Staa wa Bongo Fleva, Naseeb Abdul Juma 'Diamond Platnumz' kwa mara ya kwanza ameonyesha nyumba yake ya kifahari aliyonunua Johannesburg nchini Afrika Kusini.
Mbali na kuwa na vyumba vingi na samani za kupendeza, nyumba hiyo aliyoianika kupitia ukurasa wake wa Instargram, pia ina bwawa la kuogelea (swimming pool) ndani yake.
"Ni vizuri sana kurudi nyumbani!" aliandika chini ya video iliyoonyesha nyumba hiyo ambayo alipakia kwenye Instastori zake.
Katika video hiyo, baadhi ya machawa wake walionekana wakistarehe katika vyumba tofauti vya kulala ndani ya nyumba hiyo.
Diamond alitumia fursa hiyo kutangaza kuwa baada ya kupumzika Afrika Kusini kwa muda wataendelea na ziara yake ya muziki katika mataifa mbalimbali ya Bara la Ulaya na Afrika.
"SA kwa siku kadhaa! Kisha Paris, kisha London, kisha shoo ya Wembley OVO Rena, kisha Malawi," alitangaza.
Kwa muda mrefu sasa kumekuwa na ripoti kuwa staa huyo wa Bongo mwenye umri wa miaka 32 anamiliki jumba la kifahari nchini Afrika Kusini. Msanii huyo hata hivyo hakuwahi kuonyesha jumba hilo kikamilifu hapo awali.
Afrika Kusini ndiko anakoishi mpenzi wake wa zamani Zari Hassan pamoja na watoto wao wawili, Tiffah Dangote na Prince Nillan. Mwanasoshalaiti huyo kutoka Uganda amekuwa akiishi huko kwa miaka kadhaa huku akiendesha biashara zake.
Kuna uwezekano mkubwa kuwa Diamond aliamua kutafuta makao huko Afrika Kusini ili kupata fursa ya kuwa na kipindi kizuri pamoja na familia yake kila mara anapofanya ziara katika nchi hiyo.