Mchekeshaji maarufu Eric Omondi alifikishwa mahakamani siku ya Jumanne ili kujibu shtaka la kusababisha fujo jijini Nairobi.
Inadaiwa kuwa mnamo Aprili 3, mwendo wa saa tano unusu mchana, kwenye barabara ya Kenyatta Avenue, Eric alizua fujo kwa njia ambayo huenda ikasababisha uvunjifu wa amani kwa kuweka kizuizi katikati ya barabara.
Polisi walisema baada ya kuweka kizuizi hicho katikati ya barabara, alikipanda na kuanza kupiga kelele na kusababisha fujo zilisababisha vikwazo na kuwasumbua watumiaji wengine wa barabara.
Omondi anadaiwa kutenda kosa hilo mnamo Aprili 3, 2023, kando ya Barabara ya Kenyatta ndani ya Wilaya ya Kati ya Biashara ya Nairobi.
Hata hivyo, alikanusha mashtaka hayo mbele ya Hakimu Zainabu Abdul na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh5,000 pesa taslimu.
Wakili wake Danstan Omari alikuwa ameiomba mahakama kumpa mshtakiwa masharti nafuu ya dhamana.
"Waheshimiwa, nakusihi umpatie mteja wangu masharti nafuu ya bondi ili aweze kuendelea na kazi yake ya kutengeneza maudhui mtandaoni," Omari alisema.
Kesi hiyo itatajwa tena Aprili 13 kwa ajili ya kusikilizwa mapema. Ametiwa mbaroni kwa mara nyingine baada ya kuandamana jijini Nairobi.
Eric alikuwa akizuiliwa katika kituo cha polisi cha Central, jijini Nairobi, baada ya kukamatwa na maafisa siku ya Jumatatu asubuhi. Alikuwa akiandamana dhidi ya gharama ya juu ya maisha wakati ambapo alikamatwa.
Huku akiwa amejihami na kipaza sauti mkononi na kamba shingoni, Eric alisimama kwenye jukwaa ambalo alisimamisha katikati mwa jiji.
"Natoka hapa nikiwa nimekufa leo ndio sauti ya Mkenya mnyonge isikike. Mimi nitajinyonga ndio mnyonge asikike," alisikika akisema.
Msanii huyo mwenye umri wa miaka 41 alisikika akiimba wimbo wa Juliani, 'Utawala' ambao unahusu kukosoa utawala mbovu.
"Niko njaa hata siezi karanga
Hoehae shaghala bhaghala
Niko tayari kulipa gharama
Sitasimama maovu yakitawala
Sitasimama maovu yakitawala," aliimba huku kundi ndogo la watu wakiwa wamesimama huku wakimtazama.
Eric alitishia kujirusha kutoka kwenye jukwaa alilokuwa amesimama juu yake na kujitoa uhai kutumia kamba iliyokuwa shingoni kama njia ya kuishinikiza serikali ya Kenya kupunguza gharama ya maisha.
"Sauti ya Mkenya lazima itasikika, sauti ya mwananchi itasikika. Mimi nitajiua hapa leo. Mimi leo nitaruka hapa na hii kamba ininyonge na nizikwe. Lakini bei ya unga itaenda chini," Eric alisikika akisema.
Kabla ya kutiwa mbaroni, mchekeshaji huyo mahiri alisikika akimweleza afisa wa polisi sababu yake ya kuandamana.
Kizaazaa kikubwa kilizuka huku maafisa hao wakijaribu kumshawishi mchekeshaji huyo ashuke kabla ya kumchukua. Milio ya bunduki ya kutupa vitoa machozi ilisikika huku umati uliokuwa umekusanyika pale ukitawanywa.