Rekodi lebo ya Konde Music Worldwide inapita katika tanuru la moto kiasi kwamba wasanii wake wameshindwa kutoa nyimbo na hata baadhi ya zilizotoka hazijawekwa kwenye majukwaa yote ya kidigitali (digital platforms) kama ulivyo utaratibu.
Kwa mujibu wa Harmonize, ni muda sasa hawajapokea fedha yoyote ya uchapishaji na usambazaji (publishing rights) wa muziki wao kutoka kwa kampuni moja iliyokuwa inasambaza kazi zao.
Utakumbuka Konde Music ilianzishwa Oktoba 10, 2019 ikiwa ni muda mfupi baada ya Harmonize kuachana na WCB Wasafi yake Diamond Platnumz ambayo ndiyo iliyomtoa kimuziki mwaka 2015.
Ibrah ndiye alikuwa msanii wa kwanza kusainiwa kisha wakafuata wengine kama Country Boy, Cheed, Killy, Anjella na Young Skales kutokea nchini Nigeria.
Kutokana na kutopata fedha zake ambazo kwa muda amekuwa akizililia kupitia mitandao ya kijamii, Harmonize amefikia hatua kusema kuwa muziki wake mpya utapatikana You Tube pekee hadi pale suala hilo litakapotatuliwa.
Nyimbo tatu mpya za Harmonize, Hawaniwezi, Dear EX na Tena ambazo zimetoka hivi karibuni hazipatikani jukwaa lolote la kidigitali zaidi ya YouTube, huo ni msimamo wa Harmonize hadi pale mambo yatakapokaa sawa.
Kwa mwaka huu ni nyimbo tatu tu za Harmonize ambazo zimewekwa kwenye majukwaa yote ambazo ni Single Again, Zanzibar na Morning Call.
Hata hivyo, Harmonize anadai hajaingiza fedha yoyote kupitia wimbo wake, Single Again licha ya kufanya vizuri duniani, bado Baraza la Sanaa Taifa (Basata) na Taasisi ya Hakimiliki Tanzania (Cosota) wanaendelea kushughulikia suala hilo.
“Pata picha sijawahi kuingiza hata dola moja (wastani wa Sh2,400) kupitia wimbo ‘Single Again’ licha ya kuwa wimbo mkubwa duniani,” alieleza Harmonize mapema mwezi huu.
Kauli hiyo ya Harmonize inakuja baada ya Februari mwaka huu kudai zaidi ya Sh100 milioni, zimepigwa kupitia wimbo wake, Kwangwaru (2018) aliomshirikisha Diamond, fedha hizo zimeishia mikononi mwa hao anaowalalamikia.
Harmonize alienda mbali zaidi na kudai ataacha muziki ili wanaofanya hivyo wafurahi, alisema anahitaji maisha mazuri kufanya kazi kwa bidii na muziki upo kwa ajili ya kesho yake.
“Naacha basi muziki wenyewe mfurahi, nina uhakika hakuna Prodyuza yeyote anayepata haki za uchapishaji wa kazi zake na lawama zote zinaenda kwa wasanii, ni muda wa kuacha sasa msitumie madhaifu ya watu kujinufaisha,” alieleza Harmonize.
Utakumbuka Vanessa ambaye aliachana na Bongo fleva kwa madai ya kutomlipa kulingana na jitihada na uwekezaji wake, Agosti 2022 naye aliilalamikia kampuni moja kutomlipa fedha zake.
“Pesa ya muziki zinatafutwa kwa shida na wasanii kuanzia kubuni hadi ifikapo kwa wananchi, tafadhali nawaomba mnilipe pesa zangu kwa makubaliano tulionayo, nimejaribu ‘the professional way’ na timu yangu sasa imefikia hatua ya nyie kutojibu,” alieleza Vanessa.
Tayari Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini Tanzania, Hamisi Mwinjuma ‘Mwana FA’ ambaye naye ni msanii wa Bongofleva, ameelekeza wasanii wanaodai kudhulumiwa kupatiwa haki zao mara moja.
Hilo ndilo limepelekea ukimya wa Ibrah ambaye ndiye msanii pekee aliyebaki chini ya Konde Music. Tangu mwaka umeanza hadi sasa, Ibrah ametoa nyimbo mbili tu, Nimepona na Tunapendeza ikiwa ni mara ya kwanza kuwa kimya hivyo kwa muda mrefu.
“Chinga (Ibrah) anarudi, wamezuia mapato yake pamoja na ripoti zote miezi minane sasa bila sababu yoyote, serikali inalifanyia kazi suala la Ibrah najua mnasubiri sana,” alieleza Harmonize.
Utakumbuka hadi sasa Ibrah ametoa EP moja, Steps (2020) na albamu moja, The King of New School (2022), akiwashirikisha Maud Elka, Christian Bella, L.A.X, Waje, AV, Roberto na Bracket.
Ni miongoni mwa wasanii waliofanya vizuri zaidi miaka miwili iliyopita ila sasa muziki wake unapitia changamoto, katika orodha ya wasanii wa Tanzania waliopokea mirabaha kwa mwaka 2022 Ibrah alikamata nafasi ya nne akikabidhiwa kitita cha Sh4.5 milioni.
Wakati hayo yanaendelea, hivi karibuni mpigapicha wa Harmonize, Jabulant ambaye walifanya kazi pamoja kwa zaidi miaka minne, alitangaza kuacha kazi Konde Music, suala la maslahi limekuwa likitajwa kusababisha uamuzi huo.
Harmonize katika wimbo wake, Leave Me Alone (2022) akimshirikisha Abigail Chams, alisema katika muziki wake sasa hahitaji wapambe kama Mwijaku, H. Baba na Baba Levo, hiyo ni baada ya watu hao kuachana naye na kuungana na mahasimu wake kimuziki.
H. Baba ambaye walishirikiana kwenye wimbo, Attitude (2021) na Awilo Longomba kutokea DR Congo, amekuwa akidai kuwa hakulipwa kwa kufanya kolabo hiyo ingawa Awilo alipewa fedha zake zote.
Na Attitude ni kati ya nyimbo za Harmonize zilizofanya vizuri sana upande mauzo kwenye majukwaa ya kidigitali na ulishinda tuzo za Muziki Tanzania (TMA) 2021 kama Wimbo Bora wa Kushirikiana Afrika.
Ikumbukwe mwaka uliopita Konde Music ilivunja mikataba na wasanii wake watatu, Anjella, Cheed na Killy, ambao katika mahojiano mbalimbali wamekuwa wakidai kutolipwa fidia ingawa mkataba wao ulieleza kama msanii angevunja mkataba basi angeilipa fidia lebo hiyo.