Msanii maarufu wa Bongo Fleva, Mbwana Yusuf Kilungi maarufu kama Mbosso amefunguka kuhusu tatizo la ugonjwa wa moyo ambalo limemwandama tangu akiwa mtoto.
Akizungumza katika mahojiano maalum Mbosso ambaye ni msanii wa lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) amesema kwamba ugonjwa huo unasababishwa na mafuta kuwa mengi kwenye mishipa ya damu ya kwenda kwenye moyo.
Dalili alilozitaja za ugonjwa huo ni pamoja na maumivu upande wa kushoto wa kifua, viungo kupoteza hisia na kwake anatetemeka vidole.
Kwa kitaalam ugonjwa wa mtu kuwa na mafuta mengi kwenye damu huitwa Familial hypercholesterolemia. Ni ugonjwa wa kurithi.
Ugonjwa huu unamweka mgonjwa katika hatari ya mishipa ya damu kuziba katika umri mdogo na hivyo kusababisha moyo kukosa Oxygen.
Matibabu ya ugonjwa huu ni kutumia dawa za kupunguza mafuta. Alipohojiwa na mwandishi wetu kuhusu tatizo hilo Mbosso amesema tangu atambue kuwa ana ugonjwa huo wa moyo amekuwa akimtembelea daktari wake mara kwa mara na kuyafuata maagizo yake katika juhudi za kutaka kupona.
Sehemu ya mahojiano ilikuwa kama ifuatavyo: Mwandishi: Nini hasa unachotakiwa kufanya baada ya kugundulika tatizo lako? Mbosso: Najitahidi sana kufanya mazoezi kama nilivyoshauriwa na daktari wangu na huwa tunakutana sana mara kwa mara.
Mwandishi: Kuna masharti umepewa na huyo daktari wako? Mbosso: Mdio; kuna baadhi ya vyakula ambavyo nimeambiwa nisivile japokuwa uchu unanitesa sana. Pia natakiwa kufanya mazoezi.
Mwandishi: Ni vyakula gani hivyo ambayo umekatazwa na daktari wako?
Mbosso: Daktari wangu ameniagiza kutokula nyama zozote nyekundu, ameniiambia nile nyama nyeupe pekee. Natakiwa nile samaki, kuku na mboga za majani.
Mwandishi: Je unatimiza masharti hayo?
Mbosso: Nikiri tu kwamba napenda nyama hivyo huwa nashindwa kuyafuata maagizo ya daktari wangu kikamilifu, huwa nikiona mshikaki naweza kula mmoja. Nyama kuachana nayo kabisa huwa mtiti sana.
Mwandishi: Kwani ugonjwa huu umeanza kuugua lini?
Mbosso: Nimekuwa nikiishi na tatizo hili la moyo na la kutetemeka mikono yangu tangu nizaliwe.
Mwandishi: Wewe ulipogundua kuwa una tatizo hilo umefanya hilo?
Mbosso: Niliamua kufuatilia matatizo yangu na kutafuta matibabu; baada ya kuwa mtu mzima nikaambiwa kuwa tatizo la mtiririko wa damu mwilini mwangu lilisababishwa na kuzibwa kwa mishipa ya damu ya kwenda kwenye moyo.
Mwandishi: Uliambiwa na madaktari? Mbosso: Ndio; waliniambia kwamba nina tatizo la mafuta kwenye mishipa yangu ya damu kwenda kwenye moyo; imezibwa na mafuta. Kwa hiyo damu haizunguki vizuri kwenye mwili.
Mwandishi: Hilo tatizo linakusababshia nini au unajisikiaje?
Mbosso: Nikilala usiku napata maumivu makali kwenye upande wangu wa kushoto hadi nalia wakati mwingine. Mwandishi: Ina maana tatizo hilo la moyo limesababisha matatizo mengine mwilini mwako kama hilo la kutetemeka mikono?
Mbosso: Ndio tatizo hilo la moyo ndilo linalosababisha mikono yangu kutetemeka; wakati najiunga kwa Mkubwa Fella; watu wengine walidhani natumia madawa.
Mwandishi: Baada ya kukutana na madaktari na kukupa tiba sasa unaendeleaje?
Mbosso: Maendeleo yangu sio mabaya. Naendelea vizuri, sasa najitahidi kuzingatia ninayoambiwa. Jambo baya ni kwamba daktari aliniambia shida yangu huenda ikawa kubwa zaidi baada ya kufikisha miaka 30 na huenda ikanisababishia nisipate tena watoto nisipopata matibabu.
Mwandishi: Hili tatizo umewahi kulisema kwa wafuasi wako na mabosi wako?
Mbosso: Wengi wanajua; niliamua kuwafichulia mashabiki wangu kuhusu tatizo langu la moyo ili wasije wakasikia Mbosso kaanguka ghafla washangae na kujiuliza vipi.
Mwandishi: Katika familia yenu kuna mtu mwingine ana tatizo kama hilo? Mbosso: Ndio shangazi yangu alipata tatizo hilo kwenye shingo. Niliamini ni ishu za kifamilia kwa sababu hata mama na mdogo wangu wana tatizo hili.
Mwandishi: Tatizo hili halikupi shida unapokuwa kazini yaani ukiwa kwenye shoo? Mbosso: Huwa linanipa shida kwani naweza kuhisi hali mbaya jukwaani, ikitokea hivyo mimi huinama na kujifanya kama nazuga kumbe naumwa na hali ikitengemaa, nainuka na kuendelea na shoo.
Mwandishi: Unawashauri nini watu wanaokusoma katika ukurasa huu? Mbosso: Nawashauri wawe wepesi kwenda kupima afya zao. Mimi nilikuwa naogopa kupima lakini sasa nimejua tatizo baada ya kufanya vipimo. Pia watu wabadili mtindo wa maisha, kwa mfano mimi sinywi soda na badala yake nakunywa maji tu au juisi halisi za matunda.
Mwandishi: Pole na asante.
Mbosso: Asante sana.
Matibabu ya Magonjwa ya MoyoKwa mujbu wa Dk. Godfrey Chale kusimamia ugonjwa wa moyo na dawa na mabadiliko ya mtindo wa maisha ni ya kuhitajika lakini haiwezekani kila wakati, hasa ikiwa vizuizi ni vingi.
“Uingiliaji wa upasuaji unabaki kuwa chaguo pekee la matibabu katika hali nyingi, hata hivyo kuna njia mbili za kutibu magonjwa ya moyo:
“Angioplasty ni kuingiza stents kwenye mishipa kwa msaada wa catheter ili kushikilia mishipa iliyoziba kufunguliwa.
“Pili kitaalamu huitwa CABG; hii ni kupandikizwa kwa mishipa ya damu kuunda njia mbadala ya mtiririko wa damu kwenda moyoni. Na Angioplasty ni chaguo la matibabu lisilo vamizi na linahitaji kukaa kwa muda mfupi hospitalini.
“Hata hivyo, angioplasty haipendekezwi ikiwa vizuizi vimeenea kwenye ateri au ikiwa mishipa ya damu karibu na moyo ina miundo isiyo ya kawaida au iliyobadilishwa.”