Lifestyle

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

SIL

Faili la Malkia Elizabeth II hili hapa

Malkia Eliza Wa Pili Malkia Elizabeth II na familia yake

Mon, 12 Sep 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mchana wa Alhamisi (Septemba 8, 2022), upepo ulibadilika baada ya taarifa kutoka ndani ya kasri la Kifalme la UK, Buckingham Palace, kutoa habari kuwa hali ya Malkia Elizabeth II haikuwa njema na aliwekwa kwenye uangalizi maalum.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa Malkia Elizabeth II, alikuwa amepumzishwa kwa ajili ya kutazamwa kwa ukaribu na madaktari, kwenye kasri la Balmoral Castle, Aberdeenshire, Scotland.

Balmoral Castle ni jumba la mtoto wa kwanza wa Malkia Elizabeth II, Mfalme Charles, ambaye ameshavaa rasmi taji la Ufalme wa UK na baadhi ya nchi za Jumuiya ya Madola, kufuatia kifo cha mama yake.

Mshangao ulikuwa baada ya taarifa hiyo, wanafamilia wa Malkia Elizabeth II, walifunga safari kutoka sehemu mbalimbali, kuelekea Balmoral Castle.

Watoto wote wanne wa Malkia Elizabeth; Charles, Anne, Andrew na Edward, vilevile mtoto wa kwanza wa Charles, William ambaye ni hivi sasa ndiye mrithi namba moja wa taji la Mfalme, wote walifika haraka Balmoral.

Wajukuu wengine wa Malkia Elizabeth II, akiwemo Harry na mkewe Meghan, ambao walisusa maisha ya kifalme na kwenda kuishi Marekani kwa madai ya ubaguzi, waliahirisha ghafla ushiriki wao kwenye Tuzo za Wellchild, zilizofanyika London, Alhamisi usiku.

Harry alisafiri kwenda Scotland, kuungana na wanafamilia kwenye kasri la Balmoral Castle. Meghan alibaki London kwa muda kabla ya kuungana na mumewe msibani siku.

Wito wa haraka kwa kila mwanafamilia ya kifalme, vilevile taarifa ya afya ya Malkia Elizabeth II kuwekwa hadharani, ilianza kujenga picha hudhuni duniani. Wengi kuanza kusubiri tangazo la kifo.

Mamia ya watu walikusanyika nje ya kasri la Balmoral Castle kuonesha kuguswa na afya ya Malki Elizabeth II. Wapo walioshindwa kujizuia na kumwaga machozi. Hisia ziliwajuza kuwa Malkia tayari amekwenda.

Mshangao ulikuwa mkubwa pia kutokana na ukweli kuwa siku mbili kabla, yaani Jumanne (Septemba 6), alimteua Liz Truss kuwa Waziri Mkuu mpya wa Uingereza.

Siku hiyo, Malkia alikuwa mwenye tabasamu pana. Kitendo cha afya yake kubadilika ghafla, kulijenga pia hofu kwamba pengine Malkia alidondoka.

Kumbe, ilimpendeza Mungu kazi ya mwisho ya Malkia Elizabeth II, iwe kumteua Liz Truss na kumbariki kwenda kuunda serikali mpya, kwani jioni ya Alhamisi, saa 12:30 Greenwich (saa 2:30 usiku Tanzania), tangazo lilitolewa kuwa mwanamke huyo aliyekuwa na nguvu kuliko wote duniani, tayari alishaitikia wito wa mauti.

Naam, ni ahadi iliyopo kwenye kila kitabu kitakatifu kuwa mwisho wa binadamu ni kifo. Rastafarians ndio hawaamini katika kufa kupitia nadharia yao ya Livity, kwamba wao huishi milele. Ukiondoka duniani unakwenda bustanini Eden kuendelea na maisha.

TUFUNGUE FAILI

Elizabeth Alexandra Mary ndio jina alilomaanishwa kulitumia. Alikuwa mtoto wa mwanamfalme ambaye haikutarajiwa hata kidogo kama angekuwa Malkia wa United Kingdom na dola nyingine za Jumuiya ya Madola.

Tuweke tafsiri sahihi; United Kingdom (UK) ni dola kubwa inayojumuisha Uingereza (England), Scotland, Wales na Northern Ireland.

England, Scotland na Wales kwa pamoja huitwa Great Britain. Hivyo UK ni Great Britain jumlisha Northern Ireland.

Tuendelee; Elizabeth alikuwa mbali kabisa na mnyororo wa kurithi taji la Ufalme wa UK. Elizabeth ni mtoto wa Albert ambaye ni mdogo wa Edward.

Mfalme George V na mkewe, Malkia Mary, walipata watoto sita; Edward wa kwanza, wa pili Albert, kisha Victoria (Princess Mary au Princess Royal), Henry, George na John.

Januari 20, 1936, Mfalme George V alifariki dunia. Edward alitawazwa kuwa Mfalme wa UK, akatumia jina la Edward VIII.

Kwa utaratibu wa urithi wa Ufalme wa UK wakati huo, mtoto mkubwa wa kiume anakuwa namba moja, kisha watoto wa mtoto mkubwa wa kiume wanaunga orodha kulingana na uzao. Mkubwa anakuwa wa kwanza.

Ikiwa Mfalme au Malkia anakuwa hana mtoto wa kiume, basi yule mkubwa wa kike ndiye anatawazwa kuwa Malkia. Elizabeth kwa baba na mama yao walizaliwa wawili, wote wa kike. Mdogo wake ni Margaret ambaye alifariki dunia Februari 9, 2002.

Mathalan, mtoto mkubwa wa Elizabeth ni Charles ambaye ndiye Mfalme wa UK anayesubiri utawazo. Mrithi namba moja wa kiti cha ufalme (the Crown Prince au Heir Apparent) ni William (mtoto wa kwanza wa Charles). Mrithi namba mbili (second in line) ni George (mtoto wa kwanza wa William).

George naye akipata watoto, yule wa kwanza ndiye atakuwa mrithi namba tatu. Hivyo, Edward VIII angeendelea kuwa Mfalme wa UK, ingekuwa ndoto kwa Elizabeth kutawazwa kuwa Malkia. Mtoto wa kwanza wa Edward angerithi, kisha mjukuu namba moja na kuendelea.

Mwaka 2011, Bunge la UK, lilifanya mabadiliko ya sheria na kuondoa kikwazo cha mtoto wa kike kurithi ufalme mbele watoto wa kiume. Hivyo, kuanzia mwaka 2011, mtoto wa kike akiwa mkubwa anaruhusiwa kurithi ufalme mbele ya kaka zake.

Hiyo ndio sababu, William (Heir Apparent), mtoto wake wa pili ni wa kike, Charlotte na wa tatu ni Louis (kiume). Charlotte ni mrithi namba tatu, Louis ni wa nne. Kabla ya mabadiliko ya sheria ya mwaka 2011, Louis angekuwa wa tatu na dada yake angesogea kuwa wa nne.

ELIZA ALIKUWAJE MALKIA?

Mwaka 1936, mgogoro wa kikatiba uliibuka UK. Edward VIII akiwa Mfalme, alimchumbia mwanamke raia wa Marekani, Wallis Simpson, aliyekuwa ametalikiwa katika ndoa ya kwanza, na wakati huohuo akawa anapigania talaka kwenye ndoa yake ya pili.

Mpango wa Edward VIII kumuoa Wallis ulipingwa na Serikali ya UK na mataifa yote chini ya Ufalme wa UK. Kingine, Mfalme wa UK kidini huhesabika kama Mkuu wa Kanisa la England ambalo lilipinga mtu aliyetalikiwa kufunga ndoa kanisani.

Kwa kifupi ndoa ya Mfalme Edward VIII na Wallis ilipingwa kiserikali na kidini. Zaidi, ilitafsiriwa kwamba Wallis alitaka aolewe na Mfalme Edward kwa sababu ya fedha na madaraka. Wallis akazuiwa kuwa Malkia wa UK. Edward akalazimika kuachia kiti cha Mfalme wa UK, na kumwachia mdogo wake, Albert, atawazwe kuwa Mfalme mpya, akaitwa Mfalme George VI.

Mwandishi wa Marekani, Anne Sebba kupitia kitabu chake chenye jina “That Woman: The Life of Wallis Simpson, Duchess of Windsor”, amesimulia Kuwa Edward alisusa Ufalme kwa ajili ya Wallis si kwa sababu ya mapenzi tu, bali pia alikuwa na matatizo mengi ya kisaikolojia, vilevile hakupenda madaraka.

Sasa, kwa utaratibu uleule, Albert au Mfalme George VI, mrithi wake namba moja akawa Elizabeth, mtoto wake wa kwanza. Ndio maana Mfalme George VI alipofariki dunia Februari 6, 1952, Elizabeth akawa Malkia wa UK.

Zingatia kuwa ukiwa Mfalme au Malkia wa UK, unakuwa mkuu wa nchi za Canada, New Zealand, Australia, Jamaica, Barbados, The Bahamas, Grenada, Papua New Guinea, Visiwa vya Solomon, Tuvalu, St Lucia, St Vincent na Grenadines, Belize, Antigua na Barbuda, St Kitts na Nevis. Elizabeth alikuwa Malkia wa dola zote hizo.

MALKIA AKIWA MTINI

Mwanasiasa na mwanadiplomasia wa UK, Harold Nicolson, kupitia moja ya machapisho yake ya “Harold Nicolson Diaries”, aliandika kuwa Elizabeth alifikiwa na Umalkia wa UK akiwa juu ya mti, barani Afrika.

Harold aliandika: “Elizabeth alikuwa Malkia akiwa juu ya mti akiwashuhudia vifaru wakishuka kwenye bwawa kunywa maji.”

Elizabeth alikuwa likizo Sagana, Kirinyaga, Kenya, mbugani, akitazama wanyama. Baba yake alifikwa na mauti akiwa usingizini, Sandringham, Norfolk, England. Hivyo, kuanzia Februari 6, 1952, alianza kutambulika kama Malkia Elizabeth II.

Hata hivyo, Elizabeth alitawazwa rasmi kuwa Malkia wa UK miezi 16 baadaye. Ilikuwa Juni 2, 1953. Hivyo, ukipiga hesabu kutoka siku alipotawazwa kuwa Malkia mpaka Septemba 8, 2022, alipofariki dunia ni miaka 69 na miezi mitatu.

Hata hivyo, ukihesabu kutoka siku ya kifo cha baba yake, utapata miaka 70 na miezi saba. Elizabeth II amefariki dunia akiweka rekodi ya kuwa mtawala wa UK aliyekaa madarakani kwa miaka mingi zaidi. Alimpiku Malkia Victoria, aliyedumu madarakani kwa miaka 64 (mwaka 1837 – 1901).

Sababu ya Elizabeth kuchelewa kutawazwa kuwa Malkia wa UK ni utamaduni uliokuwepo ndani ya Familia ya Kifalme kuwa mwenye taji akifa, angalau kipite kipindi cha kumuenzi kabla ya uapisho wa mrithi wake.

Vilevile, kwa Elizabeth kulikuwa na maagizo kutoka kwa bibi yake mzaa baba, Malkia Mary wa Teck (Victoria Mary). Malkia Mary alikuwa mke wa Mfalme George V (Royal Consort) na mama mzazi wa Mfalme George VI (Queen Mother).

Malkia Mary alitaka utawazo wa Elizabeth kuwa Malkia uchelewe ili kutoa kipindi cha mpito kumuenzi mwanaye, George VI (Albert), aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 56. Malkia Mary alifariki dunia Machi 24, 1953. Miezi miwili na siku tisa baadaye, Eliza alitawazwa kuwa Malkia.

Malkia Elizabeth katika maisha yake, alipata watoto wanne; Charles, Anne, Andrew na Edward. Wote wapo hai. Ameacha wajukuu nane na vitukuu 12.

Anaitwa Elizabeth II kwa sababu yupo Malkia Elizabeth I. Ni mama yake mzazi. Elizabeth I alikuwa Queen Mother kuanzia Februari 6, 1952 mpaka Machi 30, 2002, alipofariki dunia. Vilevile alikuwa Malkia Mwenzi wa Mfalme (Royal Consort) kuanzia Desemba 11, 1936 mpaka Februari 6, 1952.

Elizabeth I alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 101, wakati Elizabeth II, amepokea faradhi ya mauti katika umri wa miaka 96.

Wakati baba yake, Mfalme George VI, alipotawazwa kuwa Mfalme, Elizabeth II alikuwa na umri wa miaka 10. Miaka mitatu baadaye, alikutana na Philip, ambaye alikuwa mwanamfalme wa Ugiriki. Penzi likachipua.

Eliza wa Pili na Philip walifunga ndoa mwaka 1947. Watoto wote wanne, Eliza wa Pili aliwapata na Philip.

Kazi ya mwisho ambayo Malkia Elizabeth II aliifanya ilikuwa Septemba 6, mwaka huu, alipomteua “wa jina wake", Liz Truss kuwa Waziri Mkuu mpya wa UK.

Jina kamili la Liz Truss ni Mary Elizabeth Truss. Hata hivyo, amekuwa akifahamika zaidi kwa jina lake la katikati, yaani Elizabeth ambalo hulifupisha na kuwa Liz. Hivyo, Liz Truss ni Elizabeth kama Malkia.

Na Luqman MALOTO

Chanzo: www.tanzaniaweb.live