Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Harmonize ana haki kudai Sh mil 100 kwa kolabo

Harmonize Mla Harmonize

Mon, 9 Jan 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Rapa wa Marekani Jay Z aliwahi kuiambia MTV kuwa mara ya mwisho kuandika mashairi ilikuwa mwaka 1996 alipoandika wimbo wake ‘Can I Live’ unaopatikana katika albamu yake ya kwanza, Reasonable Doubt iliyotoka Juni 25, 1996.

Jay Z anadai tangu wakati huo amekuwa akikariri mashairi yake na kwenda kurekodi, hana utaratibu wa kuandika popote pale, iwe kwenye karatasi au sehemu nyingine, yeye yapo kichwani tu.

Kipindi anaandaa albamu yake ya sita, The Blueprint iliyoachiwa Septemba 11, 2001 chini ya Roc-A-Fella Records na Def Jam Recordings, Jay Z aliandika na kurekodi nyimbo tisa ndani ya siku mbili tu!.

“Nyimbo hizi zilianza kutoka tu nisiko kujua, nilichonacho ni kipaji kutoka kwa Mwenyenzi Mungu, hakiwezi kuelezewa,” alisema Jay Z katika mahojiano na Jarida la Rolling Stone.

Staa wa Bongo kutoka Konde Music, Harmonize anaishi katika ulimwengu huo, bila kujali hali halisi, ni wazi mwaka 2022 unampa kila sababu kudai Sh100 milioni kwa ajili ya kufanya kolabo na msanii mwingine kama alivyoeleza!.

Mwaka huu Harmonize ameshirikishwa na wasanii 13 katika nyimbo zao na ndiye msanii aliyefanya kolabo nyingi zaidi akiwa anafuatiwa na Marioo, Phina (Saraphina) ambaye ameongoza upande wa wasanii wa kike.

“Nimeanza kutoza Sh100 milioni kwa kufanya kolabo, sharti ngoma iwe kali,” alieleza Harmonize.

Hata hivyo, kumekuwa na maswali ni wasanii wangapi Tanzania wana uwezo wa kulipa kiasi hicho cha fedha au Harmonize alitoa kauli hiyo kwa lengo lingine tofauti na inavyoonekana kwa nje.

Ni wazi uwezo wake wa kuandika mashahiri ni mzuri na ndio sababu ya kupata nafasi hiyo zaidi, na pengine sauti yake ni bidhaa inayouzika kwa urahisi katika soko la Bongofleva. Kama ni hivyo, basi ana kila sababu ya kuhitaji Sh100 milioni kwa ajili ya kolabo.

Kolabo 13 za Harmonize kwa mwaka 2022 pekee!.

1. Addiction – Ibraah ft. Harmonize.

2. Band Man – Tundaman ft. Harmonize.

3. Closer – Abigail Chams ft. Harmonize.

4. Championi Remix – Kontawa ft. Harmonize.

5. Follow Me – Aslay ft. Harmonize.

6. Furaha Remix – Iyanii ft. Harmonize.

7. Kioo – Anjella ft. Harmonize.

8. Konkodi – Cheed ft. Harmonize.

9. My Baby – Roberto ft. Harmonize.

10. Naongopa – Marioo ft. Harmonize.11. Ni Wewe – Killy ft. Harmonize.

12. Sio Kwa Ubaya – Mwana FA ft. Harmonize.

13. Utamu Remix – Mabantu ft. Harmonize.

Kati ya hizo 13, ni kolabo tatu tu ambazo Harmonize amefanya na wasanii wa lebo yake, Konde Music, hii ni ishara kuwa anajitoa zaidi hata pale ambapo ni vigumu kusema siku mbele atakuja kuchukua fedha ya mauzo ya muziki huo.

Wasanii wakubwa wenye lebo Bongo walikuwa wakinyooshewa vidole kuwa wanawabeba wasanii walio kwenye lebo zao kwa kufanya nao kolabo tu ila kwa Harmonize ameonyesha kitu cha tofauti kwa mwaka 2022.

Chid Benzi ndiye anatajwa kuwa msanii aliyefanya kolabo nyingi Bongo miaka ya hivi karibuni, amesikika kwenye ngoma za wasanii kama Diamond Platnumz, Alikiba, AY, Ray C, Profesa Jay, Lady Jaydee, Ferous, Mwasiti, Marlaw na Tundaman.

Wengine ni Spack, Angeline, Ben Pol, TID, Nikki Mbishi, Stereo, One The Incredible, Songa, Mwana FA, Mansu-Lii, Baba Johnii, Country Boy, Climax Bibo, Young Dee, Geez Mabovu, Makamua, Langa, Mhe. Temba na wengineo.

Ikumbukwe Oktoba mwaka huu Harmonize aliaachia albamu yake ya tatu, Made For Us, yenye nyimbo 18 ikiwa ni albamu yake ya pili ndani ya miezi 11.

Hiyo ni baada ya Novemba 2021 kutoa albamu yake ya pili, High School yenye ngoma 20, ukiwa ni mwaka mmoja baada ya kutoa albamu ya kwanza, Afro East iliyotoka Machi 2020 ikiwa na ngoma 18.

Kwa ujumla ndani ya miaka mitatu, Harmonize katoa albamu tatu zenye jumla ya nyimbo 56, huku nyimbo zake kama Mwaka Wangu, Wishes, Bakharesa, Omoyo Remix na Attitude zikiwa hazipo kwenye albamu hizo.

Ni wasanii wachache sana wenye uwezo kama huo, unahitajika uwezo na ubunifu wa ziada katika utunzi wa mashairi ili mashabiki waendelea kuwa na kiu ya kusikiliza muziki. Na kufanya hivyo ni kipaji tu kutoka kwa Mwenyenzi Mungu kama alivyosema Jay Z, hakiwezi kuelezewa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live