Iringa. Takribani wiki tatu zilizopita, tasnia ya filamu nchini iliwapata mastaa wapya baada ya watoto wawili kutoka mkoani Iringa kutwaa tuzo mbili kubwa nchini.
Hao ni Rashid Msigala (10) na Flora Kihombo (11) watoto ambao wanalelewa na kituo cha Tag Lwang’a Student Center kilichopo Isimani mkoani iringa.
Watoto hao wanalelewa kituoni hapo tangu mwaka 2014. Ni miongoni mwa watoto 244 wa kituo hicho kinacholea na kuwahudumia kutokana na mazingira magumu wanayoishi.
Watoto hao kwa mara ya kwanza walitambulika kuwa na kipaji cha kuigiza wakati wa sherehe za Mtoto wa Afrika walipoigiza kuhusu baba mlevi ambaye hahudumii familia na kumnyanyasa mkewe.
Katika sherehe hizo igizo hilo liliwafurahisha wageni waliofika na kuwataka viongozi wanaohusika na watoto hao kulitengenezea filamu ushauri huo ulizaa filamu ya Kesho.
Baada ya kupewa wazo hilo walijipanga kuandaa filamu hiyo na kurekodi kwa nia ya kuuza katika mikoa mbalimbali na walifanikiwa kufanya hivyo mwaka jana.
Baba mzazi wa Rashid anasema hakuwahi kugundua kipaji cha mtoto wake kwa kipindi chote alichokaa naye, lakini baada ya kupewa mafunzo na kituo cha TAG aliona ana kipaji cha kuigiza. “Kiukweli hakuna mzazi ambaye hapendi maendeleo ya mwanae, mimi napenda kuona mwanangu anaendelea kufanya vitu vingi vizuri vya kutikisa jamii zaidi ya hivyo,” anasema.
Anaongeza kuwa anatamani kuona mwanae akisoma vizuri, kupata elimu na kutimiza ndoto zake huku akitumikia kipaji chake ili awakomboe wazazi wake.
“Mpaka sasa kupitia filamu hiyo tunajua Mungu katuonyesha njia anayotaka kupita tungebaki naye tusingejua ana kipaji maisha yetu ndio kama unavyoyaona hatuna uwezo wa kumuendeleza kwa chochote,” anasema.
Mama mzazi wa Flora, anasema tangu akiwa mdogo mwanae alipenda kuwachekesha wenziwe kwa kuwaigizia jambo ambalo hawakujua kama ni kipaji mpaka kituo cha huduma ya mtoto kilipompa mafunzo ya uigizaji.
Naye baba mzazi wa mwigizaji huyo bora wa mwaka, Pasiansi Kihombo anasema baada ya kusikia ushindi wa mtoto alijisikia furaha.
“Nawashukuru wadau wote walioonesha ushirikiano katika ufanikishaji wa tuzo hizo tangu mchakato wa kuwafundisha hadi upokeaji wa tuzo pia pongezi kwa wote waliowapigia kura na hatimaye kushinda,” anasema.
Ushindi wa SZIFF
Mratibu wa kituo kinachowalea, Raphael Emmanuel anasema mwaka jana baada ya kuona tangazo la kupeleka filamu kwa ajili ya tuzo za SZIFF, alipanga kuhakikisha wanafika mkoani Mbeya kuwasilisha DVD yenye filamu ya Kesho na kuikabidhi.
Baada ya kuanza kuonyeshwa kwa sinema zilizokusanywa tuliona ratiba ya filamu yetu ya Kesho kuwa itaonyeshwa, hivyo tuliwataarifu wanakijiji na jamii nzima kwa ujumla ili waweze kuiona na kuipigia kura.
“Filamu yetu ilibahatika kuonyeshwa zaidi ya mara sita hivyo ambaye anasema hakuiona hakuwa ‘serious’ (makini) kuifuatilia kwani wasanii wengi huangalia filamu zao zinapoonyeshwa na kusahau kuangalia filamu wanazoshindana nazo.”
Anasema baada ya kuonyeshwa wana kijiji cha Isimani walijitahidi kupiga kura kuhakikisha inashinda kutokana na uzuri wa maudhui ya filamu hiyo yanayoumiza na kuelimisha jamii juu ya unyanyasaji wa watoto na wanawake katika jamii.
Anaeleza kuwa baada ya kupigiwa kura filamu hiyo ilibahatika kuingia hatua ya 10 bora na kuanza kushindanishwa na nyingine ambapo waliingia woga na kulazimika kufanya maombi ili kuongeza imani ya ushindi.
Hatimaye Rashid na Flora walifanikiwa kuchukua tuzo ya msanii bora wa kike na msanii bora wa kiume kwa kuwashinda mastaa kama Wema Sepetu, Gabo Zigamba na Hemed Suleiman.
“Kwanza hatukuamini kwamba tungeshinda kwa kuwa filamu tulizoshindanishwa nazo nyingi wamecheza mastaa na ukizingatia yetu tulicheza watoto watupu.
Anasema filamu ya Kesho inatoa funzo dhidi ya unyanyasaji wa watoto na kuwatelekeza wanawake na wengine kupoteza maisha na kuwaacha watoto yatima.
“Tunaomba Serikali iangalie vipaji kwa watoto wanaoishi katika vituo vya kulelea wenye mazingira magumu ili kukuza na kuwaendeleza,” anasema.
Kwa upande wake mchungaji kiongoziwa Kanisa la TAG Lwang’a, Mchungaji Ebehati Kafyulilo anasema waliamua kuandaa filamu hiyo ili kuandaa kesho ya mtoto.
Anasema viongozi waliopo wanapita, hivyo ni lazima kuwaandaa watoto kuwa viongozi wa kesho kwa kuwajengea uwezo wa kujiamini kujitambua na kujitegemea.
Mchungaji Ebehati anasema furaha aliyonayo juu ya watoto hao kupata tuzo ni kubwa na kuahidi kuendelea kuwalea katika misingi ya dini.
“Sisi kama kanisa tunajivunia kuwalea watoto wenye vipaji kama hivi, ni jambo la kumshukuru Mungu kupata tuzo hizo hivyo tutajitahidi kulinda maadili yao na kuwaepusha na mitandao ya kijamii ili watimize ndoto zao wakiwa na hofu ya Mungu”.
Alieleza kuwa kikundi chao kimesajiliwa na endapo msanii atataka kuja kumchukua mtoto yeyote haitakubalika kwani katiba ya kikundi inasema haondoki kituoni mpaka atimize umri wa miaka 22.
Kwa upande wake, Isaya Mkiwa mwanajamii katika kituo cha huduma ya mtoto anasema jamii imewapokea vizuri watoto hao baada ya kushinda tuzo hususani wanakijiji wa Isimani.
Anasema wamejipanga kusimamia maadili ya watoto hao ambao tayari wameonyesha mwanga wa kuwa mastaa kwa sababu katika kituo hicho wanahusika na mambo ya kiroho.
“Tutaendelea kuwa washauri na sio kwa kuonekana kwao kuwa mastaa ndio wasiwe na maadili. Wanatakiwa kuendana na maadili ya kituo na kanisa ili waweze kufika wanapotaka, hivyo hatutapenda wajikite sana katika mitandao ya kijamii badala ya kusoma. Kanisa na kituo kwa ujumla tunafanya kazi ya kumlinda mtoto katika nyanja mbalimbali,” anasema.