Unaukumbuka vipi mwaka 1998? Dr Dre kumsaini Eminem kwenye label ya Aftermath Entertainment Machi 9, mwaka huo au milipuko ya mabomu kwenye balozi za Marekani, Dar es Salaam, Tanzania na Nairobi, Kenya, Agosti 7, 1998?
Snoop Dogg, kuondoka Death Row Records, Januari 26, 1998, ndiyo inakupa kumbukumbu ya mwaka? Je, kifo cha gwiji wa muziki, Frank Sinatra Mei 14, 1998? Usiniambie unachokikumbuka ni ile diamond ring ya uchumba ambayo David Beckham aliichomeka kwenye kidole cha Posh Spice, Januari 25, 1998.
Format ubongo sasa. Upokee habari yenye maana kubwa iliyojiri mwaka 1998. Mwanafunzi Lusajo Mwaikenda Israel, alihamia Shule ya Sekondari Makongo, kidato cha pili, akitokea Mbezi Beach Sekondari, Dar es Salaam.
Lusajo, akiwa Makongo, akakutana na wanafunzi wawili, Feruzi Rehani Mrisho na Noely Michael Kapinga. Kitu kimoja kiliwaunganisha haraka, Lusajo, Feruzi na Noely; Muziki. Wakaunda kundi lililoitwa O-Rang U-Tang.
Misele ya talent shows ndani ya Jiji la Dar, ikawafikisha O-Rang U-Tang, Shule ya Sekondari Jitegemee. Kuna mwanafunzi wa Jitegemee aliwakosha O-Rang U-Tang. Jina lake ni David Selestin Nyika. Wakaunga undugu, timu ikawa ya mtu nne; Lusajo, Feruzi, Noely na David.
Noely, alisoma Makongo lakini hood yake Kimara. Ruaha Galaxy ni chimbo la Kimara ambalo Noely alikuwa akikutana na mchizi anaye-rap kibabe sana. Anaitwa Rashid Hamis Kaombwe. Yakafanyika mazungumzo, Rashid aka-join the team. Goma likawa pentagon. Pembe tano; Noely, Feruzi, David, Lusajo na Rashid.
Kikao kazi kilichofanyika maskani Sinza, Dar mwaka 1999, kiliibua azimio la kutoendelea na jina la O-Rang U-Tang. Mtu tano wote ni manunda. Kwa nini wasijiite kanda hatari ya manunda? Wakaiweka kwa English; Dangerous Zone of Nundaz. Kifupi Daz Nundaz.
Noely akataka majukwaa yamtambue kama Critic, David “Daz Mwalimu” au “Daz Baba”, Feruzi “Ferooz”, Lusajo “Sajo wa Daz” na Rashid ni La’Rhumba.
Ni mapitio ya kundi bora kabisa, Daz Nundaz, kuelekea induction ceremony yao ya Bongo Flava Honors, itakayofanyika Julai 19, 2024, Warehouse Arena, Oysterbay, Dar. Ni siku isiyo na mfano. Sugu The Jongwe, atakuwa mwenyeji wa shughuli.