Kwa kawaida, Jaji wa Wilaya ya Marekani Gary J Brown angeagiza mtu huyo kushikiliwa katika jela ya serikali ya eneo hilo ili kutumikia kifungo chake kwa ulaghai wa kodi.
Lakini jambo moja lilimzuia: “Hali hatari katika jela ya Metropolitan mjini Brooklyn.”
Jela hiyo maarufu, inayojulikana kama MDC, iko kwenye uangalizi kwa mara nyingine tena kutokana na mfungwa wake mashuhuri wa hivi punde. Wiki iliyopita, hakimu wa New York aliamuru Sean "Diddy" Combs ashikiliwe hapo baada ya waendesha mashtaka kumfungulia mashtaka ya unyanyasaji wa kingono, ulaghai, na usafirishaji ili kujihusisha na ukahaba. Amekanusha mashataka.
Washtakiwa mashuhuri kama Bw Combs wakati mwingine hupokea ulinzi maalum wanapofungwa, na nguli huyo wa muziki anaripotiwa kushikiliwa katika sehemu ya MDC Brooklyn iliyotengwa kwa wafungwa wanaohitaji ulinzi maalum.
Kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya ndani, Bw Combs amefungiwa katika chumba kimoja na mjasiriamali wa sarafu ya crypto Sam Bankman-Fried, ambaye aliwahi kuendesha kampuni yenye thamani ya mabilioni ya dola lakini akapatikana na hatia ya ulaghai mwezi Machi.
Na kwa sababu ndiyo jela pekee katika Jiji la New York, ambapo kesi nyingi za hadhi ya juu hushughulikiwa, wawili hao ndio wafungwa wa hivi punde zaidi katika orodha pana ya watu mashuhuri kupita kwenye milango ya kituo hicho. Orodha hiyo inajumuisha rapper R Kelly pamoja na mshirika wa Jeffrey Epstein, Ghislaine Maxwell.
Katika uamuzi wa hukumu wa Agosti, Jaji Brown alitaja kesi nyingi za majaji wenzake ambao walisita kuwapeleka washtakiwa na wafungwa katika jela hiyo kutokana na hali yake.
"Madai ya kutosimamiwa ipasavyo, mashambulio yasiyodhibitiwa, na ukosefu wa huduma ya matibabu yanashabihiana na ushahidi ambao hauwezi kupingwa," alisema.
"Machafuko yanatawala, pamoja na ghasia zisizodhibitiwa," Jaji Brown aliongeza. Uamuzi wake ulijumuisha kisa cha mshtakiwa ambaye alichomwa kisu mara kadha lakini akaripoti kuwa hakupata huduma ya matibabu, badala yake alitengwa kwa kwa chumba kingine siku 25. Jaji alitaja uhaba wa wafanyikazi na hali mbaya zaidi baada ya janga la Covid ambayo ililazimu jela kufungwa.
Ikiwa Ofisi ya Magereza itaamua kumpeleka mshtakiwa wa kesi ya ulaghai wa kodi katika jela ya MDC, hakimu aliandika, angeondoa kifungo cha mtu huyo.
Historia ya matatizo Jela la MDC Brooklyn lilifunguliwa miaka ya1990, na masuala yake yalianzia miaka ya nyuma.
Mnamo 2019, tukio la moto katika majira ya baridi kali lilisababisha kukatika kwa umeme, na kutumbukiza jela hilo kwenye giza na hali ya baridi.
Na mnamo Juni 2020, mfungwa, Jamel Floyd, alifariki baada ya kunyunyiziwa pilipili na maafisa wa magereza. Familia yake iliishtaki serikali kwa kifo chake. Ukaguzi wa Idara ya Haki ulihitimisha kuwa kulikuwa na "ushahidi wa kutosha" kwamba mamlaka ya magereza "ilijihusisha na utovu wa nidhamu," lakini ilikubali kwamba utumiaji wa dawa ya pilipili ilikiuka sera.
Jaji Brown sio jaji pekee aliyekosoa vikali kituo hicho.
Mnamo Januari, Jaji Jesse Furman wa Mahakama ya Wilaya ya huko Manhattan alikataa kutuma mtu ambaye alikiri hatia katika kesi ya dawa za kulevya kwa sababu ya hali yake hatari.
Baada ya kumruhusu mtu huyo Gustavo Chavez, hapo awali kusubiri hukumu baada ya kuachiliwa huru, hatimaye Jaji Furman alimruhusu kupita MDC na kuripoti moja kwa moja gerezani ambako angetumikia kifungo chake.
Mnamo Julai, Edwin Cordero mwenye umri wa miaka 36 alikufa baada ya kujeruhiwa kwenye mapigano alipokuwa akitumikia kifungo katika jela MDC.
"Mazingira duni yanachochewa na aina hii ya mkanganyiko wa hali," Andrew Dalack, wakili wa Bw Cordero na Bw Chavez, aliiambia BBC. "Msongamano, uhaba wa wafanyikazi na ukosefu wa utashi wa kisiasa wa kushughulikia hali hiyo."
Kama mtetezi wa umma anayeishi Brooklyn, Bw Dalack amewakilisha wateja wengi ambao wamepelekwa MDC. "Ni mahali pa kutisha sana kushikiliwa," alisema.
Baada ya kifo cha Bw Cordero, Mbunge wa Marekani Dan Goldman, ambaye anawakilisha wilaya ambayo kituo cha Brooklyn kinapatikana, alitoa wito kwa serikali kushughulikia "upungufu wa wafanyikazi, kifungo cha upweke na vurugu iliyoenea".
Ofisi ya Idara ya Magereza, ambayo inasimamia kituo hicho, ilisema katika taarifa kwamba "tunachukua kwa uzito jukumu letu la kuwalinda watu waliowekwa chini ya ulinzi wetu, na pia kudumisha usalama wa wafanyikazi wa magereza na jamii".
Msemaji wa ofisi hiyo alidokeza kuundwa kwa timu ya dharura, ambayo itashughulikia masuala katika MDC, na jitihada zinazoendelea za kuajiri wafanyakazi zaidi na kushughulikia masuala ya ukarabati.
Ripoti ya Februari 2024 iliyokusanywa na ofisi ya Watetezi wa kitaifa ilihusisha masuala ya msongamano wa watu na kufungwa kwa kituo kingine huko Manhattan, ambacho serikali ilifunga mwaka 2021 - miaka miwili baada ya kifo cha Jeffrey Epstein katika kituo hicho.
Pia walisema uwepo wa dawa za kulevya na magendo mengine huchangia mazingira hatarishi ya kituo hicho.
Kituo hicho kinashikilia watu ambao wamepatikana na hatia ya uhalifu, lakini sehemu kubwa ya watu wanasubiri uamuzi wa kesi katika mahakama za kitaifa zinazoendeshea katika ngazi ya jiji.
Masharti yalikuwa magumu kwa wateja wa Bw Dalack, ambao tayari walikuwa wanakabiliwa na uwezekano wa kufungwa jela zaidi.
"Hufai kutelekezwa wakati unapigania uhuru wako," alisema. "MDC Brooklyn ina njia ya kuwavunja watu, na kuwafanya wakose matumaini."