Mchekeshaji wa muda mrefu wa vichekesho nchini, Zimwi ambaye amekuwa akiumwa kwa muda mrefu sasa amepata mwanga wa kupata nafuu ya maradhi yake baada ya wasanii wenzake kuungana kumsaidia.
Kwa takribani mwaka na miezi kadhaa Zimwi amedai amekuwa akisumbuliwa na maradhi ya moyo na tumbo na kisha ripoti ambayo imetoka hivi karibuni ni kuwa ana tatizo pia la ugonjwa wa kichocho.
Msemaji wa Chama cha Bongo Comedy, Mkono wa Mkonole alisema kuwa wameamua kufikia hatua hiyo ya kuungana na kutoa taarifa za wazi kuwa wamekuwa wakimsaidia Zimwi kwa muda mrefu na sasa imefikia wakati wanaomba pia Watanzania wasapoti matibabu yake.
“Tumekuwa tukimuhudumia Zimwi kwa zaidi ya mwaka sasa, matibabu yake kwa mwezi ni 700,000 kwa hiyo tulipofikia ni kwamba hatuwezi tena peke yetu na tunaomba wadau, serikali na mashabiki kuwashika mkono,” alisema.
Kwa upande wa Zimwi mwenyewe aliongeza kuwa: “Kimsingi nawashukuru sana wenzangu kwa jitihada kubwa ambayo wamekuwa wakiifanya juu yangu, kwa sababu peke yangu nilishindwa kujihudumia baada ya kupambana muda mrefu.
“Niwaombe pia Watanzania na wadau kunisaidia kupambana na hali yangu hii. Kwa sababu sina uwezo tena wa kupambana mwenyewe.”