Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Eric Omondi amtoa jela machinga aliyekamatwa kwa kupiga kelele

Eric Omondi Amtoa Jela Machinga Aliyekamatwa Kwa Kupiga Kelele.png Eric Omondi amtoa jela machinga aliyekamatwa kwa kupiga kelele

Mon, 13 Mar 2023 Chanzo: Radio Jambo

Eric Omondi hatimaye amefanikiwa katika kumtoa jela mwanadada aliyeshikwa na polisi kwa kaunti ya Nairobi almaarufu ‘kanju’ kwa kosa la kupiga kelele akiita wateja jijini.

Hadithi ya kutia huruma ya mwanadada huyo ilisambaa siku chache zilizopita ambapo alionekana akisimulia kwamba alikuwa anafanya biashara ya uchuuzi katikati mwa jiji na kipindi anawaita wateja kwa sauti, kanju wakamshika na kumtia ndani.

“Nilikuwa nje nikiita wateja na kanju walikuja wakanishika, wakanipeleka kituo cha Central na ile pesa nilikuwa naitishwa kama dhamana taslimu sikupata kwa huo wakati. Kituoni niliitishwa elfu 5 lakini nilipokosa nilipelekwa kortini nikapewa dhamani ya pesa taslimu elfu 10 ambazo pia zilikosekana,” mwanadada huyo alielezea katika video moja.

Baada ya kukosa taslimu ya dhamana, alipelekwa katika jela ya wanawake Lang’ata ambako amekuwa akikaa bila kupatiwa dhamana tena.

Mwanadada huyo alikuwa akifanya kazi ya umachinga ambayo malipo yake ni kwa ada ya mauzo.

Baada ya simulizi yake kusambaa, watu mbalimbali walijitoa kwa udi na ambary kumpa msaada, ikiwemo kumtoa jela na kumtafutia kazi nzuri ya kujikimu kimaisha.

Wahisani hao waliongozwa na mchekeshaji Eric Omondi ambaye Jumatatu mchana alipakia video akiwa katika jela ya wanawake ya Lang’ata ambapo alimtoa mwanadada huyo na kusema tayari kuna wengine ambao wamemuahidi kazi ya kufanya.

“Mpaka sasa watu wengi wamejitokeza kumpa msaada...Asante @bernicesaroni kwa kumpatia kazi. Tumemwachilia Joyce Naserian kutoka Gereza la Wanawake la Langata. Alitakiwa kukaa jela miezi 3 kwa kosa dogo na kulipa faini ya Ksh 10,000 pekee sasa anaweza kurudi kwa Watoto wake,” Omondi alisema.

Chanzo: Radio Jambo