Dar es Salaam. Msanii wa filamu za vichekesho nchini Tanzania, Annastazia Exavery (22) maarufu Ebitoke amesema atashiriki shindano la Miss Tanzania mwaka 2020.
Akizungumza leo Ijumaa Februari 28, 2020 Ebitoke ametaja sababu tatu za kushiriki shindano hilo, “sababu ya kwanza mimi ni mrembo nisingependa kutumia urembo huu kwa mambo mengine yasiyokuwa na tija, ndio maana nimeamua kushiriki kwa kuwa kuna fursa nyingi.”
“Pili nataka kuwaonyesha vijana kuwa hakuna kinachoshindikana kama mtu ukiamua, hii itasaidia wengi kujiamini na kushiriki. Tatu, mimi ni msanii napaswa kubadilika. Katika urembo ni moja ya njia kuonyesha kipaji changu kingine mbali ya kuigiza filamu na vichekesho.”
Mwandaaji wa shindano hilo, Basila Mwanukuzi amethibitisha ushiriki wa Ebitoke akibainisha kuwa amerudisha fomu jana.
Msanii huyo amejizolea umaarufu kutokana na kuigiza vichekesho akitumia lafudhi ya kabila la Wahaya.
Washiriki wanapatikanaje
Pia Soma
- VIDEO: Mama wa binti kiziwi afunguka mwanaye alipo
- Jeje wa Diamond wadaiwa kufanana na wimbo wa Wizkid, Burna Boy
- Miss Rwanda apewa gari, mshahara wa kila mwezi
Amesema utaratibu huo mpya wa kutafuta warembo watakaoshiriki shindano la Miss Tanzania unatarajiwa kuanza Machi, 2020.
Amesema utaratibu huo utasaidia kuondoa changamoto mbalimbali zilizojitokeza kwa baadhi ya mawakala ambao hawakuwa waaminifu.
Amezitaja changamoto hizo kuwa ni kusimamia warembo, utoaji wa zawadi, kujaza na urudishaji fomu kwa wakati ili warembo waweze kufanyiwa usahili.
“Usahili utaanza Kanda ya kati Machi 7 jijini Dodoma, Kanda ya Kaskazini Machi 14, Kanda ya Ziwa Machi 28, Kanda ya Mashariki Aprili 4. Kanda ya vyuo vikuu Aprili 21, Kanda ya nyanda za juu Kusini Aprili 11 na Kanda ya Dar es Salaam itakuwa Mei 2, 2020,”amesema mkurugenzi huyo katika mkutano wake na waandishi wa habari.
Amesema Miss Tanzania mwaka 2020 itajikita kutangaza misitu na utalii wa asili, uhamasishaji wa kupanda miti katika kila kanda.