Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Harmonize aomba radhi baada ya kuimba kuhusu bangi

Harmonize Bangi Harmonize

Thu, 8 Dec 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Staa wa Bongo Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize ameomba radhi kutokana na wimbo wake na mwimbaji wa  dancehall wa Jamaica, Konshens  ‘Weed Language’, siku moja tu baada ya kupokea onyo kali kutoka kwa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini Tanzania (DCEA).

Siku ya Jumatano, Kamishna Mkuu wa DCEA, Bw Gerald Kusaya alionya kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wanamuziki wanaotunga nyimbo za kuhamasisha matumizi ya dawa za kulevya.

"Kuna wasanii wanahamasisha matumizi ya dawa za kulevya ikiwemo bangi. Kama kuna wasaniii wanaodhani badala ya kutunga nyimbo za kuhamasisha jamii, wanatunga za kuhamasisha matumizi ya dawa za kulevya, sheria yetu inasema hao tutawachukulia hatua," Bw Kusaya aliwaambia waandishi wa habari.

Onyo hilo linaonekana kuzua hofu kwa Harmonize ambaye Alhamisi asubuhi aliomba radhi hadharani kupitia taarifa iliyoandikwa.

Mwimbaji huyo mahiri, kupitia lebo yake ya Konde Music Worldwide alisisitiza kuwa wimbo wake 'Weed Language' ulikuwa na lengo la kuupanua na kuukuza muziki wa Tanzania duniani kote lakini ulitafsiriwa isivyofaa.

"Kutokana na kadhia iliyosababishwa na maudhui ya wimbo huo tunaomba radhi na tunaahidi kuuondoa wimbo huo kwenye mitandaoyote ya kijamii," taarifa kutoka kwa usimamizi wa Konde Music Worldwide ilisoma.

Waliongeza, "Pia tunaahidi kuboresha nyimbo zetu ili ziendane na utamaduni wetu pamoja na miongozo ya mamlaka ya serikali." 

Hapo awali, Harmonize akiwa na meneja wake Choppa TZ walikutana na BASATA kuzungumzia muziki wake.

"Shukrani sana!! Baraza La Sanaa @basata.tanzania Kwa Hakika Tumezungumza Mengi! Yenye Tija Kubwa kwa maslahi ya taifa kama vijana tunaahidi kutekeleza," Harmonize alisema baada ya mkutano huo.

Katika taaifa yake Jumatano,Kusaya alimtaja msanii fulani ambaye alisema amekuwa akijaribu kujipatia umaarufu kwa kuhamasisha matumizi ya dawa za kulevya na akatoa tahadhari kuwa atachukuliwa hatua za kisheria hivi karibuni.

"Mbona mashairi yapo ya aina nyingi unashindwaje kutunga mashairi ya vitu vyote??  Si wahamasishe hata kilimo bora au biashara, kwani lazima wahamasishe mambo ya bangi? hatutoruhusu Mtanzania yoyote afanye uhamasishaji wa matumizi ya dawa za kulevya," alisema Bw  Kusaya.

Wiki jana Harmonize aliachia kibao 'Weed Language' ambacho alimshikisha msanii wa Jamaica, Konshens.

Katika wimbo huo ambao tayari umefutwa, mastaa hao wawili wa muziki wanazungumzia bangi na kuangazia majina tofauti ambayo mataifa mbalimbali yanaita dawa hiyo ambayo ni haramu Afrika Mashariki.

“Unaitaje bangi kwa lugha yako,” anasema Harmonize kwenye ubeti wake wa wimbo huo.

Katika ubeti wake, Konshens anaimba kuhusu jinsi wanavyoita bangi katika nchi yake ya Jamaica na kuhusu mapenzi yake kwa mihadarati hiyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live