Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Harmonize atoa sababu ya kugawa bure nguo zake

90193 Harmonizepic Harmonize atoa sababu ya kugawa bure nguo zake

Mon, 30 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Ushawahi itamani nguo yangu yeyote? Hilo ni swali kutoka kwa msanii wa Tanzania Harmonize kuelekea kuufunga mwaka 2019.

Harmonize ambaye jina lake halisi ni Rajabu Abdul, Desemba 31, 2019 anatarajiwa kukutana na wakazi wa Mtwara ikiwamo Tandahimba eneo alikozaliwa na kufanya shoo ya kufunga mwaka.

Pamoja na mambo mengine ikiwamo kuwapa mkono wa heri ya mwaka mpya 2020 wakazi wa mkoani Mtwara, pia ametangaza kuwapo kwa tukio la kugawa nguo zake bure, shughuli itakayofanyika nyumbani kwao Tandahimba sokoni.

Harmonize anayafanya haya ikiwa ni siku chache tangu Rais wa Tanzania, John Magufuli kumtamkia kwamba angetamani siku moja msanii huyo agombee jimbo la Tandahimba, jambo ambalo Harmonize alisema analifanyia kazi.

Oktoba 15, 2019 akiwa katika mkutanao wa hadhara mjini Ruangwa, Rais Magufuli alimsifia msanii huyo kwa kazi yake ya kuburudisha na kusema anatamani agombee katika jimbo hilo na kuwa mbunge. Jimbo hilo kwa sasa linaongozwa na Katani Katani wa CUF.

Tukio hilo la ugawaji nguo alilolipa jina la ‘Kondeboy Gala, alilitangaza kupitia ukurasa wake wa Instagram kwa kuandika, “wacha nikujuze hili kama hujajua. Sehemu kubwa inayokula pesa ya msanii yeyote duniani ni mavazi, namaanisha nguo viatu sijui makofia cheni, mara pete.”

“Nguo za gharama  kwa msanii huwezi kuzikwepa ni lazima ununue kila siku na ubaya wake ni kwamba ukishavaa mara moja ukapiga picha na kupost instagram ikitrend huirudii tena.!! kesho unanunua nyingine.”

“Hivyo basi nimekuwa katika muziki kwa miaka mitano sasa na kila siku ziendazo kwa Mungu nanunua nguo,” amesema

Msanii huyo amesema, “kwa kuwa Desemba 31 ni siku special (maalum) kwangu na ndugu zangu wa nyumbani nimefikiria nifanye Kondeboygala ambalo litakuwa na nguo zote nilizoanza kununua na kuvaa kuanzia mwaka 2015 mpaka 2019 nitazigawa pale nyumbani Tandahimba Sokoni bure.”

“Hivyo  kama kuna nguo umeiona kwenye video..!! picha..!!! popote pale yeyote we njoo pale nitakupatia bure hutolipia hata shilingi,” ameandika Harmonize.

Menja wa msanii huyo Beauty Mmari maarufu 'Mjerumani amesema hilo ni moja ya matukio Harmonize atakayowafanyia wakazi wa mkoa wa Mtwara ikiwa ni kuonyesha shukurani kwao kwa kumuunga mkono.

“Siku zote Harmonize huthamini alikotoka, ndiyo maana ameamua kufanya yote haya, siyo mwisho kutakuwa na vitu vingi vya kushtukiza vitafanyika siku hiyo,” amesema Mjerumani.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz