Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Diamond, Hamisa wanapiga fedha ndefu

Misa Mond Diamond na Hamisa

Sat, 12 Nov 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Wasanii wa muziki na filamu duniani kote wamekuwa wakijizolea mamilioni ya wafuasi katika mitandao ya kijamii kutokana na umaarufu wa kazi zao na hata mtindo wao wa maisha una mchango mkubwa kwenye hilo.

Hii hutoa fursa kwa wasanii kupata dili mbalimbali za kutangaza (influencer marketing) bidhaa au huduma zinazotolewa na kampuni, taasisi au mashirika katika jamii fulani ambayo wasanii husika wana nguvu ya ushawishi.

Nchini Tanzania wasanii kama Diamond Platnumz, Hamisa Mobetto, Idris Sultan, Nandy, G Nako, Wema Sepetu, Lulu, AY, Zuchu, Jux, Rosa Ree, Navy Kenzo, Joti na Shilole ni miongoni mwa wasanii wanaokula matunda kutokana na idadi ya wafuasi wao mtandaoni.

Wakizungumza G Nako na Rosa Ree wamesema hii ni fursa kwa wasanii kuingiza kipato kupitia sanaa yao na kuwataka wasanii kusimamia chapa zao vizuri kwa kutengeneza picha yenye ushawishi katika eneo fulani la kazi yao ili kuvuta dili nyingi.

Mfano Diamond aliweka wazi kwa mwezi mmoja anapokea wastani wa Sh200 milioni kwa kutangaza bidhaa na huduma mbalimbali, dili ambazo anazipata kutokana na ushawishi wake na mitandao yake ya kijamii ndio hasa wamekuwa akiitumia kufanya kazi hiyo.

Utakumbuka Diamond ndiye msanii anayeongoza Tanzania kuwa na wafuasi wengi kwenye mitandao ya Instagram (milioni 15.4), Facebook (milioni 6.8), Twitter (milioni 1.2), TikTok (milioni 2) na YouTube (milioni 7.1). Upande wa Instagram anafuatiwa na Wema Sepetu, Hamisa Mobetto na Shilole.

Rosa Ree ambaye amekuwa akitangaza bidhaa za pombe na nywele, amesema fursa ni nzuri kwao ila inategemea zaidi msanii husika ameijenga vipi chapa (brand) yake mbele ya jamii na wanaohitaji kumtumia.

“Ni kitu kikubwa kwa sababu sanaa ni ajira, pale ambapo kampuni zinakufuata zinataka kufanya kazi na wewe ina maana sanaa yako ina ushawishi katika jamii. Kitu hiki kimewapa mafanikio makubwa wasanii wengi na nina furahi na mimi ni miongoni mwa hao, nimepata dili nyingi,” amesema.

“Kwa kifupi hiki kitu ni kikubwa kwa wasanii kwani kimeweza kutengeneza mlango mwingine wa kuingiza kipato upande wetu. Shukrani kwa mashabiki wameniweka sehemu ambayo imenifungulia milango mingi,” amesema Rosa Ree.

Anasema kampuni yoyote inapomtazama msanii na kuona ana ushawishi (influence) na anaweza kuwaongezea kitu, ndipo wanamuita mezani na kumpa dili, hakuna msanii anayepewa dili kwa bahati mbaya, lazima awe na kitu ambacho unakiweka mezani na yeye.

“Hivyo wasanii wote unaona wanafanya kazi na kampuni mbalimbali, ni kwamba wanaweza kushawishi jamii kuhusu bidhaa na huduma za kampuni husika, na pia wanaweza kuwaongezea kiasi kikubwa cha mauzo ndio maana wanatoa hizo dili,” amesema Rosa Ree.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Serengeti Bytes ambaye ni Mtaalam wa Masoko Mtandaoni (digital marketing), Kennedy Mmari anasema msanii ni lazima aonyeshe ushawishi kwa kile anachotangaza, nje ya umaarufu wake mtandaoni.

“Hapa kuwa na wafuasi ni kitu kimoja, lakini kuwa na ushawishi katika sekta fulani ndio kitu cha muhimu zaidi, sasa ili kupewa kazi lazima uwe na uwezo wa kushawishi lile soko ambalo linahitajika. Kama umepewa kazi ya ubalozi wa kampuni ya pombe lazima uonyeshe unaweza kuwashawishi wanywaji,” anasema Kennedy.

Kwa upande wa G Nako ambaye anatangaza mavazi, huduma za televisheni za kulipia, mitandao ya simu na pombe, amesema wasanii kupata dili hizo kwa wingi sasa ni ishara kuwa tasnia inazidi kukua.

“Ni kitu kingine ambacho inaonyesha ‘industry’ inatanuka, kampuni nyingi zinawatumia wasanii kama ‘influencer’ na hiyo inaonyesha kwamba wasanii ni watu ambao wanaaminika na kuweza kuzishika hizo ‘brand’ na kwenda nazo mbele,” anasema.

Je, kampuni hizo zinapokuwa zinamfuata G Nako huhitaji nini hasa kutoka kwake na kwa kuzingatia nini? Rapa huyo anasema cha muhimu na taswira (image) ambayo tayari msanii anakuwa ameitengeneza ambayo inaendana na bidhaa anayoenda kuitangaza.

“Ni namna msanii anavyokuwa ‘anajibrand’, na brand nyingine zinakuwa zinakuona, na kila brand inakuwa anamuhitaji msanii kwa namna ambavyo anakuwa amejiweka mbele ya jamii,” anasema.

“Kwa mfano mimi nimewejiweka kama mtu ambaye napenda mavazi, kwa hiyo ni rahisi kumshawishi mtu ambaye anatengeneza brand zake na mavazi kuniona. Au ni mtu ambaye anapenda kusafiri, ni rahisi kwa mtu ambaye anahusika na vitu vya safari kama hoteli kuniona na kunipa dili,” anasema G Nako.

Lakini baadhi ya wasanii wamekuwa wakilalamika kuwa chapa kubwa zimekuwa zikitoa dili hizo kwa upandeleo, jambo hilo linapigwa vikali na Reuben Ndege (Ncha Kalih), Afisa Ubunifu na Mkakati Clouds Media Group, ambaye anasema ili msanii apate tangazo, anapaswa kufahamu kila chapa ina misingi yake na misimamo yake.

Anasema chapa fulani ikitaka kuzungumza (kuwauzia bidhaa au huduma) na watu wa aina fulani, itamtafuta mtu au msanii ambaye ana kitu fulani ambacho wale watu wanakitambua au wana kikubali.

“Kwa hiyo sasa hivi kama nina chapa ya mafuta ya kupikia, nitamchukua Shilole, na kweli ukimuweka kwenye tangazo mtu anakubali kwa sababu huyu dada anamuona kwenye mambo ya chakula,” anasema Ncha Kalih akiongea na Times FM.

“Unajua zamani hayo mambo yalikuwa yanatolewa kishkaji tu, lakini sasa hivi kuna uwajibikaji, kama ni kampuni inayouza vinywaji, kinarudi nini?, aidha tunakuza chapa au tunapata fedha kwa bidhaa tunazouza, kwa hiyo kama nimekupa milioni 400 unatakiwa kuuza zaidi ya milioni 400 au kukuza chapa yangu kwa thamani ya milioni 400,” anasema Ncha Kalih.

Utakumbuka kwa mwaka 2021 msanii wa Pop Marekani, Ariana Grande mwenye wafuasi milioni 338 alikuwa ndiye msanii analiyelipwa fedha nyingi katika kutangaza kupitia ukurasa wake wa Instagram akiwa anachukua Dola 1.51 milioni, wastani wa Sh3.5 bilioni.

Hiyo ni kwa mujibu wa kampuni ya kimataifa ya masoko, Hopper HQ kutoka nchini England ambayo tangu mwaka 2017 imekuwa akitoa orodha ya watu matajiri duniani kwenye mtandao wa Instagram.

Chanzo: Mwanaspoti