Mwanamuziki Rajab Abdul maarufu Harmonize jana, Februari 6 alishikiliwa kwa zaidi ya saa tano katika Kituo cha Polisi Central, jijini Dar es Salaam alipokwenda kujisalimisha akituhumiwa kuvuta kitu kinachofanana na kinachotoa moshi alipokuwa nchini Ghana hivi karibuni.
Akizungumza na wasanii mwishoni mwa wiki iliyopita katika viwanja vya Leaders Club, mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alisema ameagiza mwanamuziki huyo anayetamba na wimbo Paranawe achunguzwe baada ya kuweka picha inayomuonyesha akivuta kitu kinachotoa moshi.
Makonda alisema alimwagiza Gavana wa kule amchunguze alichokuwa akivuta na kama ikithibitika kilikuwa na kilevi angemweka ndani.
Makonda ambaye ni mlezi wa lebo ya WCB inayomilikiwa na mwanamuziki Diamond, alisema kama mzazi angemwajibisha kwa kumweka ndani Harmonize ambaye ni sawa na mwanaye, iwapo itathibitika kuwa kilikuwa kilevi.
Mwanamuziki huyo anayetamba na wimbo Kwangwaru aliwasili katika kituo hicho akiwa amejifunika kichwani kwa kuvaa sweta jeusi na miwani.
Alipofika kituoni hapo alitimua mbio huku akiwafurusha waandishi waliokuwa wakijaribu kumpiga picha.