOA?
Wanaulizwa swali la kichokozi kidogo ambalo watu wengi walipenda wajue inakuwaje? Lucy na Anna wanaangaliana na kujiuliza wajibu vipi swali hilo, ”Ben kwa namna yake anajua kutufurahisha wote, ” anajibu Lucy na Anna anakubaliana naye.
Wanaeleza zaidi ikiwa Ben atafanya kitu kwa pacha mmoja katika ulimwengu huo wa mahaba lazima afanye vilevile kwa pacha mwingine. Mfano akimbusu pacha mmoja kwenye sikio na ambusu pacha mwingine hapo hapo. Wanasisitiza Ben anafahamu hilo na hakuna wakati mmoja wao atalalamika kutofanyiwa jambo ambalo mwingine hajafanyiwa.
Lucy na Anna pia wanatamani wapate ujauzito siku moja na wajifungue pamoja mapacha wa kufanana kama wao. Katika moja ya Reality show yao Ben anasema wanatafuta watoto kwa kipindi kimoja na ‘pressure’ ni kubwa. Hapa kweli Ben kazi anayo warembo wake wanataka ujauzito wakati mmoja.