Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Filamu ya Vuta N'kuvute kuiwakilisha Tanzania tuzo za Oscar

Vuta N'kuvute Filamu ya Vuta N'kuvute kuiwakilisha Tanzania tuzo za Oscar

Wed, 21 Sep 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Filamu ya Vuta N'kuvute imechaguliwa kushindanishwa katika tuzo za filamu za Oscar 2022 zitakazotolewa nchini Marekani Februari mwakani.

Vuta N'Kuvute ni filamu iliyotoka mwaka jana imeandaliwa na kampuni ya Kijiweni Production huku mwongozaji wake akiwa ni Amir Shivji.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Septemba 20,2022 Mwenyekiti wa kamati ya kuchagua filamu itakayoshiriki tuzo za Oscar, Dk Mona Mwakalinga,amesema Vita N'Kuvute imeibuka kidedea kati ya filamu nne zilizowasilishwa kwao kwa ajili ya kwenda kushindanishwa katika tuzo hizo .

Amesema kamati hiyo ilifungua dirisha ya kupokea filamu hizo kuanzia Agosti 1 hadi Agosti 30,2022.

"Kwa kipindi hicho cha mwezi mmoja kamati ilipokea filamu nne ambazo ni 'I Regret', 'Mungu ndio suluhisho' na 'Giza' zote zikiwa zimetayarishwa na Amor Abbass na filamu ya nne ilikuwa ni Vuta N'Kuvute,"amesema Dk Mona.

Hata hivyo Mwenyekiti huyo amesema katika upokeaji wa filamu hizo baadhi zilikuwa zimesambazwa mitandaoni, hazikuwa zimeonywesha kwenye kumbi za sinema kama ilivyotakiwa na uwasilishaji wa baadhi ya filamu haukuzingatia vigezo vilivyowekwa na waandaji wa tuzo za Oscar.

Kuhusu mchakato unaoenda kufanyika baada ya filamu hiyo kupitishwa, Mona amesema itaingizwa kwenye kapu moja la filamu zinazotoka nje ya nchi ya Marekani ambapo zitachujwa na kamati ya Oscar Academy na kubaki 15 na baada ya hapo zitachujwa tena na kubaki tano ambazo hizo ndizo zitatajwa kama filamu zinazoshindanishwa kwenye kipengele cha filamu za kigeni katika tuzo hizo.

Akizungumzia hatua hiyo,Katibu Mtendaji wa bodi ya filamu,Dk Kiagho Kilonzo,ameipongeza kamati kwa kazi nzuri iliyofanya kwa kutokuwa na upendeleo na kuzingatia weledi na vigezo vilivyowekwa na wandaaji.

Wakati kuhusu filamu iliyoteuliwa amesema ana uhakika itailetea Tanzania ushindi kutokana na historia yake ikiwemo kuwahi kushinda tuzo tisa za kimataifa na kushiriki kwenye matamasha ya kimataifa yasiyopungua 19 tangu ilipotoka mwaka 2021.

"Kikubwa niwaombe watanzania tuendelee kuomba tuzo hii kufika kwenye hatua ya juu ya kushondanishwa na hata kushinda kwa kuwa itakuwa sio tu imeiletea tasnia ya filamu sifa bali hata nchi ya Tanzania,"amesema Dk Kilonzo.

Kwa upande wake mwakilishi kutoka Kijiweni Rehema Yusuph,alisema hiyo ni hatua kubwa kwa tasnia ya filamu kwa ujumla kutokana na tuzo za Oscar kuwa tuzo namba moja kwa ukubwa duniani.

"Ushiriki wetu katika tuzo hizi unatupa moyo kwamba kazi tunayoifanya Tanzania inaonekana duniani,kikubwa mwakani watu wajitokeze wengi kushiriki ili tulete ushindani,'amesema Rehema.

Kwa upande wake Katibu wa Shirikisho la Filamu Tanzania, Twiza Mbarouk amesema hii inawapa hamasa wasanii na waandaaji kwa ujumla wa kazi za filamu kwenda kutengeneza kazi zilizo bora wakijua kuna nafasi ya kushiriki katika tuzo hizo kubwa.

Chanzo: Mwanaspoti