Baada ya kuachia video ya wimbo mpya wa Shu, msanii Diamond Platnumz amezindua muonekano wake mpya, akiwa amefanya upya mtindo wa nywele zake.
Msanii huyo alipakia picha ya kuonesha mtindo huo mpya, pindi tu baada ya kutua nchini Uganda kwa ajili ya kutumbuiza Julai 14 kwenye ukumbi mmoja nchini humo, katika shoo ya ucheshi itakayoongozwa na mchekeshaji maarufu Alex Muhangi.
Hata hivyo, muonekano wa mtindo wake wa kunyoa safari hii ulivutia maoni mabli mbali kutoka kwa watu kadhaa, wakiwemo wasanii walioko chini ya lebo yake ya Wasafi.
Kwenye kutoa maoni, Mbosso alipekua mfululizo wa picha hizo na kusema kwamba picha ya nne ilimtoa mtindo wa kunyoa kama beki wa Kulia wa Manchester United, Muingereza Aaron Wan-Bissaka.
“Hilo la 4 Kama Aaron Wan-Bissaka ...” Mbosso alisema.
Kwa haraka haraka, kuangalia picha za beki huyo anayesakata ligi kuu ya premia nchini Uingereza, kweli Mbosso hakuwa mbali na maoni yake.
Mtindo wa Diamond ulijitokeza kabisa kiasi kwamba ukiangalia kwa haraka unaweza dhani ni kichwa cha Wan-Bissaka.
Hata hivyo, hii si mara ya kwanza kwa mtindo wa kunyoa wa Diamond kufananishwa na kutuhumiwa kuiga kutoka kwa wasanii wengine.
Ikumbukwe mwaka jana, Diamond alipozindua mtindo wake wa nywele za rasta, wengi walimtuhumu kwamba si mbunifu kwani aliiga mtindo huo kutoka kwa msanii wa Nigeria, Asake.
Washindani wake wa muziki wa Bongo Flava akiwemo Harmonize walikuwa mstari wa mbele kumkejeli na kumdhihaki kwa nyimbo wakimuita Asake wa Tandale kutokana na jinsi alivyoiga mtindo wa kunyoa wa msanii huyo.