Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fahamu bendi 5 za majeshi zilizotikisa

Bendi Jeshi Msl Bendi 5 za majeshi zilizotikisa

Mon, 5 Dec 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati wa utawala wa Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kila shirika na kampuni nchini lilikuwa ama lina timu na mpira wa miguu, netiboli, mpira wa kikapu, ngumi, bendi za muziki wa dansi, taarabu au vyote kwa pamoja.

Na bendi za muziki wa dansi hazikuwa kwenye mashirika na makampuni peke yake, bali hata kwenye majeshi yetu ya ulinzi na usalama.

Leo tutaziangazia bendi za majeshi ya Tanzania. Lengo lilikuwa ni kuwaburudisha makamanda wapiganaji kila wikiendi, wakati mwingine na familia zao.

Kama vile haitoshi, ilikuwa ni kuwapa burudani Watanzania wote, kwani bendi hizo mbali na kupiga makambini, lakini zilikuwa zikipiga kwenye kumbi mbalimbali nchini na zilikuwa zikisafiri nchi nzima.

Kuna wakati bendi za majeshi zilisafiri na kwenda kuburudisha wapiganaji kwenye vita ya Kagera mwaka 1978 hadi 1979.

Kiufupi hazikuwa bendi za mchezo mchezo, kwani zilikuwa maarufu na tishio kwa bendi za raia. Ingawa nyingi bado zipo, lakini si shindani tena kama zamani.

Mwenge Jazz Band

Hii ndiyo unaweza kusema kama bendi mama ya zote zilizomilikuwa na majeshi. Wenyewe walipenda kuiita 'Mwenge ya Mashujaa'.

Ilikuwa ni bendi tishio na maarufu zaidi ya bendi zote, ikikusanya wanamuziki mahiri nchini Tanzania. Ilikusanya vijana wa Kitanzania wenye vipaji na kuwapa ajira za muziki, na jeshi pia.

Hata hivyo kuna wengine walibakiwa kuwa wanamuziki tu. Bendi hii ipo mpaka sasa, ingawa haina nguvu zile kama za mwanzo ilipokuwa ikishindana na bendi kubwa kama za Msondo na Sikinde.

Inamilikiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ). Ilivuma sana katikati ya miaka ya 1970 hadi katikati ya miaka ya 1980.

Nyimbo ambazo zilitia fora na kuifanya bendi hiyo kuheshimika ndani na nje ya nchini ni 'Rehemu', 'Kupatwa kwa Mwezi', 'Mwanahawa', 'Tofali la Barafu','Chenga bin Utoe', na nyingine nyingi.

Polisi Jazz Band

Ilikuwa ni bendi ya pili kwa ukubwa na umaarufu kwa bendi za majeshi, ukiondoa Mwenge Jazz Band.

Hii inamilikiwa na Jeshi la Polisi la Tanzania, Makao Makuu yake yakiwa maeneo ya Kilwa Road, maeneo ya Kurasini jijini Dar es Salaam.

Iliwika sana miaka ya 1978, hadi 1981 wakati ilipokuwa na wanamuziki mahiri kama Tx Moshi William, Kassim Mapili, Jalala Ally na wengineo. Ilipendwa mno na mashabiki wa muziki wa dansi Tanzania kwa vibao vyao kama 'Tuli', 'Mwaka wa Watoto', 'Mayasa', 'Wivu Sina' na na nyingine nyingi. Bado ipo, ingawa imepungua makali yake.

Magereza Jazz Band

Ni bendi inayomilikuwa na Jeshi la Magereza. Haikuwa maarufu sana kuliko zingine. Lakini kuna wakati ilikuwa ikitoa nyimbo chache zilizopendwa.

Hata hivyo, bendi hii ilijinyakulia umaarufu wa muda mfupi, ilipowachukua wanamuziki kama Abel Bathazar, Hassan Kunyata, Nana Njige na wengineo mwanzoni mwa miaka mwanzoni mwa 1990 na mtindo wao wa 'Mkote Ngoma, Kubali Yaishe' na kutoa vibao vilivyoondokea kuwa gumzo kama 'Edina', 'Ashura' na nyingine nyingi.

JKT Kimbunga Stereo

Bendi hii ilikuwa ya kawaida, lakini ilipomchukua John Simon kutoka Nuta Jazz, ndipo ilipoanza kupiga muziki wa ushindani.

Iliwaleta baadhi ya wanamuziki kama Mwarami Said ambaye baadaye alikwenda Sikinde, na kutoa vibao kama 'Cheza Rhumba Kimbunga', 'Ushirikina', 'Chakula Cha Shida' na nyinginezo.

Bendi hii ilimilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

JKT Mafinga 'Kimulimuli

Pia bendi hii ilimilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), lakini haikuwa Dar es Salaam, bali mkoani Iringa. Ilikuwa ni kama kikosi cha pili cha JKT Kimbunga. Ni kwamba baadhi ya wanamuziki walioonekana wamekosa nafasi Kimbunga, walipelekwa Iringa.

Walimpata pia Zahir Ally Zorro wakafanya kazi ya maana. Wimbo wao wa kwanza ambao uliwafanya kuanza kuwa maarufu na bendi tishio si kwa JKT Kibunga yenyewe tu, bali hata bendi nyingine ni 'Christina' uliotoka mwaka 1977, uliotungwa na kuimbwa na Zahir.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live