Nimewahi kukutana na washkaji ambao walifanya makosa makubwa sana kwenye maisha yao, makosa ambayo yaliwagharimu kila kitu walichokuwa nacho, walipoteza kazi, pesa, familia, upendo, heshima na kila kitu.
Lakini baada ya muda, walipambana na kurudi kwenye nafasi zao za zamani na kurudisha kila kitu walichopoteza. Familia zao zilirudi, kazi zilirudi, pesa zilirudi na watu waliendelea kuwaheshimu tena na sasa maisha yao yapo kama yalivyokuwa zamani, au bora zaidi ya zamani.
Swali langu ni, kwanini hili haliwezekani kwa wasanii? Yaani kwa nini msanii anapopoteza kila kitu huwa hakirudi tena?
Maisha yangu yote ya uandishi sijawahi kukutana na msanii ambaye alifulia, akapoteza umaarufu, akapoteza pesa, akapoteza aina ya maisha aliyokuwa akiishi kisha baada ya muda akapambana na kuyarudisha. Sijawahi kuona.
Chidi Benzi alikuwa ni kati ya rapa wachache Tanzania wenye mafanikio ya kisanaa nchini. Kipindi Chidi yuko juu kwenye msimamo wa muziki wa Bongofleva alikuwa anagombaniwa kama mpira wa kona, kila msanii alikuwa anataka kufanya naye kazi. Chidi kafanya kolabo na Diamond, Alikiba na karibu kila msanii ambaye aliwahi kuwa maarufu Bongo.
Lakini Chidi alipoyumba baada ya kuingia kwenye matumizi ya mihadarati ameshindwa kabisa kurudi kimuziki na kuendelea kuwa Chidi yuleyule.
Mr Nice alikuwa ni msanii mkubwa sio tu Tanzania, bali Afrika Mashariki na Kati. Ukienda baadhi ya nchi ngoma zake zinapigwa mpaka leo hii. Tena unaweza ukafika Burundi ukashangaa watu wanauza flash zenye nyimbo za Mr Nice na wanakuuliza kuhusu Mr Nice wanadhani kwa sasa Mr Nice na kina Diamond wapo kwenye levo moja.
Tena kwa mujibu wa Mr Nice mwenyewe anasema alipofulia alipoteza kila kitu. Marafiki, pesa na heshima yake kama Mr Nice. Na hata alipojaribu kurudisha ustaa wake mara kadhaa kwa kuachia ngoma ilishindikana.
Mifano iko mingi na inafanya nijiulize tena kwanini wasanii wanapopoteza thamani zao ni ngumu kuzirudisha? Kwa sababu kama kuimba bado wanajua, kama kuigiza bado wako vizuri. Yaani bado wana uwezo wa kufanya kile ambacho mashabiki wanakitaka. Kile ambacho ndicho mashabiki waliwafahamu nacho sasa kwanini wanapopoteza thamani ni ngumu kuirudisha?
Je, kuna siasa kwenye tasnia za burudani zinazosababisha wasanii hawa wasirudi kileleni? Au mizimu ya mababu wa Bongofleva na Bongomovie ikikukataa imekukataa. Tatizo ni nini? Yaani kama tulimpenda Ray C kwa sauti yake, macho yake na kiuno chake kwanini alivyopoteza nafasi yake alishindwa kurudi kileleni? Kiuno bado anacho, sauti bado anayo na macho mazuri bado anayo. Nini kinamzuia kuendelea kuimba jukwaa moja na Nandy? Nini kinamzuia kutrendi Youtube kama Zuchu?
Ndiyo maana nasema dunia inawaonea sana wasanii. Wakati wengine wasiokuwa wasanii hupata nafasi ya kurudisha walivyopoteza, mambo hayako hivyo kwa wasanii. Vitu vikienda vimeenda.