Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Diamond, Rayvanny watoka kifungoni

37998 Pic+basata Diamond, Rayvanny watoka kifungoni

Wed, 23 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) limewafungulia wasanii Naseeb Abdul 'Diamond' na Raymond Mwakyusa 'Rayvanny’ kuendelea na Tamasha la Wasafi.

Katika taarifa iliyoitolewa jana Jumanne Januari 22, 2019 na kusainiwa na Katibu wa Basata, Godfrey Mngereza, inasema wamefikia uamuzi huo baada ya kupokea maombi kadhaa ya kukiri kosa na kuomba msamaha kutoka kwa wasanii hao na kampuni ya Wasafi (WCB).

"Baada ya kuyapitia maombi hayo ambayo pia yaliwasilishwa kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza na kwa kuzingatia jukumu la Basata la kusimamia, kuendeleza na kukuza wasanii na sekta ya sanaa nchini. Baraza limeamua kuwaruhusu wasanii tajwa kuendelea na shughuli za sanaa," inasema taarifa hiyo.

Hata hivyo, taarifa hiyo imesema Baraza litaendelea kufuatilia kwa karibu utendaji wa wasanii hawa na kampuni ya Wasafi ili kuhakikisha wanazingatia maadili, sheria, kanuni na miongozo ya kazi za sanaa nchini.

Naye Diamond katika ukurasa wake wa mtandao wa Instagram, alishukuru kwa uamuzi huo na kueleza kuwa sanaa ni kazi hivyo ni wajibu kuilinda, kuipenda na kuithamini.

Pia, alimpongeza Rayvanny kwa kuwa huru na kueleza kuwa ni wakati sasa wa kuachia nyimbo yao mpya mwaka huu.

Rayvanny naye hakuwa nyuma kwani aliandika: "Mungu ni Mwema".

Wakati meneja wao, Babu Tale aliandika neno moja tu: " Asante'.

Rayvanny na Diamond, walifungiwa Desemba 18, 2018 kutofanya maonyesho ndani na nje ya nchi kwa muda usiojulikana wakituhumiwa kufanya makosa mbalimbali tangu kuanza kwa tamasha la wasafi ikiwamo kuimba wimbo wa Mwanza ambao umefungiwa.



Chanzo: mwananchi.co.tz