Lifestyle

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

SIL

Fanya hivi ili Januari usiwe mwezi dume kwako

Lovers Stress Bn.jpeg Fanya hivi ili Januari usiwe mwezi dume kwako

Wed, 4 Jan 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Licha ya wengi kuamini Januari ni mwezi mgumu kiuchumi, wachumi na wanasaikolojia wametaja mambo matano yanayoweza kukuvusha salama.

Mambo hayo ni kuondoa woga, kubadili fikra, kujiwekea akiba na kuwa na mipango. Ukiwa makini kwenye maeneo hayo yote, wanasema Januari utakuwa mwezi wa kawaida.

Januari ni mwezi ambao hata kukopeshana huwa ngumu kwa sababu kila mtu anakuwa na majukumu ya kifamilia anayotakiwa kuyatimiza pamoja na matumizi makubwa waliyoyafanya kwenye sikukuu za mwisho wa mwaka.

Mwanasaikolojia Modesta Kimonga ambaye ni mkufunzi wa Chuo cha Ualimu Patandi anasema jamii imejijengea woga kuwa Januari ni ngumu na wengi wao wameshaathirika na uongo huo.

“Kwenye fikra zao wanaamini hivyo jambo ambalo si kweli na wanapaswa kuiondoa hofu hiyo akilini ili mambo yaende. Makwazo yoyote huanzia kwenye fikra ambayo ikishaharibika mambo hayaendi.

"Kwanza inapaswa kuondoa woga kuhusu Januari kisha mtu afanye maandalizi kidogokidogo, si ya kiakili tu hadi ya kimwili kwa kuwa ndiyo yanaifanya Januari ionekane ngumu kwa wengi wetu,” alisema Modesta.

Watu, alisema wanatakiwa kufahamu kwamba Januari haiji kwa bahati mbaya kwani ni mwezi upo na unajulikana hivyo mtu asiyumbishe majukumu yake yanayompasa bali aweke akiba na kuwa na mipango ya muda mrefu hasa itakayomvusha mwezi huo bila tatizo lolote.

Mchumi na Mkurugenzi wa Shahada za Juu za Chuo cha Biashara (CBE), Dk Dickson Pastory kwa upande wake, anasema kwa wale ambao wanajipanga na kuweka akiba, Januari huwa haiwaathiri sana kiuchumi kwa kuwa wanayo mipango na bajeti ya matumizi.

“Kuna wale wanaoishi tu hawana bajeti, basi kipindi hiki wawe makini. Wanakiwa kutumia pesa zao vizuri na wakiweza iwe kwa matumizi ya lazima tu tena wayafanye mapema kama vile kulipa ada.

"Kipindi cha mwisho wa mwaka wengi wetu wanapokuwa na pesa hawatumii vizuri, sasa kwa wale ambao hawana bajeti na plan (mipango) ikifika Januari watakuwa na mahitaji makubwa kuliko kiasi walichonacho,” alisema.

Ili wasiyumbe sana kiuchumi, Dk Pastory alishauri waangalie vipaumbele kwa kuzingatia hali ya uchumi nchini kwa ujumla si nzuri sana hivyo watumie fedha walizonazo kwenye matumizi ya lazima kwanza kwani Januari ni mwezi mrefu kwa mtu ambaye hakuwa na mipango.

Ushauri kwa Watanzania

“Kama mtu ana kipato ambacho hakieleweki, yaani leo anapata ila kesho hana uhakika basi ajipange ili asivuruge maisha ya kila siku na kukosa hata nauli ya kwenda kazini au kwenye shughuli zake za kujitafutia kipato mwezi huu,” alishauri Dk Pastory.

Watu hao, alisema waangalie mahitaji muhimu kwanza na kuyatekeleza katika kipindi hiki cha mwanzo wa mwaka ili wasije kuyumba katikati ya Januari ambako wengi wanaumia ila kitu cha msingi alisisitiza ni kuwa na utaratibu wa kuweka akiba na kuwa na mipango isiyoyumbishwa na changamoto zinazojitokeza kila siku.

Kwa maoni na ushauri wa mchumi huyo mwandamizi, kwa kufanya hivi, kutawaondoa wengi kwenye dhana ya kuamini Januari ni mwezi mgumu na mrefu.

Mchumi mwingine, Profesa Haji Semboja wa Chuo Kikuu Zanzibar (Suza) alisema Januari kuna saikolojia na utamaduni wa jamii kubwa kuamini ni mwezi mgumu jambo ambalo si kweli.

“Mwisho wa mwaka kuna matumizi mengi na kwa kawaida mtu anakuwa amepata mshahara ambao huupokea kila mwezi lakini wakati wa mwisho wa mwaka wengi wanakuwa na matumizi makubwa tofauti na kila siku. Kwenye sherehe za mwisho wa mwaka wapo watu wanazifanyia mipango na bajeti na wengine wanastukia tu zimefika lakini aliyejitayarisha na ambaye hakujitayarisha wote watasherehekea,” alisema Profesa Semboja.

Profesa huyo alisema kuwa kuna matumizi makubwa yanafanyika kipindi hicho na wengi kufika Januari wakiwa hawana pesa jambo ambalo linaweza kuepukika siku zijazo kwa kujipanga mapema.

“Ili tusifike huko ni kujitayarisha kwa maisha na kujipanga vizuri kwa kuwa na mpango na kuweka akiba kwa mwaka mzima ili haya matumizi ya pili kama ya ada, kodi na mengineyo yakifika isiwe kama yamekufumania.

Hii itarahisisha na kuiona Januari kuwa mwezi wa kawaida kama mingine na hizi sherehe za mwisho wa mwaka zinatakiwa kusheherehekewa kulingana na ukubwa wa mfuko wako, kama hauko vizuri sio lazima ufanye,” alisitiza Profesa Semboja.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live