“Hakuna shida, tunamuachia Mungu”. Ni kauli ya baadhi ya wakazi wa Tabata, Mtaa wa Matumbi C, jijini Dar es Salaam, wanaoomboleza kifo cha Athuman Semfukwe (32), aliyeuawa kwa kuchomwa kisu mara tatu tumboni.
Athuman, aliyejizolea umaarufu na kufahamika na wengi kutokana na kazi ya kupiga muziki (DJ) kwenye sherehe mitaani maarufu vigodoro ameuawa Februari 3, 2024.
Kijana aliyetajwa kwa jina moja la Evans anashikiliwa na Jeshi la Polisi akituhumiwa kwa mauaji hayo.
Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Yustino Mgonja simu yake ilipokewa na mtu aliyejitambusha kuwa msaidizi wake akieleza ni kweli taarifa hizo zimeshawafikia ofisini.
“Ofisi yetu haizungumzii matukio kama haya, mtafute Kamanda wa Kanda Maalumu anayepaswa kuzungumzia suala hili,” amesema.
Alipotafutwa kamanda wa kanda hiyo, Jumanne Muliro hakupatikana kuzungumzia tukio hilo.
Katika tukio hilo, wapo waliojeruhiwa walipokuwa wakimwokoa DJ huyo, wakiwamo Rajab Omary aliyeumizwa kichwani na Bahati Shaban aliyechomwa kisu tumboni upande wa kushoto.
Athuman aliyekuwa na ofisi ya vifaa vya elektroniki mtaani hapo ameuawa akiendelea kupiga muziki kwenye tafrija iliyofanyika mtaani hapo.
Athuman aliyezikwa Februari 5, 2024 katika Makaburi ya Tabata Dampo, ameacha mke na watoto wawili, mmoja akisoma darasa la nne na mwingine hajamaliza mwaka tangu alipozaliwa.
Walioshuhudia tukio hilo wanadai chanzo cha DJ kuchomwa kisu ni kukatisha muziki ghafla kutokana na tatizo la kukatika umeme. Baadhi ya waliohudhuria tafrija hiyo walitaka muziki upigwe hadi asubuhi.
Bahati aliyenusurika katika tukio hilo amesema licha ya siku hiyo kutokea tatizo la umeme, lakini wapo watu waliokuwa hawaki muziki uzimwe.
“Watu walikuwa wanataka itafutwe namna hata kupata jenereta muziki uendelee kupigwa hadi asubuhi, ndipo ugomvi ulipoanza Evans akiongozwa na kikundi chake,” amedai.
Omary, ambaye pia amejeruhiwa amedai Evans na kikundi chake cha watu wanane walikuwa wanatumia ubabe.
“Hata wakati Athuman anapelekwa hospitali, baadhi yao walikuwa wanawafutilia wakileta ghasia, jambo lilosababisha wahudumu wa Zahanati ya Tabata kujifungia ndani,” amedai.
Mkazi wa eneo hilo, Samira Said ameziomba mamlaka husika kuchukua hatua za haraka dhidi ya mtuhumiwa.
Amesema Athuman hakuwa mtu wa makundi. Seleman Semfukwe, baba wa Athuman amesema, “Juzi alikuwa amealikwa, lakini baada ya kuonekana kuna shida ya umeme alikubaliana na mwenye shughuli wasiendelee na alimlipa,” amedai wakati akifungasha vifaa vyake ikiwemo kompyuta, ndipo Evans alimvamia na kuanza kumchoma kisu.
“Athuman akaanguka, Evans akachomoa kisu na kukimbia, wengine walipoona wakashtuka na kuanza kumkimbiza Evans na kumuacha kijana wangu akigaagaa,” amesema.
Amesema wakati wengine wakimfukuza Evans, baadhi walikodi bajaji kumpeleka Athuman hospitali.
Ameeleza kijana wake alifariki dunia njiani akipelekwa Hospitali ya Amana. Bahati Abdallah, mke wa Athuman amesema taarifa za mumewe kuzidiwa na kupelekwa hospitali alizipata usiku akiwa kwa wazazi wake alikokuwa anauguza mtoto wake.
Amesema atamkumbuka kutokana na upendo aliokuwa anampa katika kipindi chote cha miaka mitatu walichoishi pamoja.
“Miasha yetu tulikuwa tunaishi Karakata, huku ni kwa wazazi wake na ofisini kwake muda mwingi alikuwa anashinda huku, hakuwahi kuwa na shida na mtu, basi ni kazi ya Mungu,” amesema.