Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dk Abbasi: Serikali haitapoteza muda na wasanii wa ‘kiki’

2060ec2743baa4b1354d5d1c83d70533 Dk Abbasi: Serikali haitapoteza muda na wasanii wa ‘kiki’

Thu, 18 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

KATIBU Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi amesema serikali haitapoteza muda na wasanii wanaofanya ‘kiki’ badala ya kutumia muda wao kutengeneza kazi bora zitakazouzika ndani na nje ya nchi kwa manufaa yao na taifa.

Dk Abbasi alisema hayo juzi alipokuwa akikagua majengo ya serikali yaliyopo Kivukoni jijini Dar es Salaam akiwa ameambatana na Katibu wa Kamati ya Kitaifa ya Kuratibu Mpango wa Serikali Kuhamia Dodoma na ujenzi wa Mji wa Serikali, Meshack Bandawe.

Majengo hayo yatakabidhi kwa taasisi zinazosimamia sekta ya sanaa za Cosata, Basata na Bodi ya Filamu ikiwa ni juhudi za kuziwezesha kufanya kazi ndani ya eneo moja ili kurahisisha utoaji huduma.

“Serikali kama alivyoahidi Rais Dk John Magufuli ipo kazini kuhakikisha sekta ya sanaa inakua na kutoa mchango kwa vijana. Hapa tunapambana ili taasisi zetu hizi zipate ofisi nzuri na kutoa huduma katika sehemu moja baada ya malalamiko ya miaka mingi kuwa ziko mbalimbali, lakini baadhi ya wasanii wanaturudisha nyuma kwa kufanya kiki badala ya kazi nzuri,” alisema.

Dk Abbasi alisema serikali haitakuwa upande wa wasanii wanaovunja sheria za nchi na maadili badala yake itakua bega kwa bega na wale ambao wako tayari kufanya kazi nzuri na kuitangaza nchi vizuri.

“Jana (juzi) nililetewa habari nyingi sana wengine wamepelekana polisi, hawa wanataka kuturudisha nyuma niwaambie serikali haiwezi kuwaendekeza, nasisitiza hizi ni zama za kazi sio kiki, waambieni hao vijana anayesikia asikie hii ni sauti na amri kutoka serikali kuu,” alisisitiza.

Dk Abbasi alisema uamuzi wa taasisi hizo kukaa pamoja umepitishwa kilichobaki ni kugawiwa na kuhamia eneo hilo, huku mipango kama hiyo ikiendelea katika makao makuu ya nchi, Dodoma.

Chanzo: habarileo.co.tz