Msanii wa muziki wa Bongo ambaye pia ni mkurugenzi mkuu wa Wasafi Naseeb Abdul maarufu kama Diamond Platnumz amemtunuku mzee mmoja kutoka Iringa kitika cha shilingi milioni 10 pesa taslimu za Tanzania.
Diamond amefanya hivo baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na mzee huyo kwa jina Ramadhani Mrisho aliyevuma kwenye mitandao ya kijamii kutokana na simulizi yake ya maisha ilioonekana kugusa mioyo ya watu wengi.
Mzee Makosa jinsi anavyofahamika na watu wengi, katika mahojiano na kituo kimoja cha mawasiliano cha nchini Tanzania alieleza jinsi aliingia kwenye dimbwi la umaskini kutoka kwenye utajiri aliokuwa nao.
Kwa mujibu wa chombo kimoja cha mawasiliano nchini Tanzania, Diamond Platnumz aliguswa na simulizi ya mzee huyo na alitaka sana kukutana naye kwa mazungumzo na angalau apate fursa ya kumsalamia mkononi.
Aidha baada ya kupata fursa ya kukutana na Mzee Makosa na hata kuwa na nafasi ya kuzungumza na kumsalamiamkononi jinsi alivyokuwa ametamani, Diamond Platnumz hatimaye alikabidhi kitita cha shilingi milioni 10 mzee huyo.
Baada ya kupokezwa hela hizo Mzee Makosa alisema kuwa msanii huyo alimfanyia kitu ambacho hakijawai kufanywa kwa ajili yake.
“Mimi sina maneno mengi, kwa sababu cha kusema kuhusu Diamond sikioni kikija kichwani. Alichokifanya alichokifikiri ni yeye. Kafanya kitu ambacho watu wengi hawajafanya. Basi nibaki tu kumshukuru yeye na kuwashukuru wanaomuunga mkono katika harakati zake.” Alisema Mzee Makosa katika mahojiano na kituo cha redio cha Wasafi.