Miezi kadhaa baada ya muigizaji Will Smith, kumzaba kofi la moto mchekeshaji Chris Rock kwa kile alichosema ni kumtania mkewe mbele ya macho yake wakati wa hafla ya tuzo za Oscars za mwaka huu, mchekeshaji huyo sasa anasema kuwa alifuatwa ili kushiriki katika tuzo hizo za mwaka 2023 lakini amekataa.
Kulingana na jarida la Marekani, New York Post, Chris Rock alikataa mwaliko huo kwa kusema kwamba kurudi katika ukumbi wa tuzo za Oscars ni kama kurudi kwenye eneo la tukio baya.
“Mcheshi huyo mwenye umri wa miaka 57 aliambia hadhira ya kipindi cha vichekesho cha Phoenix Jumapili iliyopita kwamba aliombwa kuhudhuria hafla ya mwaka ujao lakini alikataa fursa hiyo,” New York Post waliripoti.
Machi 27, 2022, Smith, aliushangaza ulimwengu alipopanda jukwaani na kumpiga kofi la uso Chris wakati akisherehesha Tuzo za Oscar baada ya kufanya mzaha kuhusu mke wake, Jada Pinkett Smith, kuhusu kuonekana kama "G.I. Jane” kutokana na upara wake.
Tukio la Smith kumpiga kofi hilo lilizua gumzo kubwa mitandaoni kote duniani na baadaye Smith alionekana kuomba radhi kwa kitendo kile huku akijitetea kwamba alikuwa anaitetea na kuilinda familia yake.
Smith alifichua kwamba kichekesho cha Rock kuhusu mkewe kilikuja kwake kama kejeli kutokana na hali ya afya inayomkumba Jada ambayo inasababisha kupotea kwa nywele, hali ambayo inalmazimu kunyoa upara ambao Rock alitumia kama uwanja wa kichekesho chake pasi na kujua.
"Kwa hivyo nitakuambia, Chris, nakuomba msamaha, tabia yangu haikukubalika, na mimi huwa hapa wakati wowote unapokuwa tayari kuzungumza," Smith alisema kwa huzuni inayoonekana, ila mpaka sasa Smith hajawahi kulizungumzia suala hilo hadharani.