Miaka 20 iliyopita Fid Q alikuwa akipambana kutoka kimuziki, safari ilikuwa ni ngumu ila kuna siku akapata nguvu na matumaini makubwa kuwa kuna nyakati zitakuja naye atakuwa msanii mkubwa wa Hip Hop Bongo kama ilivyo sasa.
Ni baada ya kusikiliza albamu ya kwanza ya Professor Jay, Machozi Jasho na Damu (2001), kupitia wimbo ‘Yataka Moyo’, Jay aliwasihi wasanii ambao aliamini wana uwezo ila bado hawajapata wanachostahili kutokata tamaa maana sanaa ya Bongo yataka moyo.
Fid Q ni miongoni mwa waliotajwa katika wimbo huo, kitendo hicho kilimpa nguvu kwa sababu Professor Jay alikuwa ni msanii mkubwa, tayari alishavuma na kundi la Hard Blasters Crew (HBC) kupitia albamu yao, Funga Kazi (2000).
Mungu akajalia Fid Q akutana na Hardmad ambaye ndiye mtu wa kwanza kumpeleka MJ Records kwa Master Jay aliporekodi wimbo wake ‘Huyu na Yule’ akimshirikisha Mr. Paul, wimbo huo ulimtambulisha vizuri ndani ya Bongofleva.
Baadaye akarekodi ‘Fid Q Dot Com’ ndani ya Baucha Records ukiwa ndio wimbo wa kwanza kurekodi katika studio hiyo, vilevile huu ni wimbo wa kwanza kwa rapa huyo kuufanyia video.
Nyimbo hizo mbili zikaliweka jina la Fid Q katika ramani na hadi sasa ni miongoni mwa wasanii wenye heshima kubwa upande wa Hip Hop Bongo, huku akiwa ametoa albamu tatu, Vina Mwanzo Kati na Mwisho (2005), Propaganda (2009) na KitaaOLOJIA (2019).
Katika ngoma yake, Bongo Hip Hop (2014) akimshirikisha P-Funk Majani, Fid Q ameeleza changamoto nyingi zinazoukumba muziki huo na wasanii wake ila bado yeye atasimama na Hip Hop maana kwake ni mfano wa mwanamke mzuri tena malkia.
“Bongofleva mzuri kiasi, Hip Hop wewe ndio my queen. My first my last, everything in between.... Kama kukupenda ni dhambi, basi shetani yu nami, na kamwe sitonyea kambi ili niwabambe dukani,” anachana Fid Q.
Hivyo kitendo cha kuifananisha Hip Hop ya Bongo na mwanamke mzuri anayepitia changamoto ila bado akaamua kuwa naye, ni wazi Fid Q anaendelea kukubaliana na Professor Jay aliposema sanaa yataka moyo.
Tunaweza kupata picha kubwa ya jambo hili kupitia wimbo wake mwingine, Ripoti za Mtaani (2009) akimshirikisha Zahiri Zorro, ndani yake amemzungumzia binti ambaye maisha yake yaliishia vibaya baada ya kuendekeza tamaa nje ya ndoa yake.
“Alipenda kwenda na tarehe akasahau siku huwa hazilingani, pesa huja na sterehe na matatizo humo humo ndani. Hakuna kinachokauka mapema zaidi ya machozi, japo macho hubaki mekundu na usoni ishara ya majonzi,” anachana Fid Q.
Ndivyo yalivyo maisha ya wasanii wengi Bongo, muziki huwapatia umaarufu na fedha na baadaye starehe zinachukua nafasi yake na hata kusahau kazi yao, wasiokuwa makini hujikuta katika matatizo ambayo hubadilisha kabisa taswira ya maisha yao.
Mathalani wiki iliyopita nimeona mahoajino ya Chid Benz na Clouds TV, kwa kweli, “inasikitisha, inahuzunisha... lazima niseme”, kama alivyoimba Zahiri Zorro katika wimbo huo wa Fid Q, Ripoti za Mtaani.
Tangu Chid Benz alipotumbukia katika urahibu wa dawa za kulevya maisha yake hayajawahi kuwa sawa, hata ukimtazama alivyokuwa anaongea na ukamtazama yule Chid aliyekuwa akipanda jukaani kuchukua tuzo za TMA, utabaini kuna kitu hakipo sawa.
Hata hivyo, kuna wasanii wengi wanapitia changamoto mbalimbali ambazo sio sawa na za Chid licha ya muziki wao kuwa mkubwa, wanalazimika kuficha ili kulinda chapa zao na kuteswa na ile hali ya umaarufu lakini kumbe polopole ndivyo wanajimaliza.
“Anaamini yeye ni mwema na wabaya Mungu hawahitaji, samaki ana mengi ya kusema ila mdomoni ana maji.... Siku zikapita kimaisha akaanza kufeli, kwa kuwa uwongo aliuzidisha amejikuta yupo nje ya ukweli,” Fid Q katika Ripoti za Mtaani.
Ndicho kilichomkuta na Vanessa Mdee hadi Juni 2020 alipoamua kutangaza kuachana na Bongofleva kutokana na kumfanya kuishi maisha ya uongo kitu kilichopelekea kuwa na msongo wa mawazo na kujikuta ametumbukia katika ulevi wa kupita kiasi.
Chid Benz amekuwa mkweli katikati ya matatizo yake, kwa mfano alisema hata sehemu anayoishi sasa ni changamoto, hajachagua maisha hayo ila ameyakuta kama alivyoukuta muziki. Hata hivyo, bado ana matumaini ya mbele na kuwataka mashabiki kufuatilia kazi zake mpya.
Lakini huyu ni msanii aliyeshirikishwa sana tena wasanii karibia wote wakubwa Bongo, amefanya kazi na wadau na ameshiriki matamasha mengi makubwa nchini n.k, leo hii inakosaje hata sehemu nzuri ya kuishi ukiachilia mbali uangalizi wa afya yake?
“Aliowavisha kofia wote hawakuwa na vichwa, alichopoteza hakihesabu anasehabu alichobakiza,” alimaliza Fid Q katika wimbo wake, ‘Ripoti za Mtaani’ kutoka kwenye albamu yake ya pili, Propaganda (2009).
Ikumbukwe katika muziki Chid Benz ameshirikishwa na wasanii wenzake kama Alikiba, Diamond Platnumz, Ray C, Mwasiti, Marlaw, TID, Makamua, Tundaman, K-Lynn, Spack, Lady Jaydee, Professor Jay, JCB, Mwana FA, Nako 2 Nako Soldiers, Nikki Mbishi, Young Dee, Stereo, Mh. Temba, One The Incredible, Country Boy n.k.