Kama staa wa Bongofleva kutokea WCB Wasafi, Diamond Platnumz angekuwa ni Oliver Mtukudzi, basi angechagua kumwimbia Neria na sio Zuwena, hilo lingefanya wimbo wake kusomwa kwa muda mrefu katika vitabu vya kumbukumbu na hata kuuza zaidi.
Mtukudzi alikuwa mwimbaji maarufu wa Afro Jazz barani Afrika kutokea Zimbabwe, alifariki Januari 23, 2019 akiwa na umri wa miaka 66 huko Harare baada ya kuugua kwa muda mrefu ugonjwa wa kisukari.
Mtukudzi aliyeanza kutumbuiza mwaka 1977 alipojiunga na bendi ya Wagon Wheels, aliimba kwa lugha rasmi za taifa lake, Kishona, Ndebele na hata Kiingereza, huku akiupa muziki wake mtindo wa kipekee unaojulikana kama Tuku.
Miongoni mwa nyimbo maarufu za Mtukudzi duniani ni ule uitwao 'Neria' ambao aliuandika maalumu kwa ajili ya kutumika katika filamu (Soundtrack) inayokwenda kwa jina hilo (Neria) iliyotoka mwaka 1991.
Filamu ya Neria iliandikwa na mwandishi wa riwaya, Tsitsi Dangarembga na kuongozwa na Godwin Mawuru, inahusu misukosuko ya mwanamke mmoja (Neria) katika kitongoji cha Warren Park huko Harare, Zimbabwe ambaye alimpoteza mumewe wake katika ajali.
Mwaka 1990 Neria na Patrick walikuwa ni wanandoa wenye maisha mazuri, Patrick anapofariki familia yake hutumia mila ya Washona kumnyima Neria mali na watoto wake, huku kaka mkubwa wa mumewe akitumia hiyo kama fursa na kuridhi mali zote.
Filamu hiyo inaanza kwa kuwaonyesha Neria na Patrick wakifurahia maisha ya kisasa, wenzi hao huenda kutembelea familia yao kijijini ambako wanashawishiwa na mama yake Patrick kubaki nyumbani badala ya kukaa mjini ambapo ni mbali na familia.
Hata hivyo, Patrick anakataa wazo hilo na kusema yeye na Neria wamejenga nyumba mjini na wameamua maisha yao ni huko, kurudi mjini, gari la Patrick linaharibika kisha anatumia baiskeli kwenda kazini ndipo anagongwa na lori na kufariki dunia papo hapo!.
Ndipo Mtukudzi aliyecheza pia filamu hiyo akivaa uhusika wa Jethro, kwa sauti yake ya unyonge anatumia wimbo wake 'Neria' kujaribu kumfariji na kumtia moyo mwanamke huyo kwa kumueleza kuwa maisha yamejaa dhiki ila ajipe moyo.
“Usivunjike moyo Neria, Mungu yu pamoja nawe (Mwari anewe). Moyo wako uwe hodari, uwe hodari, Mungu yu pamoja nawe. Kifo ni wivu, hutenganisha wale walio katika upendo. Usikate tamaa dada yangu, Mungu yu pamoja nawe." anaimba Mtukudzi katika wimbo huo ulioshinda tuzo ya M-Net kama Best Soundtrack 1992.
Muigizaji wa Zimbabwe, Jesesi Mungoshi ambaye kwa mara ya kwanza alionekana katika filamu ya African Journey (1989), ndiye alicheza nafasi ya Neria kwa mafanikio makubwa.
Kwa kutambua mchango wake katika tasnia ya filamu nchini Zimbabwe, Mei 2017, Jesesi alitunukiwa tuzo ya mafanikio maishani (Lifetime Achievement) na Chuo Kikuu cha Great Zimbabwe.
Hadi sasa Neria inatajwa kama filamu iliyoingiza fedha nyingi zaidi nchini humo kwa muda wote, zinafuata filamu nyingine maarufu kama More Time (1993), Every’s Child (1996), Flame (1996) na Yellow Card (2000).
Ukisikiliza wimbo wa Diamond, Zuwena ambao ni wa pili kuachia kwa mwaka huu, ni wazi ndani yake itaiona filamu nzuri ajabu, hata video yake iliyoongozwa na Director Ivan imeonyesha hilo kwa kifupi na kuvutia wengi kutokana na uhalisia wake.
Hata hivyo, endapo wimbo huu ungetoka kama filamu rasmi, bila shaka ujumbe wake ungepokelewa kwa wigo mpana zaidi ya sasa na kutengeneza ajira nyingi zaidi kwa washiriki wote na mtiririko wa mauzo sokoni.
Kwa mujibu Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), wanakadiria soka la filamu barani Afrika linaweza kuzalisha ajira milioni 20 kila mwaka.
Meneja wa Diamond na WCB kwa ujumla, Babu Tale ambaye pia ni Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, alikuwa na wazo linaloshabiana na hilo pale alipomtafuta Director wa tamthilia ya Jua Kali, Leah Mwendamseke 'Lamata' ili kuongoza video ya wimbo huo.
"Niliwahi kumtafuta Lamata awe Director wa huu wimbo na alikuwa tayari, tatizo lilikuwa kwa mwanamuziki mwenyewe (Diamond) alidai muda wa huu wimbo kutoka bado," alisema Babu Tale muda mfupi baada ya kuachiwa Zuwena.
Kama waliweza kumfikiria Lamata anayefanya vizuri upande wa tamthili Bongo kwa sasa, basi kulikuwa na chumba za kufikiria filamu, vipi kama Lamata angeandaa filamu kisha wimbo huo ukatumika kama 'soundtrack' huku Diamond naye akihusika?
Hata hivyo, kutokana na miundombinu dhaifu ya usambazaji na uuzaji pamoja wizi uliokidhiri katika soko, ni vigumu kushawishi majina makubwa kama Diamond na wadau wengine kuwekeza katika filamu, wengi wamekimbilia tamthilia.
Kwa sasa usambazaji wa filamu kupitia programu tumishi unaanza kushika kasi Tanzania na barani Afrika, lakini ni wananchi wachache sana ambao wanamudu matumizi ya teknolojia hiyo na gharama zake. Msanii mmoja wa filamu alikaririwa akisema ni hatua muhimu katika kufikia mabadiliko lakini bado halaji wakubwa wa maudhui yao ni wananchi wa kawaida ambao hutegemea zaidi runinga.