D Voice anahusishwa na kwenye tetesi za mahusiano ya mapenzi na Lulu Diva. Msanii huyo wa WCB Wasafi, amefungukia stori ya kuhusishwa kuwa kwenye mahusiano na muimbaji Lulu Diva, ambapo wanatajwa kuonekana pamoja mara nyingi.
D Voice amekanusha taarifa hiyo kwa kudai kuwa yeye na Lulu Diva wanafahamiana vizuri kama wasanii na watu wa karibu. Licha ya kukanusha, D Voice ameonyesha kuvutiwa na taarifa hizo. Akiongea kwa kuchangamka, amesimulia jinsi ambavyo yeye na Lulu Diva wanavyofahamiana.
“Lulu Diva ni mtu wangu wa karibu sana, ikitokea bahati ya kuwa pamoja, umri ni namba tu. Lulu sio mkubwa kihivyo, umri ni namba tu. Mtume alioa mkewe anamzidi miaka zaidi ya ishirini. Lulu ni chombo kile, bonge la pisi kali, akinielewa safi tu”. Alisema.
D Voice ameelezea mitazamo yake kuhusu kuingia kwenye mahusiano na Lulu Diva kwa kusema ikitokea nafasi wamekubaliana kuanzisha mapenzi yao, haoni kama WCB ni kikwazo kwake kwani hata viongozi wake hawawezi kuchukulia kama ni kitu cha ajabu. “Mapenzi yangu sio ya WCB, mtu atapendana na mimi, sio lebo nzima, kikubwa ni kufanana tu, yeye akiona mimi sina baya, niko avaialable kwa ajili yake”.
Tetesi za D Voice kuingia kwenye mahusiano na Lulu zinatajwa kupamba moto zaidi siku ilipokuwa inarekodiwa video ya ‘Wanawake Moto’. D Voice anatajwa kumpeleka Lulu location, na taarifa za couple hiyo zikasambaa kwa kasi. Hata hivyo, D Voice amekataa kumsindikiza Lulu location.
“Mara nyingi tunakutana, sikumsindikiza Lulu location, nilienda siku ya wanawake kumsapoti dada Queen Darlin ambaye alikuwa hapo eneo la tukio, nilikwenda kumsapoti dada yangu.”
Ukiweka kando tetesi za kutoka kimapenzi na Lulu Diva, kwa sasa D Voice anatamba na wimbo wake ‘Zoba’, aliouachia Aprili 12. Wimbo huo mpya umekuja miezi 5 baada ya D Voice kutambulishwa na WCB, kisha kuwa na albamu iliyoshikiria nafasi ya kwanza kwa miezi mitano mfululizo.