Lifestyle

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

SIL

Faida na Hasara kwa wapenzi wanaotumia majina ya wenza wao

Enemies To Lovers Romance Faida na Hasara kwa wapenzi wanaotumia majina ya wenza wao

Wed, 1 Sep 2021 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Wakati utamaduni wa baadhi ya wanawake kubadilisha majina na kutumia ya familia za wenza wao, ukionekana kama njia mojawapo ya kukuza upendo, wanasheria wameonya kuhusu utamaduni huo na kueleza kuwa una athari nyingi ikilinganishwa na faida.

Baadhi ya wanasheria hao wameeleza kuwa kubadilisha jina kunaweza kumletea usumbufu mhusika, na wakati mwingine kuingia kwenye mvutano pindi ndoa inapokoma.

Kuna ushahidi wa matukio kadhaa ya wanawake kutakiwa kusitisha kutumia majina ya wenza wao, baada ya ndoa kuvunjika ilhali walishajitambulisha kwa majina hayo tena kisheria.

Akizungumza na Mwananchi hivi karibuni, wakili wa kujitegemea, Bashir Yakub alishauri kuwa ni vyema wanawake wakaachana na utaratibu wa kubadilisha majina, kwa kuwa faida zake ni chache ukilinganisha na hasara.

Kwa mujibu wa Yakub, faida pekee inayoonekana baada ya mke kutumia jina la mumewe ni kutimiza lengo la kuingia kwenye familia hiyo na kuwa mwili mmoja, lakini mambo huwa tofauti pale ndoa hiyo inapofika ukomo na wenza hao kulazimika kuachana.

Alisema mbali na usumbufu unaoweza kujitokeza baada ya ndoa kuvunjika, matumizi ya jina la ukoo mwingine yanaweza kuleta shida kwenye utambulisho.

ADVERTISEMENT Wakili huyo alifafanua kuna baadhi ya taasisi za Serikali zinazotoa nyaraka nyeti kama vile vyeti vya kuzaliwa au vyeti vya elimu ambazo huwa hazitakiwi kubadilisha jina, hivyo mhusika licha ya kubadilisha jina pia atatakiwa kuwa na nyaraka za jina alilosajiliwa awali.

“Binafsi nikiambiwa nishauri ningewashauri wanawake kuachana na huu utamaduni. Ukiangalia kwa kina hasara ni nyingi na hakuna uthibitisho wowote kwamba ukitumia jina la ukoo wa mumeo ndoa itakuwa imara zaidi.

“Ikitokea umetumia jina la ukoo wa mumeo kwenye biashara au utambulisho mwingine wowote na yeye akaamua jina hilo lisitumike baada ya ndoa hiyo kukoma, jambo hilo linaweza kukuyumbisha kwa namna moja au nyingine. Kesi hizi zipo na binafsi nimeshawahi kukutana nazo.

Kwa mfano, ilikuwepo moja ambayo nimeifanyia kazi; mume alisimama kidete hataki jina lake litumike kwenye biashara ya aliyekuwa mkewe,” alisema wakili Yakub na kuongeza;

“Hata ikitokea unafuatilia hati ya kusafiria, itakuchukua muda mrefu kujieleza ukilinganishwa na yule ambaye nyaraka zake zote zinaonyesha jina moja, hivyo kwa kifupi kuna changamoto.”

Hilo liliungwa mkono na mwanasheria mwingine ambaye hakutaka kuweka wazi jina lake akieleza kuwa hasara za kubadilisha jina ni nyingi kuliko wengi wanavyofikiria.

Alisema inamfanya mwanamke kupoteza utambulisho wake uliokuwa ukifahamika awali, kitu ambacho ni muhimu katika harakati za kimaisha.

Pia, alisema kutumia jina la ukoo mwingine inaweza kumfanya mwanamke kunyanyasika, akionekana kama anapata hisani kwa kutumia jina hilo.

“Katika familia zetu za Kiafrika si kitu cha ajabu kusikia hakuna maelewano kati ya mke na mawifi, au mashemeji.

Sasa hawa wanaweza kuona huyu kutumia jina la ukoo wao ni fahari kwake, basi hapo ndipo unyanyasaji unapoanzia, huku wakihoji kwa nini utumie jina letu kwanza wewe sio wa kwetu,” alisema mwanasheria huyo.

Hata hivyo, wakili Yakub alibainisha kuwa katika miaka ya karibuni wanawake wachache wamekuwa wakibadili majina yao baada ya kufunga ndoa ikilinganishwa na ilivyokuwa miaka ya nyuma.

“Sasa ni wanawake wachache wanaofanya hivyo, huenda ni kwa sababu ndoa zenyewe zimekuwa hazidumu au wameshaona athari za kubadili. Wapo wachache wanaoendelea ila wengi siku hizi wanatumia majina yao ya awali.”

Rhoda Otaigo mkazi wa Chang’ombe jijini Dar es Salaam, alisema licha ya kuolewa hatumii jina la ukoo wa mume wake kwa kuwa haoni sababu ya kufanya hivyo.

“Sioni kama kuna ulazima wa kubadilisha jina, nimeolewa na ninatambua kuwa yule ni mume wangu, lakini sioni ulazima wa kutumia jina lake.

Kwanza tayari natambulika kwa jina langu, pili siku hizi ndoa zenyewe hazieleweki ikitokea mmeachana inakuwa shida, yaani nianze tena kuingia kwenye kibarua kingine cha kubadilisha jina; hapana acha tu nibaki na jina langu,” alisema Rhoda.

Kauli ya mwanasaikolojia

Akizungumzia hilo, mwanasaikolojia Saldin Kimangale alisema wanawake wengi wanatumia majina ya ukoo wa wenza wao kwa ajili ya usalama na kuonyesha utambulisho.

“Huu ni utaratibu ambao jamii tumeutengeneza, ila sioni kama ni sahihi; unaweza kumsababishia mwanamke kupoteza haki zake na hata utambulisho wake, kwa kuwa anaamini kwamba anapata usalama au kuonekana ameolewa kwenye familia fulani,” alisema Kimangale.

Mshauri wa uhusiano, Deogratius Sukambi anasema mazingira ya sasa yamefanya wanawake kukosa umuhimu wa kutumia majina ya waume zao tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz