Baada ya kukaa kimya kwa miaka kadhaa bila kusikika kwenye spika za burudani na msikio ya mashabiki, hatimaye rapa mkongwe Tanzania, Ibrahim Musa ‘Roma Mkatoliki’ amesema mapema mwaka huu ataachia albam yake mpya aliyoipa jina la #NipeniMauaYangu.
Roma ambaye kwa sasa anaishi nchini Marekani, amesema ukimya wake wa muda mrefu alikuwa akiandaa albamu hiyo atakayoiachia mapema mwaka huu na tayari ameshatanguliza ngoma ya kwanza aliyoipa jina la albam.
“Huu wimbo una muda ni kama mwaka mmoja hivi, niliuandika mwaka jana mwezi Agosti, nikaanza kuweka hashtag ya #NipeniMauaYangau, watu walinisema kweli, ilitakitakiwa utoke tangu Januari mwaka huu.
“Kingine ambacho watu hawakijui, #NipeniMauaYangu ni jina la wimbo lakini pia ni jina la albam yangu mpya. Kwa hiyo ukimya wa ROMA wa muda wote huo nilikuwa naandaa albam.
“Kabla ya hapo, wimbo wangu wa mwisho unaitwa Diaspora ambao nimefanya na Lady JD. Wakati natambulisha wimbo huo nikasema ndio wimbo wangu wa mwisho.
“Hapo watu hawakunielewa, wakadhjani ni wimbo wa mwisho kwa maana ya kwamba naacha muziki, hapana, nilikuwa naenda kuandaa albam hii mpya ya #NipeniMauaYangu ambayo mwaka huu 2023 itatoka.
“Wakati tunasikiliza huu wimbo na timu yangu wakasema #NipeniMauaYangu ndio wimbo mbovu kuliko zote kwenye albam, nikasema basi acha tuanze kwa kuutoa huu wimbo mbovu,” amesema Roma.