Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hadithi ya Aibumwiko na wanamuziki wa Mwongopee

46983 Anko+kitime

Mon, 18 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Leo hebu niwape hadithi ya nchi ya kufikirika iliyoitwa Mwongopee. Ilikuwa ni nchi yenye watu wachangamfu waliopenda sana muziki. Kulikuwa na wapenzi wa muziki wa kila mahadhi.

Awali nchi hii ilikuwa na kumbi nyingi za muziki na kwa kweli popote pale nchini kuanzia siku ya Jumatano mpaka Jumapili, lazima ungekuta wanamuziki wanakesha kufurahisha wapenzi wao. Mfalme wa Mwongopee naye alipenda sana muziki na si mara moja alijitokeza na kufurahi na wananchi wake katika ukumbi mmoja au mwingine.

Pamoja na kuwa wananchi wa Mwongopee walipenda sana muziki, wanamuziki wa Mwongopee walijikuta wakiwa maskini miaka nenda rudi.

Kazi zao walizorekodi ziliishia mikononi mwa wasambazaji wasio halali waliochapisha na kuziuza nchi nzima bila makubaliano.

Walianza kutumia mbinu mbalimbali za kumbembeleza mfalme aweke sheria ya kulinda kazi zao, lakini miaka ikawa inakatika mfalme akabaki kimya.

Lakini kelele za wanamuziki hawa zikawafanya baadhi ya wafanyabiashara wa Mwongopee wakubali kuwalipa fedha kiasi kwa CD ambazo wangekubaliana kuzisambaza, hivyo kidogo kukawa na ahueni kwa wale ambao kazi zao zilikuwa zikisambazwa.

Wakati hali hii ikiendelea, kijana mmoja mkazi wa Fujofujoni, mji mkuu wa Mwongopee akapata wazo la kuingia katika biashara ya muziki. Hakutaka biashara ya kupiga muziki wala kusambaza muziki. Kijana huyu aliyejipa jina Aibumwiko aliwaendea wasambazaji na kuwaambia kuwa anachotaka ni kazi ya kutangaza vizuri albamu zao zinazouzwa ili wasambazaji wapate biashara nzuri.

Hakika wafanyabiashara wakafurahi sana, Aibumwiko akawapa sharti moja tu kuwa ili kazi yao ifanyike vizuri wasikubali kusambaza kazi ambayo yeye hajaipitisha. Hili nalo likakubaliwa, wakakubaliana kuwa Aibumwiko atakuwa anapata mgawo kwa kila CD inayouzwa.

Biashara ikaanza na muda si mrefu wanamuziki wakaelewa kuwa bila kazi zao kupitia kwa Aibumwiko wasambazaji hawashughuliki nazo.

Aibumwiko akawa muhimu sana kwa wanamuziki wa Mwongopee. Jina la Aibumwiko na utajiri wake ukaanza kukua. Wanamuziki wakaanza hata kuwahonga marafiki na ndugu wa Aibumwiko ili kazi zao zikubaliwe kusambazwa. Wanamuziki wengi wakakata tamaa kwani usipopendwa au usiposikilizwa na Aibumwiko hata ungekuwa na muziki wenye ubora gani ilikuwa kazi bure.

Aibumwiko akawa na nguvu sana dhidi ya wanamuziki, akaanza kufanya matamasha makubwa kwa kutumia wanamuziki hao, akawa anawalipa pesa kidogo na wao wakijiridhisha kuwa ni faida kubwa kuwa tu karibu na Aibumwiko.

Kwa kuwa wananchi wa Mwongopee walipenda sana muziki matamasha yakawa yanaweza kukusanya maelfu ya watu. Kampuni zilimgombania Aibumwiko ili kutumia nguvu zake kutangaza bidhaa zao. Wanasiasa nao wakamgombania kwani alikuwa na uwezo wa kukusanya watu wengi kwenye mikutano kwa kutumia wanamuziki hao.

Naye mfalme akawa karibu na Aibumwiko. Akawa mshauri mkuu wa mfalme katika mambo ya muziki. Kwa kuwa Aibumwiko alikuwa mjanja sana akaanza kumshauri mfalme sheria ambazo alimhakikishia kuwa zitaondoa kero na kuwafaidisha wanamuziki.

Mfalme akamsikiliza na kupitisha sheria hizo alizodhani zitawalinda wanamuziki. Sheria hizi zikaishia kuwaondoa wasambazaji ambao walikuwa maswahiba wa zamani wa Aibumwiko na hivyo kuwaacha wanamuziki wakiwa na njia moja tu ya kuingiza kipato nayo ilikuwa ni kutegemea mialiko ya matamasha aliyotayarisha Aibumwiko. Nguvu ya Aibumwiko dhidi ya wanamuziki ikaongezeka maradufu.

Aibumwiko hakuwa tena mtu wa mchezomchezo, balaa kubwa lilimkuta mwanamuziki aliyejaribu kumpinga Aibumwiko, kampuni za biashara zilikataa kudhamini kazi za mwanamuziki wa aina hiyo kwa kuogopa kumuudhi Aibumwiko, ambaye alikuwa akiwapa mgawo mzuri mameneja masoko kila walipodhamini kazi zake. Balaa liliendelea kwenye redio za nchi ile ambazo Aibumwiko aliweza kuziteka kwa kuwalipa baadhi ya watangazaji fedha za ziada ilimradi tu watimize matakwa yake, nako huko muziki wa aliyempinga Aibumwiko uliacha kupigwa, na hivyo kumuondoa kabisa mwanamuziki huyo katika ulimwengu wa muziki.

Ili kumridhisha mfalme, Aibumwiko alitayarisha mikutano ya mara kwa mara kati ya wanamuziki na mfalme. Alichagua wanamuziki maalumu katika mikutano hii, akawaacha mbali wale ambao wangeweza kumshitua mfalme kuwa Aibumwiko si mzuri kama wengi walivyodhani.

Wakati sifa za Aibumwiko zikipaa kuwa ndiye mkombozi wa muziki, muziki ukawa unashuka thamani, kumbi zilizokuwa zikijaa watu Jumatano mpaka Jumapili zikaanza kukosa watu, wanamuziki waliojaribu kubaki wakijitahidi kuendeleza gurudumu maisha yao yakawa mabaya zaidi kuliko kabla ya himaya ya Aibumwiko.

Kwa kuwa Aibumwiko alipenda sana aina moja tu ya muziki na huo ndio wananchi wa Mwongopee wakawa wanalazimisha kusikiliza mchana na usiku. Na hata ukaanza kutambulishwa kama ndio muziki wa Taifa wa Mwongopee.

Kila chenye mwanzo kina mwisho, mfalme wa Mwongopee akakutwa amefariki dunia ghafla asubuhi moja, mwanawe akaapishwa kuwa mfalme mpya.

Mfalme mpya alikulia mikononi mwa baba aliyependa muziki, hivyo naye alikuwa mpenzi mkubwa wa muziki ila yeye alikuwa anashangaa kwa nini wanamuziki wa nchi yake ndio wenye hali duni wakati wa nchi jirani na yake - nchi ambayo ilikuwa chini yake kiuchumi wanamuziki wake walikuwa na hali nzuri.

Akaamua kuita mkutano wa wanamuziki bila kumtumia Aibumwiko, jambo ambalo Aibumwiko na wapambe walijitahidi kila njia kulipinga. Wanamuziki waliongea mengi siku hiyo wengine wakitokwa na machozi kuhusu waliyotendewa na Aibumwiko, lakini walimueleza mfalme hasara ambayo kwa miaka mingi Serikali imepata.

Walimweleza mfalme kuwa mfumo uliokuwepo ulikuwa ni wa kukwepa kulipa kodi na ushauri aliokuwa akipewa baba yake ulikuwa ni wa kuifanya tasnia ionekane ni ya burudani tu haina mchango wowote katika uchumi wa Taifa zaidi ya kukusanya watu kwenye mikutano.

Taifa lile lilikuwa limepoteza mabilioni ya pesa kwa kumwamini Aibumwiko. Mfalme aliinama kisha alipoinuka machozi yalikuwa yakimlengalenga akasema neno moja tu, “kuanzia sasa hayo yamekwisha”. Na hadithi ya leo imeishia hapa.



Chanzo: mwananchi.co.tz