Takwimu zinasema talaka zimekuwa nyingi sana siku hizi. Ndoa nyingi zinavunjika, uhusiano unaharibika, huku sababu kubwa ikitajwa kuwa ni uaminifu.
Watu kwenye hizi ndoa, uchumba na uhusiano kwa jumla wamekosa uaminifu kabisa.
Pia, takwimu zinasema wanaume wanaongoza kwa kutokuwa waaminifu na kukamatwa kwa kosa la kutokuwa waaminifu.
Yaani mwanamke na mwanamume wote wanaweza kuchepuka, lakini mwanamume atakuwa na asilimia kubwa ya kubambwa.
Nitakupa sababu mbili za kwanini iko hivyo.
Kwanza tunafanya uhuni na wanawake wasiojua mipaka yako. Uaminifu ni uongo na una sheria kuu mbili, kuwa na kumbukumbu na kuwa na msimamo wa kufuata makubaliano.
Unapokuwa na mchepuko huwa unatengeneza sheria ya mawasiliano kwamba hakuna kukupigia simu baada ya saa nne usiku. Hakuna kutuma meseji hatarishi giza likishaingia na mambo mengine kama hayo.
Na kwa kawaida hamuishii kwenye kupeana sheria tu, bali mnapeana hadi sababu za kwa nini sheria hizo zipo.
Hakuna kutafutana baada ya saa nne kwa sababu muda huo unakuwa usharudi nyumbani na uko karibu ya mkeo.
Lakini tatizo michepuko yetu ndio pasua kichwa, ni kama vile hawaelewi mipaka yao. Mtu anataka kuwa kama yeye ndio mke vile.
Anataka kukupigia simu popote anapojisikia, kukutumia meseji za kihuni kihuni na wizi wizi popote anapoona sawa. Matokeo yake inakupa ugumu kutunza siri ya huu uhuni wako usijulikane.
Tofauti na sisi. Mwanamume anapokuwa mchepuko, anapojua anakula visivyo vyake huwa ni makini sana kufuata sheria. Ni nadra kuona mwanamume anapiga simu usiku, anatuma meseji kwenye mazingira hatarishi.
Na ndiyo maana wanawake wanaonekana wako vizuri kwenye kuficha uhuni wao. Sio wao, ni sisi ndio tunawasaidia.
Pili, kuchepuka ni kazi ngumu sana. Inahitaji ufiche meseji, uzime simu, utunze kumbukumbu usije ukajichanganya ukamuita mkeo jina la mchepuko wako na kadhalika.
Ubaya ni kwamba, hiyo ni kazi kubwa sana kwa mwanamume, huwezi kufanya mambo yote hayo na bado uwaze ada za watoto, kodi na majukumu mengine muhimu. Hata sayansi inakataa, inasema wanaume hatuwezi kufanya vitu vingi kwa wakati mmoja.
Tufanye nini? Je, tuanze kuchepuka na wanawake wanaojua mipaka yao? Ambao hawapigi simu tukisharudi nyumbani, tukiwa na wake zetu?
Au je, na sisi twende tukajifunze namna ya kufanya mambo mengi kwa pamoja? Njia bora zaidi ni kuachana tu na haya mambo ya kutokuwa waaminifu.