Staa na CEO wa lebo ya WCB Wasafi Diamond Platnumz kwa mara ya kwanza amezungumza kwa kukiri kwamba wakati Rayvanny anaondoka kwenye lebo hiyo, walikuwa na mazungumzo ya baridi sana na hata kutofautiana naye vikali.
Diamond alizungumza hayo kwenye jukwaa la Acces lililowakutanisha wadau wa sanaa jijini Dar ambapo, Rais huyo wa Bongo Fleva, alikuwa miongoni mwa wazungumzaji na alipokuwa akizungumza kuhusu fursa za mitandao ndipo alipomgusia Rayvanny.
Alisema kuwa japo walipishana kidogo katika Kiswahili na maelewano, baadae walinyoosha mambo na urafiki ukarudi.
Aliweka wazi kuwa anajihisi fahari sana kwani hata baada ya kutoka WCB, Rayvanny bado anazidi kutamba ambapo juzi ameshinda tuzo ya Afrimma katka kitengo cha mwanamuziki bora wa kiume kutoka ukanda wa Afrika Mashariki.
Alisema kuwa fahari yake inaongezeka hata zaidi baada ya Rayvanny kumshirikisha katika kibao chake cha kwanza tangu kuondoka WCB, ‘Nitongoze’ ambacho kinazidi kufanya vizuri kwenye majukwaa ya kidijitali kote duniani.
"Rayvanny kama mnavyojua alindoka WCB namshukuru Mungu ananiheshimu, tulitofautiana kidogo kama unavyojua mnapoachana kunakuwa na vitu wakati mwingine inaweza visiende sawa lakini namshukuru Mungu tulimaliza vizuri. Kama unaona ameenda WCB anafanya kazi Next Level anafanya kazi na Mziki na wimbo wake wa kwanza amenishirikisha mimi," alisema Diamond.
Diamond alisema kuwa hata baada ya Rayvanny kuondoka WCB, bado amesalia pale kama rafiki na mshikadau tu wa karibu na kusifia ukomavu wake.