Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Diddy ni nani na anatuhumiwa nini?

Diddy Kuendelea Kusota Gerezani.png Diddy ni nani na anatuhumiwa nini?

Fri, 11 Oct 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ni nguli wa muziki aliyefanikiwa sana, Sean "Diddy" Combs, lakini sasa anakabiliwa na msururu wa tuhuma za unyanyasaji wa kingono ambazo zinaweza kuhitimisha kazi yake ya miongo mitatu.

Rapa huyo wa Marekani alikamatwa tarehe 17 Septemba na kushtakiwa kwa utumwa wa kingono na utapeli na waendesha mashtaka wa New York.

Tangu kufunguliwa mashtaka, zaidi ya madai mapya 120 yameibuka dhidi ya Combs, ambaye alikana kufanya makosa hayo. Hakimu alimnyima dhamana baada ya waendesha mashtaka kusema ni "tishio kwa jamii.”

Combs amekanusha tuhuma zote za makosa ya jinai. Lakini anakabiliwa na kazi kubwa ili kusafisha jina lake.

Kesi ya jinai inahusu nini? Combs, 54, alikamatwa katika hoteli ya New York kwa tuhuma za utapeli, utumwa wa kingono na usafirishaji wa watu kwa madhumuni ya ukahaba.

Waendesha mashtaka wa shirikisho wamemshutumu kwa "kuunda biashara ya uhalifu" ambapo "aliwanyanyasa, kuwatishia, na kuwalazimisha wanawake na watu wengine walio karibu naye kutimiza tamaa zake za ngono, kulinda sifa yake, na kuficha tabia yake".

Walisema Combs alitumia dawa za kulevya, vurugu na nguvu ya hadhi yake "kuwashawishi waathiriwa wa kike" katika vitendo vya ngono.

Wanaeleza pia waligundua bunduki, risasi na chupa zaidi ya 1,000 za mafuta ya vilainishi wakati wa uvamizi wa nyumba za Combs huko Miami na Los Angeles mwezi Machi.

Sean 'Diddy' Combs ni nani? Mzaliwa wa New York mwaka 1969, Combs alilelewa na mama yake Janice, aliyefanya kazi ya ualimu. Baba yake, Melvin, alikuwa mwanajeshi wa zamani wa Jeshi la Anga la Marekani ambaye baadaye alijihusisha na uhalifu.

Mkali huyo wa muziki alikuwa na miaka mitatu pale babake alipopigwa risasi akiwa ndani ya gari wakati wa biashara ya dawa za kulevya baada ya kutuhumiwa kimakosa kuwa ni mpasha habari wa polisi.

Mpenda michezo aliyependa muziki, Combs alipata umaarufu katika miaka yake ya ujana kwa kucheza katika video za muziki za bendi ya pop-rock ya Uingereza ya Fine Young Cannibals na katika wimbo wa soul diva wa Diana Ross kutoka Marekani.

Wakati wa masomo yake ya biashara katika Chuo Kikuu cha Howard, huko Washington DC, miaka ya mapema ya 1990, Combs alipata sifa kwa kufanya karamu za kifahari ambazo wakati mwingine zilivutia wageni zaidi ya elfu moja.

Mara nyingi alikuwa akialika wasanii mashuhuri kutumbuiza kwenye hafla hizi, ambazo zilivutia macho ya mtunzi wa muziki Andre Harrell na kumpa nafasi ya kujifunza muziki katika lebo yake ya kurikodi muziki ya Uptown Records yenye makao yake New York.

Aliacha chuo kikuu ili kufanya kazi hiyo na alifanikiwa. Combs alimsaini rapa mchanga kutoka Brooklyn anayejulikana kama Biggie Smalls na albamu ya kwanza ya Smalls chini ya Combs ikawa na mafanikio makubwa.

Msiba ulitokea mwaka 1997, pale Smalls alipopigwa risasi kwenye gari huko Los Angeles, muuaji hakuweza kupatikana lakini alihusishwa na matukio ya mauaji ambayo yaliukumba muziki wa kufokafoka katika muongo mzima.

Combs, ambaye alishuhudia tukio hilo, alitoa heshima kwa msaani wake huyo kwa kuandika wimbo wa I'll Be Missing You, ambo ulikuja kuwa moja ya nyimbo kubwa za mwaka na kisha akaingia mwenyewe kwenye kazi ya muziki.

Mbali na muziki Combs pia amejitosa katika biashara zingine, ikiwa ni pamoja na mavazi, vinywaji na utayarishaji wa vipindi vya TV. Mwaka 2022, jina lake lilionekana kwenye orodha ya mabilionea ya jarida la Forbes la Marekani.

Ni mara ya kwanza kuingia matatizoni? Mwaka 1991, Combs aliandaa hafla katika Chuo Kikuu cha New York City, ambayo ilimalizika kwa msiba. Takribani watu 5,000 walijitokeza kwenye jumba la mazoezi lenye uwezo wa kuchukua watu 2,800.

Kulitokea mkanyagano na watu tisa walikufa. Hakuna mashtaka ya jinai yaliyowasilishwa lakini jamaa za waliokufa waliwashtaki wasimamizi, chuo na jiji la New York. Combs alilipa dola za kimarekani 750,000 kama sehemu ya malipo ya dola milioni 3.8.

Mei 1999, alikamatwa kwa tuhuma za kumpiga mtendaji mkuu wa kampuni ya muziki Steve Stout kufuatia kutokubaliana juu ya video ya muziki. Combs alikiri makosa na alihukumiwa kwenda mafunzo ya siku moja ya namna ya kudhibiti hasira.

Mwaka huo huo, alishtakiwa kwa kosa la kumiliki silaha lakini baadaye akaachiliwa.

Mwaka 2015, Combs aliingia kwenye mzozo na mkufunzi wa mpira wa miguu wa mtoto wake, baada ya kutokea mabishano wakati wa mazoezi. Baadaye alikamatwa na kushtakiwa kwa shambulio baya, lakini mashtaka yalifutwa.

Unyanyasaji wa kingono

Madai ya kwanza ya unyanyasaji yalitolewa na mwanamitindo wake wa zamani, Gina Huynh, mwaka 2019 wakati wa mahojiano ya YouTube, na Tasha K. Ingawa madai hayo hayakufika kwenye vyombo vya habari vya Marekani.

Tarehe 16 Novemba 2023, Combs alishtakiwa kwa ubakaji na unyanyasaji na mpenzi wake wa zamani na mwanamuziki Cassie. Aliwasilisha malalamiko katika mahakama ya shirikisho huko New York akidai nguli huyo wa muziki alimnyanyasa kingono na kimwili wakati wa uhusiano wao wa miaka 13.

Siku moja baada ya kesi hiyo kufika kortini, pande zote mbili zilisema "zimesuluhisha kesi hiyo kwa amani," ingawa wakili wa Combs alisema kuwa suluhu hiyo "haikuwa ya kukubali makosa."

Katika wiki hiyo hiyo, wanawake wengine wawili walijitokeza. Mmoja ni Joi Dickerson-Neal, alimshutumu nyota huyo kwa kumpa dawa za kulevya na kumshambulia alipokuwa mwanafunzi wa chuo mwaka 1991. Combs alikanusha madai yote na msemaji wake aliita kesi hizo ni za "kutafuta pesa."

Mwezi mmoja baadaye, mwanamke wa nne alimshitaki, akidai aliingizwa kwenye utumwa wa kingono na kubakwa na kikundi cha watu na Combs na wanaume wengine wawili alipokuwa na umri wa miaka 17. Kujibu, Combs alikana madai yote.

Machi mwaka huu, polisi walivamia nyumba mbili za Combs huko Los Angeles na Miami. Miezi sita baadaye, alikamatwa katika hoteli ya New York na tarehe 1 Oktoba wakili Tony Buzbee anayeishi Texas alifanya mkutano na waandishi wa habari na kusema zaidi ya watu 100, wanaume na wanawake, wamemshitaki rapa huyo kwa unyanyasaji wa kingono, ubakaji na kuwatumia kingono. Buzbee aliongeza kuwa baadhi ya waathiriwa ni watu ambao walikuwa watoto wadogo wakati wa madai ya unyanyasaji huo.

Erica Wolff, wakili anayemwakilisha Combs, alisema mwimbaji huyo "kwa msisitizo anakanusha madai hayo, akisema ni "uongo na kumchafua."

Katika kazi yake ya miongo mitatu, Combs alibadilisha jina lake la kisanii mara kadhaa katika juhudi za kujaribu kuja upya. Lakini itachukua zaidi ya hilo ili kurejesha heshima yake kwa sasa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live