Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hapa ndipo ulipo uchoyo wa Zuchu

E8409D49 FFB8 43AF 9B3A C8F4E6DC52E0.jpeg Zuchu

Sun, 12 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Moyo huficha siri ambazo kwa macho huzioni, kwa vile mie sio mchoyo nitakupa jambo jipya sikioni. Anachana Fid Q katika wimbo wake wa ‘Juhudi za Wasiojiweza’ kutoka albamu yake ya pili, Propaganda (2009) akimshirisha Bi Kidude.

Ndivyo ilivyo kwa Staa wa Bongofleva, Zuchu ambaye ni takribani miaka mitatu tangu kusainiwa WCB ya Diamond akiwa ni msanii wa pili wa kike wa Lebo hiyo baada ya Queen Darleen.

Binti huyo wa Malkia wa Taarab nchini, Khadija Kopa, ndiye kiziwanda wa WCB kwani tangu asainiwe Aprili 2020 hakuna mwingine aliyetambulishwa, japo hivi karibuni inadiwa kuna msanii mpya atatumbulishwa mwaka huu.

Hanstone ndiye alikuwa anatajwa angefuata muda mfupi baada ya Zuchu, ila mambo kati yake na WCB yakavurugika na sasa Mavokali anatajwa kuchukua nafasi.

Uwekezaji uliofanywa kwa Zuchu umemfanya kuwa staa mkubwa wa muziki Afrika Mashariki kwa muda mfupi, ndiye msanii wa kwanza wa kike ukanda huo video ya wimbo wake (Sukari) kupata ‘views zaidi ya 80 milioni YouTube, huku ikiwa ngoma pekee ya solo yenye mafanikio hayo.

Pia ndiye msanii wa kwanza wa kike Afrika Mashariki kufikisha views 100 milioni YouTube kisha akafuata Nandy, pia ndiye wa kwanza kufikisha streams 100 milioni Boomplay Music.

Utakumbuka EP yake I Am Zuchu yenye nyimbo saba ilikaa tano bora chati za Boomplay Album kwa wiki 75, huku ukishika namba moja kwa wiki 35, hakuna msanii wa kike Afrika Mashariki mwenye rekodi hiyo, ni Zuchu pekee.

Hadi sasa Zuchu amefikisha views zaidi ya 431.0 milioni YouTube na kuwa msanii wa kike namba tatu Kusini mwa Jangwa la Sahara, akitanguliwa na Sinach (views 721.7 milioni) na Yemi Alade (694.4 milioni), wote ni Nigeria.

Zuchu ameshinda tuzo mbili za African Muzik Magazine (AFRIMMA) kama Msanii Bora Chipukizi (2020) na Msanii Bora wa Kike Afrika Mashariki (2022), huku akiteuliwa kuwania MTV Europe Music Awards (MTV EMA) 2022.

Pengine mafanikio ya muda mfupi yamemfanya Zuchu kuwa mbinafsi sana, kama sio yeye, basi WCB ndio wamemfanya awe hivyo ili kulinda chapa yake kutozoeleka na kuchokwa mapema katika soko. Je, ni kwa namna gani na kwanini?.

Tangu ametoboa, Zuchu hashirikishi kabisa wasanii wa Bongofleva nje ya WCB katika ngoma zake, hata wa WCB waliopata nafasi hiyo ni Diamond na Mbosso licha ya kuikuta Lebo hiyo ikiwa na wasanii watano.

Kwa ujumla wasanii wa Tanzania ambao Zuchu amewahi kuwashirikisha ni watatu tu; Diamond, Mbosso na Khadija Kopa, huku wa kimataifa wakiwa ni wanne; Joeboy na Adekunle Gold kutokea Nigeria, pia kuna Bontle Smith na Tyler ICU wa Afrika Kusini.

Jux ndiye msanii pekee nchini nje ya Lebo ya WCB aliyeinasa sauti ya Zuchu anayesikika kwenye wimbo wa ‘Nidhibithiti’ uliopo katika albamu ya pili, King of Hearts (2022).

Hakuna ubishi, Jux ameweza hilo kutokana na ukaribu wake wa kikazi na Diamond anayesikika kwenye wimbo wa ‘Sugua’ unaopatikana katika albamu yake ya kwanza, The Love Album (2020).

Kwa asilimia kubwa Zuchu anacheza uwanja wa nyumbani; WCB, huku ni Diamond, Mbosso na Rayvanny pekee ndio wamemshirikisha, Lava Lava na Queen Darleen bado wanasotea benchi.

Hadi sasa Mondi ndiye pekee aliyefanya kolabo nyingi na Zuchu tatu; ‘Litawachoma’ na ‘Cheche’ zake binafsi na ‘Mtasubiri’ kutoka kwenye EP ya Chibu, First of All (FOA).

Pengine Zuchu na WCB wanajua nguvu ya ushawishi alinayo kwa sasa, hivyo wameamua upepo huo uwanufaishe wao pekee, mathalani, wimbo ‘Mtasubiri’ ndio uliofanya vizuri zaidi katika EP ya Diamond, video yake ndio iliyoongoza kutazamwa YouTube Tanzania mwaka 2022 ikiwa na viewsí zaidi 23 milioni.

Rayvanny kabla ya kuondoka WCB alimshirikisha Zuchu katika nyimbo mbili, ni mfano halisi wa jambo hilo, video ya kolabo yao Number One, ndio video pekee ya Rayvanny iliyotazamwa zaidi YouTube kwa muda wote ikiwa na views zaidi 75 milioni ikiwa ni miaka miwili tangu kutoka kwake.

Hivyo hivyo upande wa kimataifa, ni wasanii wawili tu waliobahatika kuinasa sauti yake; Spice Diana (Uganda) na Olakira (Nigeria), hivyo kupata sauti ya Zuchu sio rahisi na siri ambazo kwa macho huzioni kama alivyoeleza Fid Q katika Juhudi za Wasiojiweza.

Ikumbukwe kipindi cha nyuma baada ya Diamond kuanza kuwasaini wasanii WCB mnamo mwaka 2015, alikosolewa sana kwa tabia yake ya kufanya kazi na wasanii wa lebo hiyo pekee ndani ya Bongofleva, ila baadaye akabadilika ndipo akaja kusikika kwenye ngoma za wasanii kama AY, Fid Q, Navy Kenzo, Jux, Baba Levo na Barnaba.

Chanzo: Mwanaspoti