Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hawa ‘Nitarejea’ wa Diamond alazwa Muhimbili

18332 HAWA+PIC TanzaniaWeb

Fri, 21 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Hali ya msanii wa Bongo Fleva, Hawa Said maarufu kama Hawa Nitarejea, imezidi kuwa mbaya na sasa inaelezwa kuwa amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).

Hawa ambaye amewahi kutamba na wimbo wa 'Nitarejea' alioshirikishwa na mwanamuziki Diamond Platnumz, kwa muda wa mwezi sasa amekuwa akisumbuliwa na tatizo la kujaa maji tumboni.

Akizungumza na MCL Digital, jana Septemba 19 nyumbani kwake Buguruni, mama wa Hawa, Ndagina Shabani, amesema hali ya mwanawe  ilibadilika juzi asubuhi ambapo walilazimika kumpeleka hospitali.

Ndagina amesema japokuwa alipangiwa tarehe ya kurudi hospitali kuwa Oktoba 17, 2018, lakini walishindwa kufika huko kutokana na hali yake kuzidi kudhoofu akilalamika tumbo kumuuma.

"Kwa kweli hiyo Oktoba kwetu imekuwa mbali kwani mtoto wangu kwa wiki nzima amekuwa hapati usingizi na afya yake kuzidi kudhoofu kila kukicha, hivyo juzi hali ilizidi kuwa mbaya ikabidi tumpeleke tu hospitali kwa matibabu zaidi,” amesema.

"Hata hivyo alipofika alinyonywa maji takribani lita nne na madaktari kushauri kuwa ni vyema akabaki hapo kwa uangalizi zaidi na hii ni mara ya nne sasa amekuwa akilazwa na kuruhusiwa.”

Mama yake Hawa anajishughulisha na biashara ya kupika vitafunio.

Pia, alitumia nafasi hiyo ya mahojiano kuwaomba Watanzania kumsaidia ikiwemo Serikali kwa kile alichoeleza kuwa imebidi asimamishe shughuli zake kwa ajili ya kumuuguza Hawa ambaye anahitaji uangalizi wa karibu na sasa ni takribani mwezi mmoja alikuwa akiugulia nyumbani.

Chanzo: mwananchi.co.tz