Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Diamond azindua tamasha la Wasafi, ‘walilia’ udhamini

Tue, 25 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kampuni ya Wasafi Media leo Jumanne Juni 25, 2019 imezindua rasmi tamasha la Wasafi 2019 linalotarajiwa kufanyika katika mikoa nane Tanzania Bara na Zanzibar.

Akizungumza kuhusu tamasha hilo, Mkurugenzi wa Wasafi Media  Naseeb Abdul maarufu Diamond amesema tamasha hilo litaanzia wilaya ya Muleba mkoani Kagera Julai 12, 2019 kabla ya kufanyika mkoani Tabora Julai 14 na mkoani Iringa Julai 20, 2019.

Diamond amesema tamasha hilo kwa mara ya mwisho lilifanyika mwaka 2018 ambapo lilifanyika katika mikoa kadhaa ikiwamo Iringa, Mtwara, Morogoro na Nairobi nchini Kenya.

Amesema tofauti na miaka ya nyuma mwaka huu tamasha hilo litakuwa na vitu mbalimbali ikiwamo elimu kwa vijana itakayotolewa kwa ushirikiano na Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania Bara (TACAIDS).

Akifafanua zaidi kuhusu tamasha hilo, Diamond amesema watataja msemo wa tamasha hivi karibuni, huku akigoma kutaja wasanii watakaoshiriki.

“Tutataja mikoa mingine kadri muda unavyoendelea, shamrashamra ya mikaoni ndiyo itakayovutia wadhamini kuendelea kudhamini kwenye mikoa mingine, hivyo kwa sasa itakuwa nane na tutaanza na maeneo hayo matatu,” amesema Diamond.

Pia Soma

Naye Mkubwa Fella ambaye ni Meneja wa WCB amesema licha ya nia njema ya Rais wa Tanzania, John Magufuli kuwapa vijana nafasi kwenye kampuni mbalimbali inaonekana bado hawajajua anataka nini.

Amesema viongozi hao vijana wamekuwa wagumu kuunga mkono juhudi za vijana wenzao.

“Tumepata taabu sana kutafuta wadhamini, kwenye kampuni ambazo tunadhani vijana ndiyo wanaongoza, lakini wameshindwa kutusapoti licha ya Rais kukubali kuwa sekta ya sanaa zinazalisha ajira nyingi.”

"Tunaomba vijana wenzetu mliopo kwenye kampuni mbalimbali msapoti kazi za sanaa, kwa sababu zinatoa ajira kwa vijana wengi na zinasisimua biashara ikiwamo mikoa ambayo tamasha hilo litapita," amesema Fella.

Chanzo: mwananchi.co.tz