Lifestyle

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

SIL

Familia ya wasioona inavyopambana kuepuka ombaomba

6c54bbf187ffa99209d7fabe0dc8e2d4.png Familia ya wasioona inavyopambana kuepuka ombaomba

Tue, 1 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WATU wenye ulemavu ni kundi ambalo huko nyuma lilionekana tegemezi, lisiloweza kujitafutia. Lakini imekuwa ikithibitika kwamba walemavu wakiwezeshwa wanaweza kujitegemea na mifano iko lukuki.

Mfano ni wanawake wenye ulemavu wa kuona katika halmashauri ya Mji wa Kibaha ambao wanafanya biashara na kujiongezea kipato. Moja ya wajasiriamali wasioona, Laila Nasoro (34), mkazi wa Simbani, kata ya Kibaha wilaya ya Kibaha, Pwani amekuwa akijishughulisha na usukaji wa mikeka, uchomaji wa mkaa na ulimaji wa vibarua kwenye mashamba ya watu ili kuendesha familia yake ya watoto watano.

Laila ambaye anashirikiana kazi na mdogo wake, Aziza Nasoro (30) anasema anatumia zaidi ya siku 10 kusuka mkeka mmoja. Mlemavu huyo wa macho ambaye watoto wake wawili ni miongoni mwa watano pia hawaoni, anasema mikeka anayoisuka anaiuza kwenye minada.

“Mkeka mmoja nauza kati ya Sh 15,000 na 20,000 na mkaa nauza kati ya Sh 15,000 hadi 18,000 lakini mtu akiufuata sehemu tunayochomea tunauza gunia dogo kwa shilingi 10,000.

“Tunaishi kwenye mazingira magumu kwani mume wangu ambaye si mlemavu huwa tunashirikiana katika shughuli hizo. Kuhusu mikeka kwa mwezi mmoja nina uwezo wa kusuka mikeka mitatu lakini tatizo ni soko la uhakika kwani huwa ninalazimika kuitembeza au kuuza kwenye minada,” anasema Laila.

Anasema kutokana na ugumu wa maisha inawabidi kulima vibarua kwenye mashamba ya watu akishirikiana na watoto wake ambapo walipewa eneo kwa ajili ya kulima kwenye bonde la msitu wa hifadhi wa Kongowe.

“Tunalima mpunga lakini mpunga wenyewe huwa tunauvuna baada ya wiki mbili na nusu unakuwa haujakomaa tunautwanga na kuuanika juani kwa siku moja na kuupika. Mara nyingi tunalazimika kuuvuna mapema kabla ya muda kutokana na njaa,” alisema Laila.

Anasema kuwa mwaka juzi alivuna magunia matano ya mpunga lakini mwaka jana kutokana na uhaba wa mvua hakuweza kupata chochote hivyo kulazimika kuelekeza nguvu kubwa kwenye kufanya vibarua na usukaji wa mikeka.

Kuhusu uchomaji mkaa anasema anaandaa sehemu ya kuchoma mkaa na kutengeneza dude la kuchomea mkaa lakini mara unapokuwa umeshakamilika humbidi kutafuta mtu wa kumtolea na kuuweka kwenye viroba na kuishonea na hivyo kulazimika kumlipa.

Anasema kwa sasa wanachoma mkaa kwa kificho kwani hawaruhusiwi kukata miti wala kuchoma mkaa na wanapobainika hunyanyang’anywa mkaa wao.

“Changamoto kubwa iliyopo ni ukosefu wa mtaji. Kama ningepata mtaji ningefanyabiashara yoyote ambayo nitakuwa nakaa tu kuliko hii ya uchomaji mkaa ambapo serikali inakataa ukataji wa miti ingawa mkaa ndio nishati ambayo bado wengi wanaitegemea kwa ajili ya kupikia na ndiyo unatusaidia kwa kiasi kikubwa katika maisha yetu ya kila siku,” anasema Laila.

Anasema katika kuhakikisha anakabili changamoto za maisha alijiunga na kikundi cha wajasiriamali cha watu wasioona cha Dira Mpya na kupata mkopo wa halmashauri kiasi cha shilingi milioni mbili ambazo waligawana kiasi cha shilingi 250,000 kila mmoja.

Anasema wanarejesha kiasi cha shilingi 28,000 kwa mwezi. Hata hivyo anasema kiasi hicho cha Sh 250,000 ni kidogo kuweza kuanzisha mradi mkubwa.

Kwa upande wake, Aziza, mdogo wa Laila anasema kuwa yeye anafanya biashara ya kuuza korosho, mkaa na mahindi ya kuchemsha ambapo hutembeza maeneo mbalimbali akisindikizwa na mwanawe ambaye yeye siyo mlemavu.

Aziza anasema naye ni mmoja wa wanufaika wa mkopo huo kutoka Halmashauri ya Mji ambaye naye anarejesha kiasi cha shilingi 28,000 kwa kila mwezi.

Akielezea juu ya namna anavyoendesha familia yake bila ya msaada wowote, mama mzazi wa Laila na Aziza anasema alitengana na mume wake ambaye pia alikuwa haoni na sasa anaishi sehemu nyingine.

Mama huyo, Mwajuma Merengwe Nasoro, mkazi wa Simbani anasema yuko kwenye wakati mgumu wa kulea familia ya watu sita ambao hawaoni huku akiwa hana shughuli yoyote ya kumuingizia kipato zaidi ya kulima vibarua na kuchoma mkaa.

Merengwe anasema aliolewa na Nasoro Abdala (80) ambaye naye haoni lakini miaka michache iliyopita waliachana na kubaki na mzigo mkubwa wa kulea familia hiyo ambayo anasema wanajipatia riziki katika mazingira magumu.

Mwajuma anasema licha ya kuwa na familia hiyo yenye watoto wanne wasioona na wajukuu wawili ambao pia hawaoni hana msaada wowote kutoka serikalini, mashirika au watu binafsi.

Anataja familia watoto wake wasioona kuwa ni Laila (30), Aziza (26), Asia (21), Kassim (18) na Latifa huku wajukuu wakiwa ni Majidi Maulid (11) anayesoma darasa la tatu mkoani Tanga kwenye shule ya wasioona ya Irente na Tariq ambaye ana miaka tisa na hajaanza kusoma.

Anasema Tariq alipopimwa alionekana hana uwezo wa kuona mbali lakini anahitaji matibabu ili asije akashindwa kuona kabisa kama wengine. “Watoto wangu wanne pamoja na wajukuu wawili hawaoni.

Ninashirikiana na mwanangu mmoja ambaye ana uoni hafifu kwani usiku haoni kabisa na mkwe wangu kuendesha familia,” anasema Mwajuma. Anasema ingawa inaweza kuwa ni suala la kurithi kwa baba yao lakini watoto wake wamekuwa wakipata ulemavu wa kutoona katika mazingira ya ajabu.

“Huwa ninawazaa wazima lakini wanapofikia umri fulani wanapoteza uwezo wa kuona,” anasema.

Anaongeza: “Ninaishi kwenye mazingira magumu mimi na familia yangu nafikiri kama kungekuwa na watu wanaosaidia basi wangetupatia misaada ili nasi tuweze kujiendesha vizuri zaidi ya sasa,” anasema Mwajuma.

Anasema nyumba wanayoishi ni ya ndugu yao na kwamba mazingira ni magumu sana kwani wanahangaika kupata mahitaji hasa ya chakula.

“Tunashukuru wakati mwingine tunapata msaada kutoka kwenye chama cha watu wasioona wilaya ya Kibaha. Wakipata chochote huwa wanatuletea tunashukuru,” anasema mama huyo.

Anasema licha ya kuwepo kwa mpango wa kunusuru kaya maskini, familia yao haijawekwa kwenye mpango huo na hajui wanaowekwa huko huwa na vigezo gani.

“Tunaomba wadau mbalimbali watuangalie namna ya kutusaidia ikiwa ni pamoja na mashirika yanayosaidia kwani hali ni ngumu sana. Kutokana na ugumu wa maisha mwanangu mmoja ambaye ni binti, licha ya kuwa haoni lakini lakini analazimika kulima, kuchoma mkaa na kufuma mikeka ili kujipatia kipato,” anasema Mwajuma.

Katibu wa Shirikisho la Watu Wenye Ulemavu (Shivywata) Kibaha, Happiness Matagi ambaye pia haoni pia anasema kuwa watu wasioona hususani wanawake hawako nyuma katika kupambana na maisha kwani wamejipambanua na kuacha kuomba omba mtaani.

Matagi anasema yeye mwenyewe anafanyabiashara ya duka la soda za jumla na rejareja pamoja na uuzaji wa sabuni ya maji eneo la Tanita kata ya Mkuza wilaya ya Kibaha.

Anasema kikubwa ambacho kinawainua ni fedha za mikopo kutoka Halmashauri ya Mji wa Kibaha ambazo watu wenye ulemavu hasa wasioona wamejitokeza kukopa.

“Katika marejesho kidogo kuna changamoto za urejeshaji mikopo lakini hata hivyo uongozi umekuwa ukiwafuatilia na kuhamasisha watumie vizuri fedha wanazokopeshwa ili waweze kufanya marejesho ili baadaye wengine waweze pia kukopeshwa,” anasema Matagi.

Kwa upande wake mlezi wa Shivywata mkoa wa Pwani ambaye pia ni mlemavu asiyeona, Robert Bundala anaishukuru serikali kwa kuendelea kutenga fedha asilimia mbili kwa ajili ya watu wenye ulemavu kwani anasema wananufaika nazo.

Bundala anasema kutokana na serikali kuhamasisha watu wenye ulemavu kushiriki shughuli za kimaendeleo na kujiongezea kipato zimesababisha kubadili maisha ya kundi hilo la watu wasioona na hasa kuwaondoa kwenye kuombaomba.

“Tunachofanya sisi kama viongozi ni kuwatafutia fursa mbalimbali ikiwa ni pamoja na mikopo kama hiyo pia tunawaomba wadau mbalimbali wajitokeze kuwasaidia watu wenye ulemavu wakiwemo wale wasioona kwani wameonekana nao hawako nyuma kujishughulisha,” anasema Bundala.

Mtoto wa Mwajuma aitwaye Kassim Nasoro ambaye pia ana uoni hafifu anasema katika kuhangaika kujipatia kipato walianzisha kikundi cha watu wasioona kiitwacho Dira Mpya ambapo walikopeshwa kiasi cha shilingi milioni mbili.

Anasema katika kikundi chao cha watu wanane kila mtu ana shughuli yake lakini yeye anajishughulisha na kuchoma mkaa. Baba wa familia ya wasioona, Mzee Nasoro Abdala (84) anasema yeye alianza kupoteza uwezo wa kuona akiwa na miaka 40 lakini watoto wake aliowazaa wakiwa wazima wamewahi sana kupoteza uwezo wa kuona na hajui sababu.

“Lakini nilikuwa ninajaribu kuwapeleka hospitali kwa ajili ya matibabu lakini sikupata mafanikio,” anasema.

Anasema alishindwa kuelewana na mkewe ndio maana akatoka lakini anakiri kwamba familia yake na hata yeye mwenyewe wana maisha Laila akiwa na mama yake mzazi, Mwajuma Merengwe. magumu sana.

Chanzo: habarileo.co.tz