Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Gabo ataka ‘washindi wa Iringa’ wasiachwe

46524 Pic+gabo

Wed, 13 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwigizaji bora wa mwaka jana, Gabo Zigamba amesema watoto wa Iringa waliochukua tuzo kubwa mwaka huu, Florah Kihombo na Rashid Msigala wasiachwe ili kukuza vipaji vyao.

Watoto hao waliochukua tuzo za mwigizaji bora wa kike na wa kiume za SZIFF, walizua gumzo hasa baada ya mastaa akiwamo Gabo waliokuwa wakishindanishwa nao kubwagwa.

Alisema anabariki ushindi wao kwa kuwa kila mmoja anaweza kushinda isipokuwa kazi ngumu ni kutetea ushindi.

“Naamini kila mtu anaweza kushinda, lakini inapokuja watu wakahoji ushindi hapo ndipo unapoweza kukutana na ugumu katika kuutetea. Mimi sina kipingamizi na ushindi wao,” alisema.

Aliongeza kuwa furaha yake itakuwa ni kuwaona watoto hao wanaonekana kwenye filamu nyingine na vipaji vyao vinakuzwa zaidi.

Alitolea mfano vipaji vilivyoanza kukuzwa na marehemu Steven Kanumba vilivyoachwa na kutoweka kabisa katika ulingo wa filamu nchini.

“Kanumba alifanya sinema mbili tatu na watoto, alijaribu kuwanyanyua lakini ni kama wameachwa hivi na sidhani kama wanajisikia vizuri. Kitu kizuri kikiwekwa vizuri kinakuwa bora zaidi,” alisema.

Mwandishi alipomuuliza iwapo anaweza kuwashirikisha katika filamu zake siku za usoni, alisema hawezi kuahidi kwa kuwa kazi hiyo hutegemea muswada unahitaji nini.

“Unajua hakuna urafiki sana na soko, kuna mipango ambayo nimeshajiwekea hivyo siwezi kuahidi hilo kwa sasa, lakini katika ile mipya ninaweza kuwaingiza,” alisema.



Chanzo: mwananchi.co.tz