Duniani sherehe kubwa haswa za harusi zimepewa kipaumbele huku umati mkubwa ukifurika ukumbi huo wa harusi.
Hata hivyo, kuna wanandoa ambao wamefuata mkondo tofauti wa harusi ndogo za kibinafsi.
Ukumbi wao huwa na watu chini ya 50 ambapo kwa kawaida hawa huwa ni watu wanaojulikana nao; marafiki wa karibu, na ndugu na jamaa.
Licha ya ukumbi huo kuwa mdogo, upendo na furaha iliyoandikwa nyusoni mwa waalikwa na wanandoa. Ni mkutano wa kimapenzi ambapo kila wakati unathaminiwa, kila mawasiliano yanathaminiwa.
David na Naomi
Kutana nao kina Karani; David 30 na Naomi 39 ambao walifanya harusi ndogo Agosti 2019 iliyokuwa tu na watu chini ya 50. Bi Naomi anaeleza kuwa tangu awe msichana mdogo hakuwahi fikiria au hata kuota akifanya harusi kubwa.
“Haina maana kuwa na watu wengi ambao asilimia 70 huwajui na hutawahi kuwaona tena baadaye kisha unateseka sababu ya madeni,” akaongezea Bw David. Hata hivyo, mara kwa mara wengi wa wanafamilia hukerwa sana wasipoalikwa kwenye harusi huku wengine wakibeba uchungu huo kwa miaka.
Licha ya hayo, kina Karani hawakubabaishwa na wakachagua babu na nyanya zao waliowakilisha familia yote pamoja na shangazi na mjomba waliowasafirisha.
Ili harusi yao inoge, chakula kilikuwa chenye maana yake kwenye siku yao huku wanandoa hao wakizunguka hoteli kadhaa kuonja vyakula tofauti.
“Isitoshe, sababu ya umati mdogo, tuliweza kuzungumza kwa urefu na waliofika,” Bw David anaelezea.
Zaidi ya hayo, ili kuongeza mguso wa kibinafsi kwenye siku yao, Bi na Bw Karani walivaa aproni iliyoandikwa Bi na Bw kwa Kiingereza wakati wa maakuli na kuwaandalia wazazi wao chakula.
Hata ingawa harusi yao ilikuwa ndogo, kulikuwepo na changamoto wakipanga. “Marinda ya wasimamizi wangu hayangewatoshea na fundi alikuwa ameyaleta siku moja kabla ya siku ya harusi bila kukarabati ifaavyo. Ilitulazimu kumtafuta fundi mwingine huku msimamizi mkuu akinunua rinda lingine,” Bi Naomi anafafanua.
Kwa upande wake Bw David, alipoteza viatu vyake saa chache kabla siku ya harusi. “Niliacha viatu vyangu kwa rafiki yangu na hakuwa na ufunguo wake sasa ikanilazimu kutembea miguu peku kwa muda mrefu,” akaeleza.
Charlie na Melissa
Tofauti na kina Karani, kina Karumi (Charlie, 32, na Melissa 32) kuchagua wakualika kwenye harusi yao haikuwa changamoto hata kidogo.
Bw Charlie na Bi Melissa walifanya sherehe kubwa ya ulipaji mahari (ruracio) miezi kadhaa kabla ya harusi yao.
“Kitamaduni ruracio hubeba maana na ina uzito mkubwa kwa wazazi na wanafamilia wetu. Kwa hivyo baada ya hafla hiyo, wengi walijua kuwa wawili hao wameoana na hawakuwapa presha ya kufanya harusi nyingine,” anaeleza.
Kwao sasa kuchagua watakaokuwa kwenye harusi yao haikuwa jambo gumu. “Kila mtu aliyealikwa alikuwa akitujua kibinafsi, safari yetu ya mapenzi. Hakuna mtu aliyetambulishwa kwa mwenzake. Sote tulikuwa tukijuana,” akaongezea.
Wanandoa hao ambao walioana Septemba 2021, kwenye umati wa watu 40 pekee wanasema kuwa harusi yao ndogo ilichangiwa pia na kutaka kuguria nchini Canada.
“Hata hivyo, tulipokuwa tukipanga tulisahau kuwa na mfawidhi (MC) lakini rafiki yetu mmoja alijitokeza na kuongoza siku hiyo.”
Zaidi ya hayo, wawili hao walipunguza sana bajeti yao na kucheza nyimbo zao, kutolipia mapambo au hata kuwa na DJ.
Kwenye kumbukumbu zao, Bw Charlie anasema kuwa siku yao ya harusi ni moja itakayobaki mioyoni mwao milele kwani ni siku waliyozingiriwa na watu wenye maana maishani mwao.
Peter na Grace
Tofauti na kina Karani au Karumi, kina Nyaga (Peter 34, na Grace 30) walifanya harusi yao ndogo wakati wa covid-19.
“Hapo awali tulipanga kuwa na waalikwa angalau 700. Hata hivyo siku ya harusi yetu ilikuwa wakati homa ya covid ilikuwa imewashika watu wengi (Julai 17, 2020) huku mipango yetu ikiathirika. Ilitulazimu kufuata sheria ya kuwa tu na watu 15,” Bw Peter anafichua.
Kuchagua watakaoalikwa kwenye harusi yao kuliwalazimu kuwa na mazunguzmo marefu na wanafamilia wao.
“Tuliwaomba ndugu zetu wakubali tu kumtuma mtu mmoja ambaye angewawakilisha. Kwa hivyo tukawa tu na wazazi wetu, shangazi na mjomba mmoja kutoka pande zote, rafiki watatu, ndugu mmoja, kasisi na wahudumu 4,” anasema Bi Grace.
Hata ingawa harusi yao ilikuwa na watu wachache haikukosa changamoto za kupanga. “Baada ya nchi kutoruhusu watu kutoka ndani au nje, hoteli tuliyokuwa tumehifadhi na kulipia kwa ajili ya fungate yetu ilifunga kabisa na hatungeweza kuwasiliana nao,” anakumbuka Bw Peter.
Hata hivyo, siku yao ilikuwa na kumbukumbu za aina yake huku wote waliooalikwa wakitoshea kwenye albamu ya picha. “Waalikwa walipata keki nyingi na wengine wakaibeba nyumbani kwao,” anaongezea Bi Grace.
Licha ya kuwa na waalikwa wachache, kina Nyaga walisherehekea, wakajibamba na hata kujiburudisha sana. Mafanikio ya siku yao ni kuwa na ndugu, jamaa na marafiki wao karibu nao.
“Hata ingawa hatukuwa tumepangia mabadiliko hayo, kufanya harusi ndogo ilituokolea kifedha,” Bw Peter anasema.
Kwa mujibu wa Abigael Ojwang, mpangaji wa harusi ndogo, lengo la harusi za aina hii nikusherehekea pamoja na waalikwa unaowajua na kutengeneza kumbukumbu. “Kila wakati unafikiria kuhusu harusi yako, unapaswa kukumbuka waalikwa, chakula, kasumba za watu na hata mazungumzo mliokuwa nayo,” anasema.
Isitoshe, Bi Ojwang, mwanzilishi wa Dhahabu Wedding Planners, anafafanua kuwa bajeti si kigezo kikuu cha harusi hizi.
“Nimewahi panga harusi ya milioni 1 na ilikuwa tu na watu 50. Harusi hizi ndogo huboreshwa na mapambo, rangi na hata ukumbi wake.”
Ili kujua watakaoalikwa, Bi Ojwang hushauri wanandoa kuchagua tu watu wale ambao wanaushirikiano wa kila siku nao.
“Unazungumza na nani zaidi? Unafungukia nani sana wakati mambo yamekulemea au ukiwa na furaha? Una uhusiano wa karibu na nani?” maswali kama haya ndiyo humwezesha mtu kuchagua wageni wake.