Mchekeshaji na mwanaharakati Eric Omondi ameanza rasmi safari ya kupeperusha kipindi chake moja kwa moja kwenye mtandao wa Instagram kwa siku tatu mfululizo ili kuchangisha pesa za kuwasaidia Wakenya wenye uhitaji maalum.
Omondi alitangaza hilo Jumanne jioni ambapo alisema kwamba atakwenda live Instagram kwa siku tatu bila kukoma ili kuhakikisha kwamba anapata hela hizo na kunyoosha mkono wa msaada kwa watu wenye uhitaji katika kipindi hiki ambapo wengi wa Wakenya wanapitia maisha magumu kutokana na kuzorota kwa uchumi.
“Kesho Jumatano kuanzia saa mbili usiku nitaanza safari ya kuandikisha historia. Nitakuwa ninaenda live Instagram kwa siku tatu mfululizo bila kukoma hadi Jumamosi ili kuchangisha hela kwa ajili ya Wakenya wenye uhitaji,” Omondi aliandika.
Hii si mara ya kwanza kwa mchekeshaji huyo aliyekengeuka na kuwa mwanaharakati na mtetezi wa wanyonge kuandaa hafla ya kuchangisha pesa mitandaoni.
Katika siku za hivi karibuni, Omondi amekuwa akichangisha pesa na kuwasaidia watu wasiojiweza kukimu mahitaji yao ikiwemo chakula na hata matibabu.
Omondi alianza kuchangisha pesa miezi michache iliyopita alipokuwa nchini Uingereza katika kile alichokiita kama ‘Woiyee tour’ ambapo alinuia kuchangisha pesa kwa kuomba omba katika mitaa ya London ili kusaidia watu nyumbani.
Wiki moja baadae, alifanya vivyo hivyo pia nchini Tanzania ambapo alichangisha Zaidi ya shilingi laki moja ambazo alirudi nazo nchini kuwasaidia watu mbali mbali akiwemo kumtoa seli jamaa aliyetiwa mbaroni na polisi wa kupambana na ghasia mtaani Mathare wakati wa maandamano.
Omondi aliahidi kumfungulia duka la kuuza viatu jamaa huyo na pia kuhamisha familia yake kutoka mtaa huo wa mabanda kwenda mtaa wenye hadhi ya wastani.