Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Harmonize alivyojipakulia minyama tuzo za AEAUSA

Rayvanny Mdas Harmonize alivyojipakulia minyama tuzo za AEAUSA

Wed, 22 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Hapo juzi Harmonize aliwasili nchini akitokea Marekani aliposhinda tuzo tatu za African Entertainment Awards USA, kisha kuzitembeza tuzo hizo katika mitaa mbalimbali jijini Dar es Salaam ikiwemo Kariakoo alipokutana na mashabiki wengi.

Harmonize alishinda katika vipengele vya Msanii wa Mwaka, Video Bora ya Mwaka kupitia kibao ‘Single Again’ pamoja Mfalme wa Afro-Bongo Afrika Mashariki.

Kwa namna Harmonize alivyofanya sherehe ya ushindi wake huo, unaweza kudhani hakuna msanii aliyewahi kushinda tuzo hizo au yeye ndiye aliyeshinda mara nyingi zaidi kitu ambacho sio kweli. Hata hivyo, ukweli ni kwamba Harmonize ameamua kujipakulia minyama katika tuzo hizi ambazo wasanii na wadau zaidi ya 15 kutoka katika tasnia ya burudani Bongo wamewahi kuzishinda kwa sababu kuu mbili.

Mosi; yeye ndiye msanii wa kwanza Bongo kushinda tuzo tatu kwa mpigo za AEAUSA, pili; ni kutokana na kukaa muda mrefu bila kushinda tuzo, mara mwisho ilikuwa mwaka 2016 aliposhinda kama Msanii Bora Chipukizi na ndio ilikuwa mara yake ya kwanza.

Utakumbuka tuzo za AEAUSA zilianza kutolewa Oktoba 2015 huko New Jersey, Marekani zikiwa na vipengele 30 kuhusu muziki na mambo mengine kwa wasanii na watu wengine wa Afrika katika tasnia ya burudani.

Harmonize anajipakulia minyama wakati anajua bado ana kibarua kizito mbele ya Diamond Platnumz ambaye ndiye kinara wa tuzo hizo upande wa Bongo hadi sasa.

Diamond ameshinda tuzo nane za AEAUSA tangu mwaka 2015 hadi 2022, ni vipengele viwili tu alivyoshinda Harmonize ambavyo Diamond hajatia mkononi tuzo zake. Navyo ni Msanii Bora Chipukizi na hicho cha Mfalme wa Afro-Bongo Afrika Mashariki ambacho ni kipya.

Ila kama ni Msanii wa Mwaka, Diamond kashinda mara tatu, 2018, 2020, 2021, kama Wimbo Bora, Diamond kashinda mara mbili, 2016 na 2016 kupitia ngoma ‘Nitampata Wapi’ na ‘Utanipenda’.

Hata hivyo, kitendo cha Harmonize kushinda tuzo kimemfanya kufikisha tuzo nne za AEAUSA sawa na Rayvanny aliyekuwa amemtangulia, huku akimpita Nandy ambaye amesalia na tuzo zake tatu.

Wanamuziki wengine Bongo waliowahi kushida tuzo hizo ni pamoja na Yamoto Band (2016), AY (2016), Alikiba (2017) na Navy Kenzo (2017).

Watanzania wengine kutoka kiwanda cha burudani ni DMK Global (2015), DJ D-Ommy (2016), Habibu Bajuni (2018), RJ The DJ (2018), Babu Tale (2019), Lil Ommy (2019), DJ Sinyorita (2020) na Director Kenny (2021).

Chanzo: Mwanaspoti